Wanafunzi wa shule ya msingi wakiwa darasani
MATOKEO mazuri au mabaya ya elimu kwa mtu,
huonekana katika namna anavyotenda mambo na dhamira yake ya kutenda, na
wala hayatokani na alichojifunza, namna alivojifunza na sababu ya
kujifunza.
Hiyo ndio tofauti kubwa kati ya shule yenye kutoa
maarifa na ujuzi na shule yenye kutoa vyeti na sifa za kumuwezesha mtu
kupata kazi.
Watu wengine wanapozungumzia elimu wanafikiri
kuhusu utaratibu mzima wa kujifunza wenye lengo la kumpatia mtu ujuzi na
maarifa na kumudu vyema kile alichojifunza.
Ujuzi na maaarifa ndio hasa lengo na upatikanaji
wake unaotarajiwa utumike katika kupambana na changamoto na hata kuibua
na kuleta maarifa mengine zaidi.
Kuna watu wengine wanapozungumzia elimu, wanafikiria umiliki wa cheti kinachoonyesha una ujuzi fulani.
Elimu ya aina hii sio kwa ajili ya kutumika katika
maisha wala kutafuta maarifa mengine, bali ni kwa ajili ya mtu
kukariri anachojifunza na kuyatoa yale maarifa yaliyokaririwa katika
mitihani ili apate cheti kizuri kitakachowezesha kupata kazi yenye
kipato kizuri.
Kimsingi, cheti kazi yake ni kumpatia mtu kazi. Cheti ndio ‘pasipoti’ ya kwenda katika nchi ya kipato.
Watanzania wengi kama sio wote, tumeangukia
katika kundi hili. Wengi wetu tunataka pasipoti ya kwenda katika ‘nchi’
ya kipato cha kuajiriwa, tunataka vyeti!
Katika mfumo wetu wa elimu
mpaka sasa ufaulu wa mtihani ndio unaosema fulani apangiwe shule gani,
apangiwe kozi gani chuoni, apate kiasi gani kwenye mikopo ya elimu ya
juu na apangiwe kazi gani na alipwe kiasi gani.
Sasa kuna vita kati yetu, kila mmoja anataka mwanawe, yeye mwenyewe au ndugu yake afaulu ili afike katika nchi ya ahadi.
Mbinu mbalimbali zinatumika kufanikisha lengo
hili, vita haina macho! Mbinu kuu ikiwa matumizi ya pesa. Kusoma shule
nzuri na ghali, kulipia twisheni, walimu bora, kununua vitabu na
mwishowe hata kununua mitihani.
Mchakamchaka huu wa kutaka kufaulu kisha kupata
vyeti, unawaacha nyuma watu wa kipato cha chini kwani hawawezi kumudu
kununua mitihani, au kusoma twisheni za gharama.
Wenye nacho wananeemeka na mtindo huu. Mwelekeo unaonyesha masikini wataachwa kwa kiasi kikubwa na wenye uwezo.
Mwanzo wa kujenga matabaka mawili kupitia elimu
bila kificho unaonekana. Angalia matokeo yaliyopita ya kidato cha nne
na matokeo ya hivi karibuni ya kidato cha pili.
Angalia hadhi ya shule zilizomo katika kumi bora. Au angalia ni
wanafunzi wa tabaka gani walio wengi katika shule hizo? Kisha zitazame
shule zilizoshika mkia na pia angalia ni wanafunzi wa kutoka tabaka gani
wanaosoma shule hizo.
Elimu yetu imeandaa matabaka mawili; tabaka la
watu wachache wanaotoka familia zinazojiweza ambao wanaweza kupata
ajira nzuri na tabaka kubwa la wahitimu kutoka familia masikini ambao
wao kazi za mtulinga ndizo zinazowangoja.
Kundi la wenye vyeti vizuri ni wazi limeshika
hatamu mbalimbali za uongozi wa nchi. Kwa vile nao elimu yao ni ya
kuonyesha uwezo wa kukariri na kuweza kujibu mtihani vyema ili wapate
kazi nzuri na hatimae kipato, jambo kubwa wanalolifanya ni kujitajirisha
na sio kumkwamua Mtanzania atoke hapa alipo.
Ripoti mbalimbali za ubadhirifu, wizi na matumizi
mabaya ya madaraka ni mifano michache tu ya watu walioenda shule kwa
ajili ya kupata vyeti na sio kuelimika.
Vyeti sasa vimekuwa ndio njia ya kuchagua nani
afanye kazi ngumu na na nani afanye kazi za ofisini. Aliyefeli au asiye
na cheti kizuri bila kujali uzalendo wake au ujuzi wake mwingine
wowote, huyo lazima afanye kazi za sulubu.
Mbinu nyingi za kufaulu mitihani zinapatikana
mjini. Hivyo basi watakaofaulu mitihani na kupata vyeti hatimaye kupata
sifa za kupata kazi, ni wazi wengi wao watakuwa watu wa mjini.
Watu
wa vijijini watakuwa wamebaguliwa na kuachwa kuendelea kuishi katika
kundi la watu wa kazi ngumu. Vivyo hivyo kwa mikoa iliyo nyuma
kimaendeleo, nayo itaachwa katika kundi la watu wa aina hiyo ya ajira.
Tumetengeneza matabaka ya watu wanaopaswa kuongoza
na wale wanaopaswa kuwa watwana wa kuwatumikia viongozi waliopata
nafasi kwa sababu wana vyeti.
Hakuna shaka yeyote kuwa ile elimu ya kikoloni iliyobagua watu kwa misingi ya rangi,
sasa imerudi na anayebaguliwa ni Mtanzania.
Kibaya zaidi anayefanya ubaguzi huo naye ni Mtanzania. Chonde
tunakoelekea sio kuzuri!
No comments:
Post a Comment