Mikopo
duni inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB), imetajwa kuwa ni moja ya mambo yanayochangia wanafunzi wa kike
kujihusisha na vitendo vya ukahaba.
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari St. Mathew, Thadei Mutembei, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE, juzi jijini Dar es Salaam.
Alisema serikali inapasa kuliangalia kwa makini suala hilo, kwani mikopo
wanayopata wanafunzi hao ni midogo, ambayo haitoshelezi mahitaji yao
muhimu.
Mutembei alisema wanafunzi hao si kama wanapenda ‘kujiuza’, bali
wanalazimika kufanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha na kwamba,
mikopo, ambayo wanapata imekuwa haiwatoshelezi.
Aliiomba serikali kuwapa kipaumbele watoto, ambao wazazi au walezi wao
wana kipato duni katika mikopo, kwani hao ndio ambao wanataabika zaidi,
hivyo wanahitaji msaada mkubwa na kwamba, wale wenye uwezo waachwe
wajisomeshe wenyewe.
Pia aliiomba serikali kutoangalia shule anayotoka mwanafunzi wakati wa
kutoa mikopo, kwani shule si kigezo cha mwanafunzi kupata au kukosa
mkopo, badala yake iangalie hali halisi ya maisha ya mwanafunzi.
Katika hatua nyingine, wahitimu wa kidato cha sita wa shule hiyo
wameiomba serikali kuweka mitaala madhubuti katika elimu ili kufanya
wanafunzi wawe na maendeleo mazuri katika masomo yao.
Walitoa maomba hayo katika mahafali ya nane ya shule huyo kupitia risala
yao kwa mgeni rasmi Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki.
Balozi Kagasheki, ambaye aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Wizara hiyo,
Dornatus Kamamba, aliahidi kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na
wanafunzi hao.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment