Wauguzi walaumiwa kwa kusababisha kifo cha kichanga

Mama mjamzito amejifungua mtoto na kufariki dunia nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kabla ya kupokelewa.


Tukio hilo lilitokea Januari juzi saa 10:00 jioni baada ya mama huyo aliyefahamika kwa jina la Tausi Saidi (29), mkazi wa kijiji cha Mbete Kata ya Mlimani  Manispaa ya Morogoro kufikishwa hospitalini baada ya kushikwa na uchungu.

Baada ya kufika hospitalini akiwa na muuguzi wa zahanati ya Mbete pamoja na ndugu wa mgonjwa huyo, wauguzi wa hospitali hiyo walianza kubishana kabla ya kumhudumia mgonjwa.


Kwa mujibu wa mume wa mwanamke huyo, Kudra Khalfani, mkewe alianza kupata uchungu akiwa nyumbani,  na kumpeleka katika zahanati ya Mbete, na baada ya kufika huko alilazimika kupelekwa katika Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kuonekana kuwa anahitaji matibabu makubwa.


Alisema baada ya kufika wodi ya wazazi, Muuguzi waliyeambatana naye aliingia wodini na kumtaka nesi wa wodi hiyo kwenda kumuangalia mgonjwa, lakini hakupewa msaada.


Alisema muuguzi huyo aliwataka kumpeleka mama huyo wodi namba saba ‘B’ bila kutoa msaada wowote.


“Kabla ya kufika wodini akasema Tumshushe, akawa amejifungulia koridoni na mtoto akafariki,” akusema.


Mashuhuda waliojitambulisha kwa majina ya Mwajuma Ally na Aida Hamis  walieleza kuwa kitendo hicho ni cha udhalilishaji, kwamba kimetokana na uzembe wa wauguzi wa wodi ya wazazi.


Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Ritha Lyamuya, alithibitisha kutokea kwa tukio na kwamba hali hiyo ilitokana muuguzi kumhudumia mgonjwa mingine.


Dk Lyamuya  alisema mimba ya mwanamke huyo ilikuwa haijafikisha umri wakujifungua, na kwamba alishawahi kupoteza mimba nne,  kutokana na kuwa na viashiria vya hatari vya uzazi.


Aliongeza kuwa pamoja na kupewa tahadhari hiyo,  kadi lake la kliniki linaonyesha kuwa amehudhuria mara moja tu, kitu ambacho ni hatari sana kwa mama mjamzito.

 

No comments:

Post a Comment