Wabunge wamchongea Mkurugenzi kwa JK

Rais wa Tanzania, Dk.Jakaya Kikwete.

Wabunge na Madiwani wa Wilaya ya Nzega wamemchongea Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete wakimtaka kuondoka naye kwa kile walichodai kuwanywesha wananchi maji machafu kwa kipindi cha miaka mitano.

Wabunge hao ni wa Nzega (CCM),  Dk. Hamis Kigwangalla na Sellemani Zedi wa Bukene (CCM), ambao walimtaka Rais Kikwete kuondoka na mkurugenzi huyo, Kyuza Kitundu, kwa kuwa alikwishakataliwa na Baraza la madiwani.


Dk. Kigwangalla alisema Mkurugenzi huyo hatakiwi katika halmashauri hiyo kutokana na kutumia miaka mitano kuwanywesha maji machafu wananchi huku uwezekano wa kupata maji safi na salama ukiwepo.


Alisema Baraza la madiwani lilikwishapitisha azimio la kumkataa katika vikao vyake lakini utekelezaji haujafanyika hali ambayo inaendelea kuwaumiza wananchi.


“Mheshimiwa Rais hapa tuna kero kubwa ya maji, wananchi wanakunywa maji machafu, yananuka na yana wadudu; yote haya ni kwa sababu ya mkurugenzi kushindwa kufanya kazi yake baraza la madiwani limekwisha mkataa naomba mkuu mkurugenzi uondoke naye kwani ni kero kwa wananchi,” mbunge huyo alimweleza Rais.


Kwa upande wake, Zedi alipopewa fursa ya kuwasalimia wananchi alimuunga mkono mbunge mwenzake na kumwomba Rais Kikwete aondoke na mkurugenzi huyo pamoja na mhandisi wa maji ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. 


Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliposikia suala hilo aliwaahidi wananchi hao kuwa mhandisi wa maji wilayani Nzega, Mariam Majara ataondoka naye katika ziara hiyo ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi na wananchi hao waweze kupata fursa ya kupata maji safi na salama.


Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa, alisema Wilaya hiyo imetengewa fedha za kutosha katika sekta ya maji hivyo ni kosa kushindwa kutoa huduma hiyo kwa wananchi.


Akijibu maombi ya wabunge hao ya kuondoka na mkurugenzi mtendaji pamoja na mhandisi wa maji Rais Kikwete alisema kuwa suala hilo litatatuliwa.


Alisema inasikitisha kwamba serikali inatenga fedha za kutosha kwenye halmashauri kwa ajili ya kurahisisha wananchi kupata huduma bora lakini baadhi ya watumishi wanakwamisha jitihada hizo.

No comments:

Post a Comment