‘Wanafunzi 62 waliofaulu la saba hawajaripoti shuleni’


WANAFUNZI 62 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kutakiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa wilayani Simanjiro, Manyara hawajaripoti shuleni.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Maendeleo cha Kata ya Endiamtu, katika Mji Mdogo wa Mirerani, Mkuu wa shule hiyo,Emmanuel Kallo alisema wanafunzi hao ni kati ya 157 waliochaguliwa kujiunga na shule yake.

Kallo alisema baadhi ya wanafunzi hao wamehamishiwa katika shule binafsi za sekondari.

Alisema wanafunzi wengine 12 wamehamishiwa katika shule nyingine za sekondari za Serikali .

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, wengine hawajaripoti katika shule yoyote na kwamba wanahesabika kuwa ni watoro.

Kwa upande wake,Diwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia, alisema jitihada lazima zifanyike ili kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanaripoti shule na kuungana na wenzao katika masomo.

“Hii tabia ya utoro siyo ya kuiachia, maana hata mwaka jana kwenye wilaya yetu kuna baadhi ya wanafunzi hawakupelekwa shule na zaidi ya wazazi sita walipelekwa mahakamani,” alisema Zacharia.

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Edmund Tibiita ,alimweleza Kallo kuwa afikishe ofisini kwake majina ya wanafunzi wote ambao walifaulu kwenda kwenye shule yake na hadi sasa hawajaripoti.

“Naomba unipatie majina ya watoto wote ambao hawajafika shuleni ili nipambane na wazazi na walezi wao,kwa sababu katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia bila elimu watoto watapata athari kubwa,” alisema Tibiita.

No comments:

Post a Comment