Wabunge wafichua uozo magereza

Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje Edward Lowassa

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, imefichua uozo ndani ya magereza hapa nchini na kusema kuwa yanahifadhi idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu nje ya uwezo wake wanaofikia 36,552 badala ya 29,400 sawa na ongezeko la asilimia 23.

Wafungwa wengi pamoja na mahabausu waliojazana katika magereza hizo ni wale waliofikishwa huko kutokana na wizi wa kuku, baiskeli, uzururaji, wizi wa simu, unywaji pombe na makosa mengine madogo madogo.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukutana na watendaji wa Idara ya magereza, polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emanuel Nchimbi.


Lowassa alisema idadi kubwa ya watu waliopo katika magereza ambao wanafikia asilimia 90 ni vijana na kwamba wamefikia huko kutokana na matatizo ya kukosa ajira na kazi zingine halali za kufanya.


Hata hivyo, Lowassa alisema sehemu  kubwa ya mahabusu waliopo katika magereza wametokana na kufikishwa huko kwa kukomolewa na askari polisi ambao wanawakamata bila ya kuwa na makosa.


Aliongeza kuwa kuna kukomoana kwingi katika Magereza ya hapa nchini na wengi wa mahabusu waliokutwa na kamati yake hawakutenda makosa kama wanayokabiliwa nayo bali "wamebambikwa".


Lowassa ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, alisema mlundikano wa wafungwa na mahabusu kunaharibu rekodi ya nchi na kuagiza hatua za haraka zichukuliwe ili kulimaliza tatizo hilo.


Aliagiza adhabu mbadala zianze kuchukuliwa kwa makosa mbalimbali anayotenda mtu badala ya kuwekwa mahabusu ama kuhukumiwa kifungo jela.


"Kamati hivi karibuni ilitembelea gereza la Segerea na kujionea idadi kubwa ya mahabusu inayofikia 2400 na wafungwa 98 na tulibaini wengi wao wamewekwa huko kutokaa na makosa madogo madogo ambayo wangeweza kutumikia adhabau mbadala nje ya jela," alisema.


"Kwa mfano mtu anamtuma mke wake dukani usiku kununua kitu, mke huyu  anakutana na polisi wanamkamata lakini mme wake anapoenda polisi kuwaambia huyu ni mke wangu wanamkatalia na kumtaka atoe Sh. 200,000 ili wamuachie kwa madai kwamba mtu huyo ni mzururaji," alisema.


Sababu nyingine iliyotajwa na Lowassa kuwa inachangia mlundikano wa wafungwa na mahabusu ni matatizo ya mwenendo wa kesi kati ya magereza, DPP, mahakama  na polisi na kutaka utaratibu wa uendeshaji wa kesi ubadilishwe.


Aidha, alitaka kuimarishwa mahakama ya watoto ili kuwatenganisha na watu wazima kwa kuwa wakichanganyikana kuna athari kubwa ikiwemo kujifunza tabia mbaya zisizofaa.

No comments:

Post a Comment