Ndugu wa aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya
Sekondari Juhudi, Gongo la Mboto, marehemu Jacqueline Matiko, wakitoka
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam mara
baada ya uchunguzi wa mwili, uliofanyika juzi.
RIPOTI ya madaktari kuhusu uchunguzi wa sababu
za kifo cha kutatanisha cha Jacqueline Matiko, mwanafunzi wa kidato cha
pili katika Shule ya Sekondari Juhudi iliyopo Gongo la mboto,
inatarajiwa kutolewa leo.
Mwanafunzi huyo alikutwa amekufa maji Januari
Mosi mwaka huu katika Hoteli ya Southern Beach, iliyopo Kigamboni jijini
Dar es Salaam.
Kulingana na maelezo ya mmoja wa madaktari
walioufanyia uchunguzi wa kitabibu mwili wa marehemu juzi katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili, ripoti hiyo ataiwasilisha polisi kwa ajili
ya hatua zaidi.
“Kazi yetu (madaktari) tulimaliza juzi na kesho
ripoti itakuwa tayari” alisema daktari huyo ambaye hata hivyo hakutaka
jina lake litajwe kwa maelezo kuwa si msemaji wa hospitali hiyo.
Pia
alisema hawezi kuingia kwa undani kuhusu ripoti hiyo lakini alisema
uchunguzi kufuatia utata juu ya kifo hicho umekamilika.
Kamanda wa Polisi Temeke, Englebert Kiyondo,
alikiri kukutwa kwa mwili wa mwanafunzi huyo na kwamba kutokana na
madai ya ndugu zake, mwili huo umefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) na jeshi lake linasubiri ripoti ya madaktari.
“Tunasubiri ripoti ya madaktari ili tuweze kujua ukweli,” alisema na kuongeza kuwa ni mapema mno kuzungumzia suala hilo.
Alisema utata wa kifo hicho unatokana na baadhi ya wafanyakazi wa hoteli kuwa marehemu alifia katika bwawa la kuogelea.
Baba wa mwanafunzi huyo, Mussa Matiko
alithibitisha kupewa taarifa na madaktari waliofanyia uchunguzi mwili wa
mwanafunzi huyo kuwa ripoti watapewa leo.
Utata huo unatokana na ndugu wa marehemu ambao
walikuwa nao siku ya tukio, kupingana na maelezo ya wafanyakazi wa
hoteli hiyo kuwa marehemu alifia katika bwawa la kuogelea na inadaiwa
siku ya tukio marehemu alipotea katika mzingira ya kutatanisha akiwa
hotelini hapo.
“Alitafutwa sehemu zote bila kuonekana na tulirudi
tena kesho yake asubuhi na kuulizia na walitueleza kuwa hajaonekana na
hata bwawa wamebadilisha maji na kuweka dawa,” alisema bibi wa marehemu
Saida Hussein.
Alisema kuwa walipoondoka katika eneo la hoteli
kwa lengo la kwenda hospitali tofauti kumtafuta, walikutana na baba wa
mtoto katika Kivuko cha Kigamboni na kurudi tena hotelini.
Alisema katika eneo hilo waliwakuta askari polisi
huku mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa kwa shuka, pembeni ya bwawa la
kuogelea.
“Inashangaza wenzangu walikuja wakaambiwa hajaonekana lakini
tuliporudi tena baadaye, bila kutarajiwa tukaukuta mwili. huku askari
polisi wakiwa wameitwa kuja kuuchukua,”Musa Matiko.
Baadhi ya kinamama ambao walishiriki katika kuosha
mwili wa marehemu mwanafunzi huyo waliliambia Mwananchi kuwa kuna kila
dalili kuwa binti alibakwa kisha kunyongwa kwani shingo yake ilikuwa
imevimba na pia alikuwa na michubuko sehemu za siri.
“Amebakwa kisha akanyongwa hilo halina ubishi ila
tusubiri ripoti za daktari,” alidai bibi wa mtoto huyo, Saida wakati
anatoka katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Muhimbili
baada ya kuosha mwili wa marehemu, ambaye alizikwa katika makaburi ya
Gongolamboto, mwishoni mwa wiki iliyopita.
No comments:
Post a Comment