Asha Musa (katikati) akiwa na bibiu yakew na mtoto wake.
SIKU hizi kuna watu wanasema; “Ni heri ukutane
na mnyama mkali kama, simba au chui unaweza kusalimika, kuliko kukutana
na binadamu, kwani anaweza kukudhuru.”
Maneno haya yanatokana na unyama wanaofanyiana
wenyewe kwa wenyewe. Kila siku tunasikia unyama unaofanywa na binadamu,
leo utasikia baba wa miaka 45 amemnajisi mtoto wa miezi minne, mke
amemkata na shoka hawara wa mume wake, majambazi wameua familia nzima na
mambo kama hayo.
Hayo yanadhihirishwa na mkasa wa Aisha (siyo jina
lake halisi), aliye na ulemavu, ambaye hajiwezi kwa lolote bila
msaada wa mtu.
Hata hivyo, pamoja na hali aliyonayo, bila chembe ya huruma, Aisha amekuwa mwathirika wa unyama wa binadamu, baada ya kubakwa.
Binti huyo anaishi katika Kijiji cha Ntisi, Kata
ya Bicha, umbali wa kilometa tano kutoka Kondoa Mjini, eneo ambalo
hakuna usafiri mwingine unaoweza kukufikisha zaidi ya bodaboda.
Katika kijiji hicho hakuna asiyemfahamu binti huyo
kutokana na hali yake na historia ya maisha yake, ambayo inasikitisha
kila aliye karibu naye.
Kwa takriban miaka 21, binti huyo ameishi na
bibi yake aitwaye Mwajabu Haji, lakini sasa familia hiyo imeongezeka,
baada ya Aisha kujifungua mtoto, ambaye ni zao la kubakwa. Mtoto huyo
sasa ana umri wa miaka sita.
Ukifika nyumbani kwao utamkuta Aisha amekaa katika kiti chake maalumu cha mbao, alichotengenezewa na bibi yake.
Hana kiungo chochote mwilini mwake kinachoweza kufanya kazi zaidi ya mdomo wake.
Hata
hivyo, inzi humwingia mdomoni na kutoka, wakirukaruka katika mwili wake
wapendavyo, kwani binti huyo hawezi kuwafukuza kwa kuwa mikono yake
haifanyi kazi.
Umbile lake lilivyo
Zaidi ya
kuzungumza, Aisha hawezi kufanya shughuli yoyote kutokana na kuwa,
mikono na miguu vimejipindapinda. Tumbo lake limesogea upande wa kushoto
na kichwa kulia.
Mara nyingi anapoongea mikono hupata nguvu ya
ajabu ambapo huanza kurukaruka huku na kule kwa kuwa hawezi kuizuia,
hujigonga na kujiumiza katika sehemu mbalimbali.
Mikono hiyo haina
nguvu ya kuweza kubeba kitu chochote au kufukuza wadudu wanaotambaa
katika mwili wake hasa inzi kutokana na vidonda vilivyojaa.
Historia ya maisha yake
Aisha
alizaliwa mwaka 1990 Musoma, mkoani Mara akiwa na ulemavu. Alipofikisha
umri wa mwaka mmoja, alipelekwa kwa bibi yake mzaa mama, baada ya baba
yake kukataa kuendelea kumlea. “Kwa kweli ninamshukuru Mungu na bibi
yangu kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa katika historia yangu, nimekutana na
changamoto nyingi, lakini hakunitupa au kuninyanyapaa,” anasema na
kuongeza:
“Ninamhurumia bibi kwa kuwa pamoja uzee, lakini
hana budi kubeba, jukumu la kututafutia riziki ya kila siku kwa ajili
yangu na mtoto wangu.
Natamani ningekuwa na uwezo hata wa kumsaidia kuosha vyombo,” anasema Aisha.
Anasimulia
kuwa, kwa mujibu wa bibi yake, mama yake alilazimika kumrudisha
kijijini hapo, baada ya baba yake kutaka wamchinje au wamtupe.
Aisha anaeleza kwamba, kwa kuwa mama yake alikuwa
akiipenda ndoa yake, hakuwa tayari kumtupa au kumuua badala yake
alimpeleka kwa bibi yake, ili kuokoa uhai wake.
“Mama yangu mzazi aliwahi kupigwa na baba, huku
akitishiwa kuachwa endapo atanilea, ndugu zake baba walimshauri
anitupe,” anasema Aisha.
Anaongeza kuwa, hajawahi kukutana na baba
yake mzazi, lakini anadai kuwa anamfahamu kwa jina la David Chacha
akieleza kuwa anafanya kazi ya upishi jeshini huko Monduli.
Mama yake
mzazi ambaye pamoja na kumrudisha kwa bibi yake, alikuwa akifika
kijijini hapo mara kwa mara kumjulia hali, hata hivyo alifariki mwaka
2011.
Alivyobakwa mpaka kupata ujauzito
Kutokana
na umbile lake lilivyo na pilikapilika za bibi wa Aisha katika kutafuta
riziki, ilimchukua miezi saba bibi huyo kugundua kuwa mjukuu wake ana
ujauzito.
Bibi huyo anasema kuwa aligundua kuwa mjukuu wake ana ujauzito, wakati tayari imeshafikisha miezi saba.
Anaeleza kuwa alibaini kuwa matiti ya Aisha yakiwa yamejaa, ndipo alipomchunguza vizuri na kugundua kuwa ni mjamzito.
Mwajabu (Bibi wa Aisha) anasimulia kuwa
alipomuuliza Aisha kutaka kujua aliyempa ujauzito na jinsi alivyoupata,
alishangaa kwa kuwa, aliyempa ujauzito huo ni binadamu mwenye akili
timamu.
Anasema kuwa baada ya hapo alimpeleka mjukuu wake
kliniki, lakini pia alimtafuta kijana aliyempa ujauzito, ambaye
anafahamika kwa jina moja la Mashoto.
“Bibi mimi huingiliwa na mwanamume aitwaye
Mashoto, ila kaniambia nisimtaje, ikitokea nimemtaja basi atanichinja
ndiyo maana nilinyamaza, nikiogopa kuchinjwa,” anaeleza Mwajabu
akimnukuu Aisha alipotaka kujua aliyempa ujauzito.
Baadaye, bibi huyo
aliamua kwenda polisi kutoa taarifa, ambapo aliambiwa atoe Sh500, ili
mgambo watumwe kwenda kumkamata Mashoto.
Mgambo hao walifanikiwa kumtia ndani mtuhumiwa,
lakini baada ya siku chache alitoka na kuwaomba waifute kesi kwa madai
kuwa atamtunza binti huyo na mtoto atakayezaliwa.
“Sijawahi kupata
msaada wowote kutoka kwa mwanamume huyo tangu wakati huo, mpaka sasa
mjukuu wangu ametimiza miaka sita, lakini nimeamua kumuachia Mungu,”
anasema Mwajabu.
Akisimulia kuhusu ujauzito wake, Aisha anasema kuwa alipitia wakati mgumu, kwani hakuwa na msaada wa kupata mahitaji muhimu.
Anasema
kuwa mtu pekee aliyemfanyia wema mbali na bibi yake ni daktari
aliyemhudumia wakati akijifungua, akisema kwamba kamwe hawezi kumsahau.
“Sikutaka kupoteza kumbukumbu ya daktari yule,
Novatus Kasongo, nikaamua kumpa jina hilo mtoto wangu, alikuwa mwema na
alinisaidia,” anasema Aisha.
Msaada anaohitaji
Hatima ya
familia hiyo ipo chini ya bibi Mwajabu ambaye hana shughuli nyingine
anayoweza kufanya zaidi ya kilimo cha jembe la mkono. Lakini pia hawezi
kulima mashamba ya mbali kwa kuwa ana jukumu la kumuangalia mjukuu wake
yake huyo na kumfanyia kila kitu ikiwemo kumtoa nje na kumrudisha ndani
jioni.
“Ninaishi kwa kutegemea kilimo cha jembe la mkono,
lakini pia siwezi kulima sana kwa kuwa nina jukumu jingine la
kumwangalia mjukuu wangu na mtoto wake,” anasema na kuongeza:
Pia siwezi kwenda mbali kwa kuwa inabidi
nimwangalie mjukuu wangu, ambaye hajiwezi kwa chochote, hapa nilipo
ninaumwa kifua kwa sababu ya kumbeba kila siku wakati wa kumtoa nje na
kumrudisha ndani jioni,” anasema.
Anaongeza: “Ninaomba wasamaria wema
wanisaidie chakula, nguo na kitukuu changu kusoma, hivi sasa umri wake
anatakiwa kuwa shuleni lakini sina uwezo. ninaomba wanaoguswa na hili
wanihurumie.
Pia ninaomba msaada wa kiti maalumu kwa ajili ya mjukuu wangu, akiwa na kiti itanipunguzia kazi kwani nitakuwa nikimsukuma tu.”
No comments:
Post a Comment