Frederick Sumaye
SHAMBA la Frederick Sumaye lililoko Kisarawe
mkoani Pwani, liko hatarini kuchukuliwa na halmashauri ya wilaya hiyo na
kuligawa upya, kutokana na Waziri Mkuu huyo mstaafu kushindwa
kuliendeleza.
Habari zilizothibitishwa na viongozi kadhaa wa
Wilaya ya Kisarawe, zimeeleza kuwa shamba la Sumaye lililoko eneo la
Vikurunge Kata ya Kiluvya, ni miongoni mwa mashamba yaliyoko kwenye
orodha ya kunyang’anywa na kugawiwa upya.
Hata hivyo mwenyewe amesema kuwa hana taarifa ya mpango huo wa halmashauri kuwanyang’anya watu mashamba.
“Sijui chochote na nipo kanisani, Sijui hata hiyo notisi ya halmashauri kutaka kunyang’anya mashamba,” alisema na kukata simu.
Chanzo cha habari kilisema “Huu ni mpango wa
halmashauri na tayari imeshatoa tangazo tangu mwaka jana. Ilitoa siku 60
tangu Desemba 30 mwaka jana kwa wamiliki wake kuyaendeleza mashamba
hayo, baada ya hapo yatanyang’anywa,” chanzo cha habari kilieleza na
kuendelea;
“Mheshimiwa Sumaye ni miongoni mwa wamiliki
hao, yeye shamba lake lina zaidi ya ekari 40 na lipo eneo la Vikurunge
Kata ya Kuluvya. Ameshindwa kuliendeleza kwa kipindi cha miaka mitano
sasa.”
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makurunge, Jocline
Mfuru alikiri Sumaye kumiliki eneo kubwa eneo hilo, lakini alisema
taarifa zaidi zipo halmashauri ndio ambao wanajua zaidi kwani hata yeye
mwenyewe ni mgeni katika nafasi hiyo ana mwezi mmoja tu tangu awepo hapo
baada ya mtendaji wa awali kuondolewa.
“Sina muda mrefu katika nafasi yangu na
ninatambua notisi ya siku 60 ya wale ambao hawajaendeleza mashamba
lakini siwezi kuzungumzia zaidi kwani sina taarifa za kutosha,” alisema
Mfuru.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe, Yona
Maki alithibitisha kutekelezwa kwa operesheni hiyo na kusema kuwa sasa
wapo katika hatua ya kufanya tathamini.
Akiwa amekwepa kuthibitisha
kama shamba la Sumaye nalo litanyang’anywa, Maki alisema, “Ni kweli
Sumaye anamiliki eneo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na
amejenga nyumba ya kuishi.”
Aliendelea “Lakini, kujenga nyumba hakutoshi
kueleza kuwa shamba hilo limeendelezwa. Tunapitia nyaraka zinazohusu
umiliki wake na kuona kama lipo kwenye mpango huo au la.”
Maki
alisema uchunguzi unaofanyika dhidi ya Sumaye ni pamoja na kujua aliomba
kumilikisha eneo hilo kwa ajili ya shughuli gani na kuangalia iwapo
kile alichoombea ndicho anachokitekeleza.
“Nipe muda niweze kujua alimilikishwa kwa
ajili ya utekelezaji wa jambo gani na kama hicho alichoombea ndicho
anachokifanya,” alisema Maki.
Maki alifafanua kuwa hatua ya kupitia upya
umiliki wa mashamba wilayani humo na uendelezwaji wake, inafanyika kwa
mujibu wa sheria ya vijiji na miji namba 4 na 5 ya mwaka 1999.
“Sheria hiyo inaeleza kuwa mtu ambaye amemilikishwa shamba au
kiwanja na kushindwa kukiendeleza katika kipindi cha miaka mitano,
umiliki wake utafutwa na kurudishwa halmashauri,” alisema Maki.
Mkurugenzi
huyo wa halmashauri alisema kuwa eneo hilo kuna watu ambao
wamemilikishwa maeneo makubwa ambao wameshindwa kuyaendeleza hali na
kulingana na utekelezaji wa sheria hiyo notisi hiyo haitawahusu wale
ambao wameanza uendelezaji hata kama watakuwa hawajafanya hivyo kwa
asilimia mia moja.
“Kuna wawekezaji kama wale wa mradi wa kilimo
cha miti aina ya mbono ambao wamepewa hekta 9,000 na tayari wameanza
uendelezaji hivyo hao hawataguswa” alisema na kuwa hakutakuwa na mjadala
kwa wale ambao watashindwa kufanya hivyo ndani ya muda ambao umetolewa.
No comments:
Post a Comment