Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai,
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, kimeeleza
nia yake ya kutaka kuachiwa mamlaka ya kumchagua mgombea urais wa visiwa
hivyo, badala ya utaratibu wa sasa unaoshirikisha wenzao wa Tanzania
Bara.
Pamoja na hatua hiyo, chama hicho pia
kinafikiria kurejea mtindo wa kupokezana kiti cha urais wa Tanzania kati
ya bara na visiwani kama ilivyokuwa awali, ili kuweka usawa katika
Muungano.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa huenda ikazua
mpasuko na malumbano mapya kuhusu suala la urais ndani ya CCM, ambako
harakati za baadhi ya wanachama wake wameanza kupiga mbio za kuutaka
urais katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu visiwani
humo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai, alisema kwa
sasa suala hilo linajadiliwa na kwamba ana matumaini kuwa litapatiwa
ufumbuzi.
Hatua hiyo imekuja wakati Zanzibar
ikiadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi yaliyoung’oa madarakani utawala wa
mabavu wa Sultani, huku ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya uchaguzi
mkuu wa Rais wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na
madiwani, utakaofanyika 2015.
“Ndani ya CCM tuna utaratibu wetu wa kupata
viongozi, lakini hilo suala la kuchaguliwa mgombea urais kutoka kwenye
vikao vya Dodoma hata sisi limetugusa... Kwa sasa tuko kwenye mchakato
wa kulijadili ili tupate ufumbuzi,” alisema Vuai na kuongeza:
“Siyo tu kuchaguliwa mgombea urais, hata suala
la kupokezana urais na jinsi ya kupata viongozi wengine kama wabunge na
wawakilishi tunalijadili kwa kina. Ninaamini tutapata ufumbuzi… Siwezi
kusema lini kwa kuwa chama chetu ni kikubwa mno, lakini tunalijadili.”
Vuai ametoa kauli hiyo, huku kukiwa na
malalamiko ya Wazanzibari wengi kuhusu Muungano, ambapo wengine wanahoji
iwapo kuna haja ya kuendelea na utaratibu wa sasa kupata mgombea na
Rais wa Zanzibar ambao ni lazima upate baraka za CCM Bara.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema jambo hilo halijafikishwa
kwenye vikao rasmi vya chama.
“Kama wao wanalifikiria hilo, acha waendelee,
labda ungewauliza kama wameshalifikisha kwetu. Ukiniuliza mimi
nitakujibu kuhusu utaratibu tulionao sasa, ila kama wao wana hoja
nyingine, basi watazileta kwenye vikao husika zitajadiliwa,” alisema
Nape.
Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, akizungumzia suala hilo alisema
hayo ni maoni tu ya wananchi na wala Serikali haiwezi kuyaingilia.
“Wazanzibari wana haki ya kutoa maoni yao na
wala Serikali hatuyaingilii. Lakini waelewe kwamba bado Muungano una
faida kubwa kwetu. Hapa kwetu uchumi ni mdogo, ardhi ni ndogo pia
Zanzibar inapata ulinzi na usalama kutoka kwenye Muungano,” alisema
Waziri Aboud.
Mapinduzi na Muungano
Akizungumzia mafanikio ya
miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Vuai alipinga madai kuwa Mapinduzi
hayo yamemezwa na Serikali ya Muungano.
“Nakubali kuwa Mapinduzi
yalilenga kuikomboa Zanzibar ili iwe huru, lakini siamini kama Zanzibar
imemezwa na Muungano.,” alisema Vuai.
Hata hivyo, Vuai alikiri kuwa upo upungufu ya hapa na pale katika Muungano, ambayo yanapaswa kurekebishwa.
Kuhusu suala la Serikali mbili kama ulivyo
msimamo wa CCM, Vuai aliuunga mkono utaratibu huo akisema kuwa Muungano
unawasadia Wazanzibari katika ulinzi na usalama wao na kulinda umoja wa
Watanzania wote.
Huku akiponda utaratibu wa Serikali tatu na
Serikali ya mkataba kama inavyonadiwa na vyama vya upinzani, Vuai
alisema bila Serikali mbili, Muungano lazima uvunjike.
“Muungano wa
Serikali mbili ndiyo njia pekee ya kulinda umoja wa Watanzania. Serikali
za mkataba zitavunja Muungano tu.,” alisema na kuongeza:
“Hizo Serikali tatu zitakuwa na michango kwa
Serikali ya Muungano. Itafika mahali kila Serikali itatoa kisingizio,
mara bei ya pamba, korosho imeshuka. Mara utasikia Zanzibar nayo inasema
kuwa bei ya karafuu imeshuka, mara machafuko na mengineyo, mwisho
Muungano utavunjika.”
Awaonya Wapemba
Vuai amewaonya wananchi
wenye asili ya Pemba akisema wao ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kutaka
kuvunja Muungano na kuongeza kuwa endapo utavunjika ni wazi kwamba
chokochoko hazitaishia hapo.
No comments:
Post a Comment