UTAFITI: Watoto wa kike wanaelewa haraka darasani kuliko wa kiume
Wanafunzi wa kike
UTAFITI mpya wa masuala ya elimu umebainisha kwamba wanafunzi wa kike hufanya vizuri zaidi darasani kuliko wanafunzi wa kiume.
Matokeo ya utafiti huo, uliofanywa hivi karibuni
na wataalamu wa elimu kutoka vyuo vikuu vya Georgia na Columbia vya
nchini Marekani, umebaini kuwa watoto wa kike wa kati ya umri wa miaka
sita hadi 12, huelewa kwa haraka darasani kuliko watoto wale wa kiume.
Wameeleza kuwa wanafunzi hao wa kike huwa makini
zaidi kumsikiliza mwalimu anapokuwa akifundisha darasani, tofauti na
watoto wa kiume, ambao hutumia muda mwingi kufanya mambo mengine ikiwamo
kucheza, kuchokozana na pengine kugombana wao kwa wao.
Matokeo hayo yaliyochapishwa katika Jarida la
Rasilimali Watu la Marekani na kuandikwa kwenye mtandao wa Daily Mail,
yanaonyesha kuwa utafiti huo uliangalia uwezo wa watoto zaidi ya 5,000
katika Kusoma, Hisabati na Sayansi.
Watafiti hao kwa kuangalia alama za majaribio
mbalimbali na maoni ya walimu, waligundua kuwa hata katika hatua za
awali (chekechea), alama za watoto wa kike zimekuwa juu siku zote
ikilinganishwa na alama za watoto wa kiume.
Mmoja wa watafiti hao, Christopher Cornwell,
anasema kuwa ujuzi wa wanafunzi hao, ndiyo njia kubwa inayotumiwa na
walimu kuwapanga wanafunzi wao katika madaraja.
Aliongeza kuwa kuna vigezo sita vya kupima uwezo
wa watoto, ambavyo ni: Usikivu, ufuatiliaji wa kazi anazopewa darasani,
kupenda kujifunza, kusoma kwa kujitegemea, uwezo wa kubadilika kutokana
na mazingira na mpangilio wa mambo yake.
“Nafikiri kwa mtu yeyote ambaye ni mzazi mwenye
mtoto wa kike na kiume, atakubaliana nami kuwa watoto wa kike wako mbele
katika mambo yote hayo,” anasema Cornwell.
Cornwell aliongeza kuwa matokeo ya utafiti huo
yamewapa mwanga kujua kwa nini hivi sasa asilimia 60 ya wahitimu wa
shahada ya kwanza nchini Marekani ni wanawake na kwamba hali hiyo
itasababisha wanaume kuwa na wakati mgumu kwenye soko la ajira.
Wizara ya elimu
Mkuu wa Elimu
wa Kitengo cha Uratibu ,Ushauri na Unasihi katika Shule na Vyuo vya
Ualimu kutoka Wizara ya ELimu na Mafunzo ya Ufundi, Franaeli Munishi,
anasema kuwa anaunga mkono utafiti huo akisema kuwa hiyo ni kulingana na
matokeo ya hivi karibuni na kwamba wasichana wamekuwa wakifanya vizuri,
ingawa mara nyingi elimu yao ni ya kujituma zaidi tofauti na wavulana.
Anasema kuwa hata kwenye baadhi ya tafiti za
kielimu ambazo amezifanya, amebaini kuwa baadhi wa walimu hupata wakati
mgumu wanapowafundisha wavulana kuliko wasichana kutokana na wavulana
kuwa wasumbufu.
Anaongeza kuwa sababu kubwa inayowafanya wasichana
wafanye vizuri ni kuwa wasikivu, lakini pia kuwa wazuri katika lugha
na kwamba kwa lugha ni kila kitu kwenye masomo ni lazima watafanya
vizuri tofauti na wavulana, ambao ni wazuri kwenye masomo kama Hesabu na
Sayansi.
“Sababu kubwa ya wasichana kuwa wasikivu darasani inatokana na
malezi yao kwa kuwa muda mwingi, wapo karibu na mama zao tofauti na
wavulana, ambao muda mwingi huwa na mambo yao kitu kinachowafanya
wajilee wenyewe na kujiamulia mambo yao,” anasema Munishi.
Naye Mratibu Msaidizi Kitengo Cha Ushauri na
Unasihi katika Shule na Vyuo vya Ualimu wizarani hapo, Madina Kemilembe
anakubaliana na utafiti huo ingawa anasema siyo kwa asilimia 100 kwa
kuwa hajafanya utafiti kama huo.
Anasema kuwa katika baadhi ya mikoa yenye shughuli
nyingi za kibiashara, wavulana hupotea kabisa kutokana na kutokuwa
wasikivu darasani jambo linalowafanya walimu wachoke kuwafuatilia, hivyo
kutumia muda wao mwingi kuwafuatilia wasichana wanaoonyesha kujali na
umakini kwenye masomo.
“Katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa au yenye migodi,
wavulana ndiyo hupotea kabisa kutokana na tabia yao ya kutokuwa wasikivu
darasani kwani walimu wanawaona mizigo kwa sababu ni watukutu na
wenyewe huamua kwenda kujihusisha na shughuli za kutafuta fedha,”
anasema Kemilembe na kuongeza:
“Matokeo yake, sehemu kama hizo wanaobaki shuleni ni wasichana pekee na hii ndiyo huwafanya wasichana wafanye vizuri.”
Anasema kuwa hata katika mazingira ya kawaida
tangu zamani wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo mengi kwa
wakati mmoja; kumsikiliza mtu na kumwelewa kuliko mvulana na linapokuja
suala la elimu hali inakuwa hivyo hivyo.
Walimu wanena
Mwalimu wa Shule
ya Sekondari Neluka, iliyopo jijini Dar es Salaam, Khalidi Abdallah,
anasema kuwa kuna unafuu kuwafundisha wasichana kuliko wavulana kwani
wavulana wanakuwa na mambo mengi, tofauti na wasichana, ambao ni rahisi
kuficha mambo yao na kuchukua muda kukusikiliza hata kama wakati
mwingine hawaelewi.
“Wasichana ni wasikivu na waelewa na ikitokea ana
tatizo ni rahisi kukufuata kutaka ushauri na wakati mwingine ni rahisi
kumsaidia akihitaji msaada,
tofauti na wavulana ambao ni nadra kuuliza jambo baada ya mwalimu kutoka darasani, hata kama hajaelewa,”anasema Abdallah.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda, yeye anaunga mkono kwa asilimia
60 utafiti huo akieleza kuwa mara nyingi wanafunzi wa kike huwa
wasikivu tofauti na wavulana jambo linalowasaidia kufikia malengo yao ya
elimu.
Anasema kikubwa zaidi kinachowafanya wawe wasikivu
ni hali yao ya kutokujiamini kunakotokana na imani kuwa wao hawawezi,
hivyo hujibidisha ili kushindana na wavulana ambao wanajiamini kupita
kiasi.
Anataja jambo jingine linachowafanya wafanye
vizuri zaidi ni kusifiwa pindi wanapofanya vizuri kwa kuonekana kama wao
ni miongoni mwa wasiotegemewa kufanya vizuri kulingana na tabia
iliyojengeka kwenye jamii kuwa wao hawawezi.
Wazazi wathibitisha
Jamillah
Masanja ambaye ni mama wa watoto watano, watatu ni wa kike na wawili wa
kiume, anasema kuwa kwa upande wake ameiona hiyo hasa katika suala la
kujisomea kwani mtoto wa kike huwa makini bila kuambiwa tofauti na wa
kiume, ambao muda mwingine huwa na mambo yao na ni wabishi.
“Wasichana wangu ni wadogo, mkubwa yupo darasa la
saba anayemfuatia yupo darasa la tano, wa mwisho la tatu na kaka zao
mkubwa yupo kidato cha nne, anayemfuata anasoma kidato cha pili.
Kazi niliyo nayo ni kwa hawa wakubwa kwani hawapendi kusoma,
walikuwa wakifanya vizuri, lakini sasa hakuna kitu hata natamani
niwapeleke kwenye shule za bweni,” anasema mama huyo.
Hata hivyo,
Jafari Ibrahimu, baba wa watoto wawili wa kiume anasema kuwa hajakutana
na tatizo hilo kwa kuwa watoto wake wapo kwenye shule za bweni, ingawa
anapata wasiwasi na matokeo yao.
Anasema walipokuwa watoto wake wako kidato cha
kwanza na cha pili walikuwa wakifanya vizuri tofauti na wanavyozidi
kupanda wanapunguza juhudi ya kufanya vizuri darasani.
Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu Kishiriki
cha Elimu (DUCE) , Joviter Katabalo anasema kuwa wasichana hupevuka
mapema kuliko wavulana, jambo ambalo huwafanya wawe makini zaidi kuliko
wavulana.
Anasema wasichana wana uwezo wa kuelewa na
kutambua mambo haraka, ingawa kuna baadhi ya tamaduni za Kiafrika
zinawanyima uhuru wa kufanya mambo fulani. Matokeo yake wanakosa
kujiamini jambo ambalo kwa namna moja au nyingine limewafanya wafanye
vizuri wakiamini wanakosea.
No comments:
Post a Comment