Maofisa ardhi wadaiwa kuuza Hifadhi Sanapa


KAMATI ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Mazingira imeijia juu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwauzia  wawekezaji wa njemaeneo yaliyo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Sanapa na imeagiza maofisa waliojiingiza katika kashfa hiyo kuchukuliwa hatua mara moja.

Imesema Januari 22, mwaka huu,  itamwita Waziri wa Ardhi, Nyumba na  Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ili atoe  maelezo kwa nini wizara yake imeingia katika hujuma ya kugawa maeneo ya Hifadhi ya Taifa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alisema hayo jana alipokuwa akielezea uamuzi wa wajumbe wa kamati yake baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Sanapa na kujionea jinsi ilivyovamiwa na kuathiri maisha ya wanyama waliomo kwenye hifadhi hiyo.

“Tumekubaliana kwamba Jumanne (kesho) hii tutakutana jijini Dar es salaam na kutamwita Waziri Tibaijuka atueleze kwa nini wizara yake imegawa eneo la Hifadhi ya Sanapa bila kuliarifu Bunge na kimsingi hatukubali kuona Sanapa inahujumiwa,” alisema Lembeli.

Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama alisema wajumbe wa kamati yake pia watataka kujua kwa nini Waziri Tibaijuka hajawachukulia hatua maofisa wa wizara yake waliouza maeneo hayo.

yanayodaiwa kuuzwa kwa wawekezaji katika Hifadhi ya Sanapa ni yanayodaiwa kuwa yatakuwa ya  kilimo cha mashamba makubwa ya miwa, kiwanda cha chumvi kilichokando ya ufukwe wa Bahari ya Hindi na hoteli ya kitalii ambayomwekezaji wake hakutajwa jina lake.

Uvamizi mwingine uliopo katika hifadhi hiyo ni wananchi kutumia mwanya wa wawekezaji hao kujihalalishia kulima mashamba yao na kujenga makazi ndani ya eneo la hifadhi hiyo.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole  Sendeka  alisema maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi wamekuwa chanzo cha migogoro kwenye maeneo mengi nchini kwa sababu ya kujiingiza katika mambo ya rushwa.

“Sanapa si hifadhi ya majaribio, ni hifadhi kamili na kutokana na kuwa ni pekee ambayo wanyama huishi mbugani na kuvinjari kwenye fukwe za Bahari ya Hindi, kamati haitakubali kuona inahujumiwa,” alisema Ole Sendeka.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema katika kamati itahakikisha kuwa inatumia rungu lake kuokoa Hifadhi ya Sanapa.

No comments:

Post a Comment