Polisi wa mkoa wa Arusha wakiangalia Nyara za Serikali zilizokamatwa katika eneo la Mateves Ngaramtoni jijni Arusha
SHEHENA za nyara za serikali zinazokadiriwa kuwa
za thamani ya mamilioni ya fedha zimekamatwa na polisi eneo Mateves,
Ngaramtoni ya Chini mjini hapa.
Nyara hizo ni meno mawili ya Tembo, ngozi, vichwa
na pembe za wanyamapori mbalimbali zikiwamo Tembo, Simba, Viboko, Nyati,
Nyumbu, Ngiri, Mbwamwitu na wanyama wengine ambao thamani ya vitu hivyo
haijajulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa ni kutokana na taarifa za raia wema
kuhusu kuwapo mtu anayejihusisha na biashara ya uwindaji bila vibali vya
mamlaka husika.
Sabas alisema baada ya kumhoji mtuhumiwa alidai
nyara hizo zimekuwa zikikusanywa tangu mwaka 2007 na zimekuwa
zikihamishwa kutoka eneo moja hadi jingine kwa nyakati tofauti.
Katika hatua nyingine, Sabas alikanusha taarifa
zilizochapishwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwa polisi
inashirikiana na majangili kuwinda na kufanikisha mtandao wa ujangili
nchini.
“Nataka niseme polisi haishirikiani na wahalifu
kufanya uhalifu, hayo yanaweza kufanywa na polisi binafsi lakini siyo
taasisi na wahusika wanachukuliwa hatua kama wahalifu wengine,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa wa Kikosi cha Kupambana na
Ujangili Kanda ya Kaskazini, Deodanus Makene alisema thamani halisi ya
nyara hizo haijajulikana na itatolewa baada ya wataalamu kufanya
tathmini. Makene alisema nyara zilizokamatwa zinaruhusiwa katika
uwindaji wa kitalii, ila mtuhumiwa hana vibali vinavyoonyesha mazingira
alikozipata.
Tukio hilo lilivuta hisia za watu wa eneo hilo
kutokana na wingi wa nyara hizo ambazo hazikuenea kwenye gari kubwa la
polisi aina ya Scania ambalo hutumika kuwapelekwa watuhumiwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment