Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi
KUNDI la majambazi limeteka mabasi matano, mojawapo likiwa la wanajeshi wa Rwanda na kupora abiria na kisha kuwacharaza viboko.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi zimeeleza kuwa tukio
hilo lilitokea juzi alfajiri katika Kijiji cha Kikoma kilichoko Kata ya
Rusahunga, Wilaya ya Biharamulo.
Mashuhuda wameeleza kuwa majambazi hao wakiwa
na silaha za kivita, waliweka kizuizi na kuyasimamisha magari hayo moja
baada ya jingine kisha, kuwashusha abiria na kuwapora kila kitu.
“Baada ya kuwapora abiria, waliamua
kuwacharaza viboko mmoja baada ya mwingine, kisha kutokomea
kusikojulikana,” alisema shuhuda mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina
lake liandikwe na kuongeza:
“Magari yaliyotekwa ni Toyota Hiace, gari moja ni la wanajeshi waliokuwa wakitokea Rwanda kwenda Dar es Salaam.”
Diwani wa Kata ya Rusahunga, Amon Mizengo alisema tukio hilo lilihusisha majambazi wanane waliokuwa na bunduki sita za kivita.
Diwani
huyo alisema magari yaliyotekwa yalikuwa yakitokea Ngara na Benaco na
kuwa baada ya abiria kuporwa kila kitu, waliamuriwa kuendelea na safari
zao.
Kamanda Kalangi alisema jeshi la polisi
linaendelea na uchunguzi... “Ni kweli taarifa za awali zilieleza kuwa
moja ya magari hayo lilikuwa na wanajeshi wa Rwanda, lakini mimi ndiyo
naelekea katika eneo la tukio.”
Msemaji wa Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ),
Kanali Kapambala Mgawe alisema hana taarifa za tukio hilo wala ujio wa
askari hao wa Rwanda nchini. “Sina taarifa zozote, lakini inawezekana
wakawa wageni wa Kanda ya Magharibi.”
Hata hivyo, alisema katika hali ya kawaida, wageni wengi wa jeshi wanaokuja nchini, hutumia usafiri wa ndege.
Tukio hilo limetokea siku chache, baada ya
wananchi wa vijiji vya mpakani wilayani Ngara, kuanza kuendesha
operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu kwa kile walichodai ni Serikali
kushindwa kuwasaidia.
Wananchi hao wamelalamikia wahamiaji hao
haramu wenye makundi makubwa ya mifugo, kukingiwa kifua na baadhi ya
viongozi wa Serikali.
Wananchi hao wa vijiji vinavyopakana na nchi
za Burundi na Rwanda, kwa nguvu zao, walikamata makundi makubwa ya
ng’ombe na kuwaweka chini ya ulinzi.
Katika kutuliza jazba za wananchi hao, Mkuu wa
Wilaya ya Ngara Constantine Kanyasu aliwataka wananchi kusitisha
operesheni hiyo akiwaeleza kuwa Serikali inajipanga kuondoa tatizo hilo
bila kukiuka sheria.
Eneo hilo limekuwa likiripotiwa matukio kadhaa
ya ujambazi na mwaka 2007 wabunge wanaotokea maeneo hayo waliomba
kuwekwa kwa minara ya mitandao ya simu ili kuwa na mawasiliano.
No comments:
Post a Comment