Albino auawa, wawili wakatwa viungo


Vicky Ntetema

HALI ya wasiwasi imetanda miongoni mwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, baada ya watu watatu kukatwa viungo na mmoja wao kuuawa mwezi huu.


Katika miaka ya hivi karibuni, jumla ya albino 72 wameuawa, 34 wamenusurika, wengi wao kwa kukatwa viungo au kuumizwa. Makaburi 15 yamefukuliwa na viungo kuchukuliwa na kumekuwa na majaribio manne ya kufukua makaburi.

Katika matukio ya hivi karibuni, walemavu hao wakazi wa Tabora na Sumbawanga wamekatwa mikono ya kushoto. Ukatili huo safari hii umekwenda kinyume na ilivyokuwa mwaka 2010-2011 wakati mikono ya kuume ndiyo iliyokuwa inakisiwa.
Aliyeuawa ni
Lugolola Bunzari (7) na waliojeruhiwa ni Mwigulu Matonange (10) na Maria Chambanenge (39).


Katika matukio hayo, mtoto mwenye umri wa miezi saba alinusurika kuuawa baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba ya mama yake usiku katika eneo la Lamadi, Wilaya ya Busega, Mwanza siku moja baada ya kupokea ujumbe mfupi wa simu kwamba mtoto wake anawindwa.


Marehemu Lugolola
Kijiji cha Kanoge kina umbali wa takriban kilomita 75 kutoka Tabora Mjini, barabara iendayo Ulyankulu kwenye machimbo ya dhahabu.
Imenichukua saa mbili na nusu kufika huko. Saa moja na nusu kati ya hizo, nilizitumia katika safari ya kilomita 15 tu kutoka Kanoge makao makuu ya kijiji hadi Kitongoji cha Kinondoni alikouawa mtoto Lugolola.


Nyumbani kwa Bunzari niliwakuta ndugu na jamaa kutoka vijiji vya jirani vya Wilaya hiyo ya Kaliua, Tabora. Bibi mzaa baba wa Lugolola, Gama Zengabuyanda (60), ndiyo kwanza alikuwa amerejea kutoka Hospitali ya Mkoa ya Kitete alikokuwa akitibiwa baada ya kushambuliwa na majambazi alipotaka kumwokoa mjukuu wake.


Huku akilia kwa huzuni, Zengabuyanda alinisimulia jinsi mjukuu wake na baba yake mzazi, Zengabuyanda Meli (95) walivyouawa kikatili.


Katika muda wa kati ya saa 10 na 11 alfajiri ya kuamkia Februari Mosi mwaka huu, Lugolola aliuawa kikatili baada ya kukatwa mkono kwa panga, kukwanguliwa nywele, kujeruhiwa mkono wa kulia na sikioni na kuondolewa ngozi kwenye sehemu ya paji la uso.


Katika mashambulizi hayo, babu yake Meli pia aliuawa alipojaribu kumwokoa mjukuu wake. Vilevile baba yake mzazi, Bunzari Shinga alijeruhiwa wakati alipojaribu kumlinda mwanaye.
Nilimkuta mama mzazi wa Lugolola aitwaye Kulwa akisaidiana na ndugu zake kumenya maharage mabichi waliyoyatoa shambani mwao muda mfupi tu uliopita.


Yeye ni mke mkubwa wa Bunzari Shinga (35). Walibahatika kupata watoto sita, wawili kati yao ni albino. Lugolola na marehemu mdogo wake aitwaye Maganga aliyefariki kwa malaria mwaka 2011.


Usiku wa mashambulizi hayo, Kulwa anasema alikuwa amelala na watoto wake wadogo wa kike (mmoja, Shija mkubwa) na Lugolola kwenye nyumba yake inayotazamana na ile ya mke mwenzake Pili, umbali wa takriban mita 20. Bunzari alikuwa amelala kwa mke huyo mdogo na binti yao mwenye umri wa mwaka mmoja hivi.


Mzee Meli alikuwa amelala na watoto wa kiume upande wa kulia wa nyumba ya Kulwa.
“Aliamshwa usingizini na kelele za watoto waliokuwa wakilalamika kwamba wanapigwa na fimbo. Alipotaka kwenda chumbani kwa watoto alishambuliwa kwa mapanga kichwani, usoni, mgongoni, mikononi na miguuni,” Gama anaelezea huku akilia.“Pamoja na hayo yote, Baba alijikongoja kuelekea kwenye nyumba alimolala mjukuu wangu, Lugolola huku akipiga mayowe, Tumevamiwa! Nani anataka kuwadhuru watoto wangu.”
Majangili hayo yakamshambulia zaidi kwa mapanga na marungu na huo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Jamani Baba yangu!”
Gama anasema alikuwa amelala kwenye banda lake lililopo kati ya nyumba ya pili na ile ya babu.


Banda hilo la nyasi na kuta za udongo na miti lilikuwa limepambwa kwa vibuyu vya aina mbalimbali, tunguri, vyungu vilivyohifadhi mizizi, magamba ya miti, kauri (nyumba za konokono), hirizi, nywele za binadamu, taya za wanyama, vipande vya mifupa mbalimbali, fuvu la mnyama na gamba la kobe. Katika mazungumzo yetu niligundua kwamba Mzee Meli alikuwa mganga wa kienyeji.


Gama aliposikia vilio vya watoto alitoka nyumbani mwake na kukimbilia kwenye nyumba ya babu ili kujua kilichowatokea wajukuu wake na sababu iliyomfanya baba yake apige mayowe.


Akiwa nje alimwona baba yake akishambuliwa na watu watatu. Watu wengine wanne walikuwa wamesimama nje ya nyumba ya Kulwa wakiwa wameshika silaha mbalimbali ikiwa ni pamoja na magobole, mapanga na marungu. Gama alipiga kelele, ‘Tumevamiwa!’ na mmoja kati ya watu hao alimshambulia kwa panga kichwani, miguuni na mikononi.

Alianguka na akapata mwanya wa kutambaa chini kwa chini kama nyoka hadi akafika kwenye shamba la mahindi na kupotelea kwenye vichaka.
Hata hivyo, alizimia na alipozinduka alijikuta akiwa Wodi ya Wanawake ya Hospitali ya Kitete.

Gama alikuwa amefiwa na mjukuu wake na baba yake mzazi. Kinachomsikitisha zaidi ni kwamba waliuawa bila ya hatia na hakupata hata fursa ya kuwaaga na kuwazika.

Itaendelea kesho...

No comments:

Post a Comment