Polisi wakiwa wanamshambulia aliyekuwa mwandishi wa Channel 10,Daudi Mwangosi
ASKARI walioshiriki katika operesheni ya
kusambaratisha mkutano wa Chadema mkoani Iringa na kusababisha kifo cha
mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi,
wanalalamika kwamba hawajalipwa posho zao zinazofikia Sh12,150,000.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema
kiasi hicho cha fedha kilipaswa kulipwa kwa askari 27 waliotokea mkoani
Dodoma kwa malipo ya Sh45,000 kwa siku kwa kila askari. Askari hao
walikaa Iringa kwa muda wa siku kumi. Mmoja wa askari hao alisema hadi
kufikia jana askari wote waliotoka mkoani Dodoma, walikuwa hawajalipwa
posho zao za operesheni hiyo iliyofanyika Septemba mwaka jana. “Kutoka
hapa tulienda (Iringa) askari 27, askari wa kawaida 24, masajenti wawili
na inspekta mmoja. Wakati tunaondoka tuliambiwa kwamba posho zetu
ambazo ni Sh45,000 kwa siku wangetutumia,” alisema askari huyo na
kuongeza;
“Tulikaa Iringa kwa siku kumi, hivyo kila askari
aliyekwenda kwenye operesheni ile, alipaswa kulipwa Sh450,000. Lakini
bahati mbaya sana, baada ya kutokea mauaji yale hakuna mtu aliyelipwa
mpaka sasa. Vocha zimeendikwa lakini hazijatolewa.”
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema hana taarifa kuhusu malipo
hayo hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni mgeni mkoani humo.
“Hapa Dodoma mimi nimekuja siku za hivi karibuni
na hilo suala la askari kutolipwa posho zao silijui na sifahamu kama
kweli walikwenda huko ulikosema,” alisema Kamanda huyo na kuongeza: “
Naomba nipe muda zaidi nifuatilie ili kujua ukweli wake. Lakini pia
nikuombe uwasiliane na mwandishi mwenzako aliyeko hapa Dodoma ili iwe
rahisi mie kuwasiliana naye kuliko kuzungumza kwa simu tu.”
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2, mwaka jana
wakati polisi hao waliodaiwa pia kutoka Mikoa ya Morogoro na Mbeya,
wakiwatawanya wafuasi wa Chadema, waliokuwa kwenye mkutano wa ndani
katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.
Askari hao walikwenda mkoani Iringa kushirikiana na wenzao katika kudhibiti, mikutano ya Chadema.
Mwangosi aliuawa kwa bomu alipokuwa akiwajibika
katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufanya mikutano ya ndani
ya kuimarisha chama.
Ripoti ya kamati iliyoundwa na Baraza la Habari
Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuchunguza kifo
hicho, ilisema Mwangosi aliuawa kwa makusudi na polisi chini ya
usimamizi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
No comments:
Post a Comment