Waziri wa ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa Anna Tibaijuka.
BARAZA la Madiwani katika Manispaa ya Temeke,
wameilalamikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
kutowashirikisha wao wala halamashauri kwa ujumla katika ujenzi wa Mji
Mpya wa Kigamboni.
Madiwani walisema hayo katika kikao cha maendeleo ya wilaya hiyo kilichofanyika katika Manispaa hiyo.
Katika kikao hicho,Diwani wa Kata ya Kurasini
Winfrey Kimati aliibuka na hoja juu ya mradi wa ujenzi wa Kigamboni,
ambapo aliilaumu wizara hiyo kwa kutokuzingatia kanuni maalumu.
Kimati alisema wizara haikushirikiana na
Halmashauri ya Temeke na badala yake iliwahusisha madiwani wanne kutoka
kata tofauti za Kigamboni. Aliongeza kuwa jambo hilo linashangaza na
kuhoji ni kwanini wizara hiyo iwahusishe madiwani hao bila kuishirikisha
halmashauri kwa ujumla kwa kuwa madiwani wote wapo chini ya halmashauri
hiyo.
“Tunahitaji kikao maalumu na wizara juu ya
utaratibu maalumu kuhusiana na ujenzi huo na huyo anayewapeleka madiwani
wa kata ina maana hajui kama wapo kwenye halmashauri? Aliuliza Kimati.
Kwa upande wake,Diwani wa Viti Maalumu, Amina
Khatibu alisema suala la Kigamboni liangaliwe kwa umakini kwa kuwa
matatizo yakianza kutokea watakaoanza kuathirika ni madiwani kwa kuwa
wao wapo karibu na wananchi.
``Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
ichukue tahadhari mapema yasije yakatokea kama ya Mtwara, hatutaki
Kigamboni kuwa uwanja wa vita, taratibu juu ya ujenzi huo ni vema
zikawekwa wazi.
Aliongeza kuwa ni vyema madiwani wakaelimishwa juu
ya taratibu za ujenzi huo,ili iwe rahisi kuwaelezea wananchi kwa kuwa
wao wapo nao karibu hivyo itakuwa ni rahisi kuwafikishia ujumbe.
Madiwani hao walisema wasiwasi wao upo juu ya
wananchi kwa kuwa wengi wao bado hawana uelewa mzuri juu ya hatma yao
mara ujenzi huo utakapoanza, hivyo ni vyema wizara ikakutana na
halmashauri ili iweze kuwafafanulia suala hilo.
Diwani wa Kata ya Makangarawe, Victor Mwakasendile
alisema tatizo ni ushirikishwaji na kusisitiza kuwa hawaukatai mradi
huo kwa kuwa wao ni madiwani wa wilaya hiyo na ujenzi unafanyika katika
wilaya husika.
Mbali na hayo walisema kuna taarifa kuwa madiwani
hao wa kata zilizopo Kigamboni wanaenda Dodoma kuongea na Profesa Anna
Tibaijuka, licha ya kuwa hawafahamu wanaenda kuongea naye nini, jambo
hilo lilizidi kuwashanganza madiwani hao iweje waonane na Waziri bila
Halmashauri kufahamu.
Hata hivyo madiwani hao walifikia muafaka wa
kumuandikia barua Tibaijuka ili waweze kuonana naye mara atakapotoka
bungeni jambo ambalo liliungwa mkono na Mkurugenzi wa manispaa hiyo.
Tibaijuka akijibu hoja hizo kupitia gazeti hili, aliwatuhumu madiwani hao kwamba waliwafukuza watendaji wake kwenye kikao.
Alisema kuhusu kuwashirikisha walijaribu sana
kuwashirikisha lakini waliwafukuza watendaji wake. “Tumewashirikisha
kadri walivyokubali kutusikiliza’ alisema Tibaijuka.
No comments:
Post a Comment