Mchungaji KKKT atoa ushahidi vurugu za Mbagala

Mchungaji Frank Kimambo (32) wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Mbagala Zakhem, jana ameiambia Mahakama ya Kisutu kuwa yeye hausiki na masuala ya kudai mali zilizoharibiwa labda aulizwe mwajiri wake ambaye ni Katibu Mkuu wa Dayosisi.

Mchungaji Kimambo alisema hayo jana alipokuwa akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Walialuwande Lema akiwa shahidi wa pili baada ya mlinzi wa kanisa hilo hilo kutoka kampuni ya Pray and Vicent,  Michael Woga (30), kutoa ushahidi wake.


Kimambo alisema yeye ni msimamizi wa kanisa la KKKT Mbagala akiwa anamwakilisha Askofu hivyo jambo la kulipwa mali halimhusu yeye na alieleza hilo baada ya Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka kumuuliza je, watadai malipo ya hasara zilizotokana na uharibifu wa kanisa?


Aliendelea kujibu swali la Kweka kuwa yeye anahusika katika tathmini iliyotolewa ya uharibifu, ambayo alisema pamoja na uongozi wa kanisa hilo walitoa tathmini ya vitu vilivyoharibiwa pia zipo picha za ushahidi.


Alisema hajawahi kusema uharibifu huo ulisababishwa na Waislamu au Wakristo bali anajua uharibifu ulifanywa na kikundi cha watu na kwamba mengine labda yalisemwa na waandishi wa habari.


Aidha aliiambia Mahakama kabla ya uharibifu wa mali hizo yeye alikuwa ofisini kwake akapigiwa simu na muumini wake kwamba kuna watu wanaofanya uhalifu na huenda wakaelekea hapo kanisani ndipo alipofunga mlango wa ofisi ili kwenda kutoa taarifa ila kabla hajafika watu walishafika na kuanza kurusha mawe.


Alisema baada ya kuona polisi wameelekea kanisani aliwafuata nyuma na alivyofika akawekwa chini ya ulinzi hadi alivyotoa kitambulisho ndipo aliposimama  na kuruhusiwa kuangalia kanisa ambalo lilikuwa kwenye hali mbaya.


Wakili Kweka alimuuliza shahidi kama anajua mlalamikaji ni nani katika kesi hiyo na alikiri kuwa hajui ila polisi ndiyo waliyokuja kuchukua maelezo na yeye ametoa ushahidi wa yale aliyoyaona.


Naye Shahidi wa pili Mlinzi Woga aliiambia Mahakama kuwa baada ya kushindwa kupiga risasi alikimbia kwani kulikuwa na watu wengi waliokuwa na mawe ila alirudi baada ya polisi kuja akakuta hali ni mbaya huku ukuta ukiwa umevunjwa.


Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 2, mwaka huu itakapoendelea na ushahidi.

Katika kesi hiyo, washtakiwa 10 wanakabiliwa na mashtaka matano, kula njama kwa  nia ya kutenda kosa kuvunja jengo na ukuta, kuharibu mali kwa makusudi zenye thamani ya Sh. milioni tano, unyang'anyi kwa kutumia silaha mali za Sh. milioni 20 pia kuchoma mali kwa makusudi na walitenda  makosa hayo Oktoba 10 hadi 12.

No comments:

Post a Comment