Wanafunzi IFM wazua tafrani Dar

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na askari kanzu wakimshushia mkong'oto mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es Salaam jana wakati walipofika kituo cha polisi Machava kilichopo Kigamboni, kuwalalamikia kwa kutolichukulia hatua genge la wahuni linalodaiwa kuwavamia baadhi yao usiku kwenye hosteli wanakoishi, kuwapora, kuwabaka na kuwalawiti

Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),  jana walifanya maandamano makubwa jijini Dar es Salaam hadi katika Makao Makuu ya  Polisi na Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakililalamikia Jeshi hilo kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya wizi na kulawitiwa wanavyofanyiwa na genge la watu katika hosteli iliyoko Kigamboni.

 Mamia ya wanafunzi hao walianza kuandamana kutoka chuoni kwao katikati ya Jiji  saa 4:40 asubuhi na kuwasili makao makuu ya Jeshi hilo ambayo yapo pia makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi saa 5:33 asubuhi.

 Baada ya kuwasili, walisema dhumuni la maandamano yao ni kutaka kuonana na Mkuu wa Polisi  (IGP), Said Mwema au Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ili kufikisha kilio chao kwao.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa IFM, Michael Charles, alisema wanafunzi wamekuwa wakivamiwa na kuibiwa mali zao ikiwamo kompyuta ndogo (Laptop), kubakwa na kulawitiwa katika hosteli ya Kigamboni wilayani Temeke.

 Charles alisema licha ya matukio hayo kuripotiwa  katika kituo cha polisi Machava kilichopo Kigamboni, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi na hivyo kuwafanya wanafunzi wahisi kuwa huenda vitendo hivyo vina baraka za polisi.

“Juzi tulivamiwa na wenzetu wawili wakapigwa mapanga, tukaibiwa kompyuta na wenzetu wengine wakalawitiwa, ndio maana tumeamua kuandamana kupeleka malalamiko yetu kwa sababu  tumeona kinachofuata tunaweza kuuawa,” alisema Charles.

Charles alisema mpaka sasa idadi ya kompyuta za wanafunzi zilizoibwa ni 300 ambazo zimekuwa zikiibwa kila siku.

 Awali  baadhi ya wanafunzi walizuiliwa eneo la jengo la PPF wasifike Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, wanafunzi hao walikwama kuonana na IGP Mwema na Dk. Nchimbi baada ya kuzuiliwa na maafisa wa jeshi hilo katika lango kuu la kuingilia badala yake walielezwa na askari waliokuwa langoni happ kuwa wachague watu watatu ili waruhusiwe kwenda kuonana na viongozi hao.

Pamoja na jitihada zilizofanywa na maafisa wa polisi H. Mbezi na N. Mariajan, kuwataka wachague watu watatu kwenda kutoa malalamiko hayo ziligonga mwamba kufuatia baadhi ya wanafunzi hao kudai watakaokwenda huko watawekwa chini ya ulinzi na suala lao halitasikilizwa tena.

Badaye wanafunzi hao walibadilisha maelezo kwa kudai kuwa wanataka kuonana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ili wamweleze kilio chao.

Ilipofika saa 6;03 mchana Kova aliwasili Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kuzua shangwe kubwa kutoka kwa wanfunzi hao ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu kwamba huyo ndiye atakayeweza kuwasikiliza kilio chao na kukipatia ufumbuzi.

Kova baadaye alizungumza na wanafunzi hao kwa kuwataka aambatane nao hadi Kigamboni ili watuhumiwa wa vitendo hivyo wakamatwe haraka.

Msafara wa Kova ambaye alikuwa katika gari namba PT 1574 ambalo lilimchukua Charles na Waziri Mkuu wa IFM, Mangesho na kuanza safari ya  kuelekea Kigamboni  saa 6:11 mchana pamoja na mamia ya wanafunzi wa chuo hicho.

Hata hivyo hali ilikuwa mbaya zaidi  baada ya idadi kubwa ya wanafunzi hao kutaka kuvuka katika kivuko eneo la Ferry na hivyo kuulazimu uongozi wa kivuko hicho kusimamisha safari ili kupunguza wengine.

Halikuwa jambo rahisi kuwapunguza wanafunzi hao katika kivuko na hivyo kusababisha mabishano yaliyochukua muda mrefu  kati ya uongozi wa kivuko, Jeshi la Polisi likiongozwa na Kova pamoja na wanafunzi hao ambao walikuwa wanagoma kupunguzwa.

Mabishano hayo yalidumu kwa zaidi ya saa tatu hadi walipokubaliana kusafirishwa kwa awamu.

“Kitaalamu hatuwezi kuondoa kivuko kwa sababu idadi ya watu ni kubwa na kitaalamu hairuhusiwi labda wengine wapunguzwe,” alisema Mhandisi wa Mambo ya Bahari, Reuben Materu.

 Kwa upande wake, Kova alisema: “ Hili jambo halihitaji ushabiki ni la kiutaalamu zaidi, tunaweza kuwaruhusu wavushwe hivyo hivyo, lakini ikaleta madhara mengine makubwa zaidi.”

 Mabishano hayo yalizuia safari za abiria wengine hadi wanafunzi wote waliposafirishwa kwa awamu.

POLISI WAFYATUA MABOMU

Licha ya wanafunzi kukubaliana na Polisi kuelekea katika Uwanja wa Machavya, lakini wanafunzi hao walikiuka  nmakubaliano hayo baadaye na  kuelekea kituo cha polisi cha Kigamboni huku wakiimba nyimbo za matusi dhidi ya Jeshi la Polisi hali iliyowalazimisha Polisi wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufyatua mabomu ya machozi kwa takribani dakika 20.

 Mbali na kufyatua mabomu, pia waliwakamata wanafunzi zaidi ya 100 na kuwapeleka katika kituo cha polisi Kigamboni, lakini baadaye waliachiwa na kuelekea sehemu ya uwanja kwa ajili ya mazungumzo na Kova.

 Baadhi ya wananchi wa  Kigamboni walijitokeza kutoa ushuhuda, akiwamo mtoto mwenye umri wa miaka tisa aliyejulikana kwa jina la Dulah Chinda alisema: “Ni kweli wanafunzi huwa wanaibiwa, nina wafahamu hao wezi na kama mkitaka nitawapeleka.”

Symphorasa Ndyamukama, mkazi wa Kigamboni na mmoja wa wamiliki wa hosteli za wanafunzi hao, alisema alishawahi kutoa taarifa hizo za uhalifu polisi ,lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Kutokana na hali hiyo, Kova ambaye alikuwa ameambatana na  Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alimtaka atoe ufafanuzi juu ya taarifa hizo.

Kamanda Kiondo alijibu kwamba taarifa hizo za uharifu hazijawahi kuripotiwa polisi rasmi isipokuwa walikuwa wanazisikia.

Kutokana  na hali hiyo, Kamanda Kova alimuagiza Kiondo kulifanyia kazi  mara moja suala hilo ili kubaini waharifu na kuwakamata.

Pia alisema atamteua askari atakayeshirikiana naye katika kuwabaini wahalifu katika eneo hilo, na kuagiza zoezi hilo kuanza jana.

 

No comments:

Post a Comment