WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta amesema kwamba anazo sifa za kuwa Rais wa Tanzania na
anafikiria kugombea 2015, iwapo dhamira yake itaridhika na mazingira na
upepo wa kisiasa wa wakati huo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili juzi, Sitta alitaja mambo kadhaa aliyoeleza kuwa ni ishara ya
kukubalika kwake, ikiwamo kuteuliwa na marais wote wanne; Julius
Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete katika
nyadhifa mbalimbali ikiwamo ya uwaziri.
Kauli ya Sitta imekuja baada
ya kuwapo kwa minong’ono ya baadhi ya wananchi kumtaja kuwa miongoni mwa
watu wanaoweza kujitokeza kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka
2015.
“Ni faraja kusikia watu wakinizungumzia kuwa
ninazo sifa (za kuwa Rais). Nami ninaamini ninazo sifa. Wakati
utakapofika nitajipima. Kama hali hii itaendelea, basi nitaona ni vizuri
nigombee,” alisema Sitta ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge.
Hata hivyo, alisema hana mkakati wowote sasa wa
kuendesha harakati za kutafuta nafasi hiyo kwa udi na uvumba kama baadhi
ya wengine (bila kuwataja), wanavyofanya... “Sina sababu za kuanza
kutafuta support (kuungwa mkono) wala uundaji wa kamati za ushawishi kwa
watu sasa,” alisema Sitta.
Badala yake alisema atasubiri hadi muda wa
kuchukua fomu za kugombea utakapofika ndipo atakapojitathmini na kusema
endapo atabaini kuwa Watanzania wengi wanamuunga mkono, atachukua uamuzi
wa kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Aitahadharisha CCM
Waziri huyo
aliwahadharisha wanachama wa CCM kwamba wasipokuwa makini, wanaweza
kuipoteza nafasi hiyo ya urais na kwenda kwa vyama vya upinzani.
Alionya kuwa iwapo watamteua mtu asiye mwadilifu,
Watanzania hawatamchagua na badala yake watampa nafasi hiyo mgombea
yeyote kutoka vyama vya upinzani.
Alisema Watanzania wengi wana werevu wa kutosha
kujua watu ambao ni mafisadi na ambao wamekuwa wakitumia fedha zao chafu
kwa ajili ya kutaka wakubalike mbele ya macho ya Watanzania. Alisema
suala la uadilifu ni moja ya vigezo muhimu ambayo CCM wanapaswa
kuvizingatia ili kupata ushindi wa kiti cha urais mwaka 2015.
“Ndiyo maana nilipokuwa mbele ya Tume ya Kukusanya
Maoni ya Katiba niliweka wazi kwamba Tanzania tunahitaji kuwa na jopo
la kuhoji viongozi na wananchi wawe na fursa ya kuwachambua,” alisema
Sitta.
Alisema kinachohitajika Tanzania ni mfumo ambao utajenga mazingira ya kuwa na viongozi waadilifu katika ngazi zote.
Alisema hali hiyo itaepusha mfumo unaoonekana sasa
wa viongozi kwenye ngazi mbalimbali kuishi kiujanjaujanja, kujinufaisha
na kutojali athari kwa uchumi wa nchi na Watanzania kwa ujumla.
Alitoa
mfano wa uzembe uliofanywa na viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA), ambao umesababisha Bandari ya Dar es Salaam kupoteza uaminifu kwa
nchi mbalimbali zinazopakana na Tanzania.
Alisema uzembe huo umeifanya Bandari ya Dar es
Salaam kuingiza Sh38 bilioni kwa mwezi tofauti na Mombasa ambayo
inaingiza Sh300 bilioni.
CCM ni imara?
Akizungumzia
miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM, mbunge huyo wa Urambo Mashariki alisema
anaamini kwamba chama hicho kimefanya vizuri licha ya kuchafuliwa na
watu wachache kutokana na tabia zao za ufisadi.
Alisema CCM kinakubalika kutokana na sera zake, lakini pia sifa
za kada mmojammoja zinawavuta Watanzania wengi kwenye chaguzi
mbalimbali.
Alitoa mfano wa CCM kuendelea kuwa na wabunge
wengi, alisema hali hiyo inatokana na wale wanaogombea kuwa na heshima
ya kipekee kwa jamii.
“Ninaamini CCM bado itaendelea kuwa na wabunge
wengi japo imetetereka wakati fulani kutokana baadhi ya makada
kutuangusha,” alisema Sitta.
Alisema anaamini kuwa sasa CCM itajisafisha na
kuondokana na sifa hiyo mbaya kupitia uongozi wa sasa ambao wamepewa
jukumu la kukirejeshea heshima.
Rushwa kwenye chaguzi
Akizungumzia
kuhusiana na rushwa kwenye uchaguzi, Sitta alisema ipo haja ya sheria
kuweka wazi suala hilo kutokana na kuingiliana na ukarimu wa kawaida
ambao ni utamaduni ya Waafrika kutafsiriwa kama ni kosa.
No comments:
Post a Comment