Askari JWTZ anaswa na pembe za ndovu Arusha

Pembe za ndovu. 

GARI aina ya Toyota VX linaloelezwa kuwa mali ya Serikali limekamatwa na polisi likiwa limebeba pembe za ndovu.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa gari hilo lilikamatwa juzi saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Kigongoni katika Mji wa Mto wa Mbu, wilayani Manyara baada ya gari hilo kupinduka.

Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya Jeshi na Polisi zimeeleza kuwa askari wa jeshi hilo aliyekuwa akiendesha gari hilo anashikiliwa na polisi.
Uchunguzi umebainisha kuwa ndani ya gari hilo kulikuwa na meno ya tembo na watu wengine watatu ambao walikimbilia porini na baadhi ya nyara hizo.

Habari hizo zimedai bado kuna utata kuhusu gari lililokuwa likitumiwa na maofisa hao kwa kuwa kibao cha namba za gari hilo kinasomeka kwa namba za kiraia lakini vioo vimechorwa namba za Serikali, huku Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa akisema pia kulikuwa na namba za JWTZ.

Kulingana na taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, kukamatwa kwa gari hilo kulitokana na Askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Hifadhi ya Ziwa Manyara kudokezwa na raia wema.

Inaelezwa kuwa baada ya askari hao kudokezwa, walianza kufuatilia nyendo za maofisa hao ndani ya hifadhi na walipogundua wanafuatiliwa, gari hilo liliongeza mwendo kuelekea Mji wa Mto wa Mbu.
Hata hivyo, kutokana na mwendokasi wa gari hilo na kutokuwa wazoefu kulinganisha na Askari wa Tanapa, gari la maofisa hao lilipinduka lilipofika Kijiji cha Kigongoni nje kidogo ya Mto wa Mbu.

“Baada ya kupekuliwa lilikutwa na pembe mbili za ndovu na uchunguzi wa awali umethibitisha maofisa waliokimbia walifanikiwa kutoroka na pembe nyingine tatu,” kilidokeza chanzo hicho.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulitokana na wananchi kumtilia shaka yeye na wenzake gari lao lilipopata ajali kwa kitendo cha watu wawili waliokuwepo kwenye gari hilo kuonekana wakihamisha mizigo  na kukimbilia porini.

“Matairi mawili ya gari yalipasuka lakini ajabu ni kwamba wananchi walipojitokeza kusaidia majeruhi, wawili kati yao walinyanyua mizigo isiyojulikana na kukimbilia porini huku wakimwacha mwenzao aliyevaa sare za jeshi akisubiri garini,” alisema mtoa taarifa wetu.

Kwa mujibu wa mashuhuda, wakati wa ajali hiyo, mtuhumiwa alikuwa amevaa jaketi la JWTZ pamoja na suruali ya jinsi akiwa na bunduki aina ya Rifle.
Katika msako uliofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi, pembe mbili zaidi  za ndovu zilikutwa zikiwa zimefichwa karibu na eneo la ajali.

Mkurugenzi mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini akasema hana taarifa kamili kwani yuko Tanga na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

“Ni kweli nimearifiwa juujuu tu, nasubiri taarifa kamili lakini nimeambiwa tu hilo gari lilipinduka wakati wakifukuzana na askari wetu, lakini mnaweza mkapata taarifa zaidi polisi,” alisema Kijazi.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema hajapata taarifa hiyo, hivyo asingeweza kutolea maoni kwa namna yeyote.

 

“Kaka ndiyo kwanza nasikia. Lakini nyie angalieni tu vyanzo vyenu kama ni sahihi, haina shida,” alisema Kanali Mgawe.

Kamanda wa Polisi Mkoa  wa Arusha, Liberatus Sabas alipopigiwa simu jana alikataa kuzungumza chochote akisema yuko safarini na yeye ndiye anayeendesha gari, hivyo kiusalama asingeweza kuongea na simu.

“Ninaendesha gari na utaratibu wangu ni kwamba ninapoendesha gari huwa siongei na simu na wewe unavyoendelea kuniongelesha hujali usalama wangu,” alisema Kamanda Sabas.

Alipoulizwa na gazeti hili apigiwe simu baada ya muda gani, Kamanda Sabas alijibu, “Ni safari ndefu sana naomba uniache kwa sasa.”

Tukio la kukamatwa kwa gari hilo limekuja takriban wiki mbili baada ya polisi wawili wa Mkoa wa Kagera kukamatwa na vipande 17 vya pembe za ndovu wilayani Serengeti.

Mbali na tukio hilo, katika kipindi hichohicho, polisi wengine wawili waliuawa na wananchi katika Kijiji cha Kasheshe wilayani Ngara wakituhumiwa kukutwa na vipande saba vya pembe za ndovu.

Katika tukio hilo lililotokea Januari 6, 2013, askari mmoja wa polisi alinusurika kifo baada ya wananchi kuchoma gari walilokuwa nalo aina ya Toyota Noah baada ya kuwakuta na pembe za ndovu zenye uzito wa kilo 34.

Matukio yote hayo yamekuja kukiwa na ongezeko la ujangili katika hifadhi mbalimbali nchini huku wananchi na wadau wa utalii wakiwanyooshea baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola kuhusika.

Kamati ya Bunge yatoa neno

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema kukamatwa kwa askari huyo anayeaminika kuwa wa JWTZ kunaashiria kuwa hali katika hifadhi za taifa nchini ni tete na ni matokeo ya Serikali kupuuza ushauri uliokuwa umetolewa na kamati yake.

Alisema hayo jana alipokuwa akiwaeleza wajumbe wa kamati yake waliokuwa katika ziara ya kutembelea Tanapa.
Alisema alipigiwa simu na wakazi wa Mkoa wa Manyara wakiomba Kamati yake iingilie kati kushauri njia za kufanya ili kukomesha ujangili huo.

“Nimepigiwa simu nyingi usiku wa kuamkia leo, tukio hili la kukamatwa kwa wanajeshi, limewakatisha tamaa kabisa wananchi, wanalia wanataka mimi na kamati yangu tuingilie kati,” alisema Lembeli.

Alisema kukithiri kwa ujangili wa meno ya Tembo kila siku kunatokana na Serikali kupuuza ushauri uliokuwa umetolewa na kamati yake ambapo matukio kama haya yasingekuwepo.
Hata hivyo, alipotakiwa kueleza ni ushauri gani uliowahi kutolewa na kamati yake, Mwenyekiti huyo alisema hawezi kusema hadharani kwa sababu itasababisha wahalifu wajiimarishe zaidi. Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walieleza kusikitishwa kwao na watu waliopewa dhamana ya kulinda maliasili za nchi kujihusisha na ujangili huo wa kuwaua Tembo na kusafirisha pembe zao.

 

Alipotakiwa kuwapa taarifa rasmi wabunge hao juu ya tukio hilo, Kijazi (Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa), alisema ofisa mmoja wa JWTZ mwenye cheo cha Sajenti amekamatwa na meno ya

Tembo huku wengine wakikimbia.

Alisema gari walilokuwa wakisafiria lilikuwa na namba tatu tofauti za usajili, moja ya jeshi, nyingine ya Serikali, yaani STK na namba nyingine ni ya kiraia.

Alisema ofisa huyo wa jeshi alikamatwa baada ya gari walilokuwa wakisafirishia meno hayo kupinduka katika harakati za kukimbia wasikamatwe, ambapo askari waliotoroka walikimbia na baadhi ya meno ya tembo.

Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alieleza kuwa hali hiyo inatokana na kushindwa kwa Serikali hadi watu wazito wanajiingiza katika ujangili wanavyotaka na kuhujumu maliasili za nchi.

“Serikali ya CCM sasa imechoka kuna kila haja wananchi kuiondoa madarakani kwa sababu imeachia hadi askari wa jeshi wanaingia katika hifadhi kuwaua Tembo na kusafirisha pembe,” alisema Mchungaji Msigwa.

No comments:

Post a Comment