Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Gregory Mushi
Watu wanane wamefariki dunia wakiwamo wanafunzi
wanne wa shule ya sekondari na watatu kujeruhiwa baada ya gari
walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Mark II kugongana na Mitsubishi
Fuso eneo la Chalinze, mkoani Pwani.
Katika ajali hiyo iliyotokea juzi saa 12:00 jioni katika Kitongoji
cha Kibiti Tarafa ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Mark II
hiyo
yenye namba za usajili T. 363 AZG, iligongana uso kwa uso na Fuso yenye namba za usajili T. 433 AYQ.
Ajali hiyo ilitokea wakati Mark II iliyokuwa ikiendeshwa na Abuu
Ahmed (21), kuwa katika mwendo kasi ikitokea Tanga kuelekea Morogoro
kujaribu kulipita Fuso lililokuwa likitoka Morogoro kuelekea Dar es
Salaam likiendeshwa na Mweta Daniel.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Gregory Mushi,
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa waliokufa katika
ajali hiyo ni wanafunzi wanne wa Shule ya Sekondari Chalinze wote wakazi
wa eneo la Msolwa.
Aliwataja kuwa ni Essau Enos (16) wa kidato cha tatu, Latifa
Shabani (17), wa kidato cha nne, Bahati George (18), wa kidato cha nne
na Stella Isaack Kazimoto, (18).
Aliwataja watu wengine waliofariki dunia wakiwa katika Mark II kuwa
ni Hassan Kulunga na Maria Sadick, wakazi wa Ubena ambao umri wao
haukufahamika mara moja. Wengine ni dereva wa Mark II, Abuu Ahmed (21)
na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka minne na mitatu
aliyefahamika kwa jina la Samwel Ismail, ambaye ni mtoto wa marehemu,
Maria Sadick. Aidha, Kaimu Kamanda huyo aliwataja majeruhi waliokuwa
wamepanda Fuso kuwa ni William Thobias (30), mkazi wa Matombo mkoani
Morogoro na utingo, Ahamad Juma (36).
Mushi alisema majeruhi hao wanaendelea na matibabu katika kituo cha
afya Chalinze na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Teule
ya Tumbi wilayani Kibaha. Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Tumbi, Rose
Mtei, alithibitisha kupokea miili minane iliyokuwa imeharibika.
Kufuatia ajali hiyo, Kamanda Mushi ametoa wito kwa madereva
kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokea
kwa uzembe na kwamba Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani litawachukulia sheria
kali madereva hao.
Shuhuda wa ajali hiyo, Godfrey Bonny, alisema ajali hiyo ilitokea
wakati dereva wa Mark II akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake
ndipo gari lake lilipokutana uso kwa uso na Fuso.
“Mimi ni mkazi wa Chalinze, ilikuwa ni saa 12:30 jioni, nilisikia
kishindo kikubwa na ndipo tulipokwenda katika eneo la tukio na kukuta
gari dogo limeharibika vibaya na ikiwa chini ya uvungu wa gari kubwa.
Lakini kutokana na kuchelewa kwa Kikosi cha Uokoaji, watu waliokuwamo
ndani walipoteza maisha kwa kukosa msaada wa haraka,” alisema Bonny.
Shuhuda mwingine, Yusuph Mjema, ambaye pia ni mkazi wa Chalinze,
alisema alipofika eneo la tukio, alikuta watu hao wamebanwa, lakini
kutokana na kukosa vifaa maalum kwa ajili ya uokoaji, ilichukua muda
mrefu kuwatoa.
No comments:
Post a Comment