Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela
Watuhumiwa wa ujambazi waliokusudia kupora fedha
kutoka kwa mkurugenzi wa kampuni moja wamezua taharuki kwenye kituo cha
mabasi Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya kurusha risasi za moto
zilizosababisha watu kukimbia ovyo kunusuru maisha yao.
Wezi hao waliokuwa na pikipiki juzi saa 3:00 usiku walivamia gari
la Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hunting International, raia wa
China Jung Won Jyo (44) kwa lengo la kumwibia fedha.
Baadhi ya abiria walikuwa na wakati mgumu kwa vile baadhi walikoswa
koswa na magari wakati huo wakikimbia kujiokoa huko magari nayo
yakikimbia kuondoka eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha
kutokea kwa mkasa huo aliosema ulihusisha watuhumiwa watatu waliokuwa
kwenye pikipiki hadi jana walikuwa hawajakamatwa.
Alieleza kuwa walipofika kituoni hapo walilifuata moja kwa moja gari
namba T 198 BRE aina ya Toyota Hiace lililokuwa limembeba Mkurugenzi Jyo
likiendeshwa na Mohamed Seleman.
Alisema ndani ya gari hilo kulikuwa na mizigo ambayo majambazi hao walidhani ni fedha.
Kamanda alisema baada ya mkurugenzi huyo kufikishwa kituoni akitokea
kazini kwake Sinza Makaburini, watuhumiwa hao walianza kufyatua risasi
zilizosababisha tafrani kwa watu waliokuwa kituoni hapo.
Alisema pia walitumia jiwe kuvunja kioo cha mbele cha gari hilo kwa
lengo la kuiba mali zilizokuwamo. "Licha ya kutumia silaha za moto
lakini watuhumiwa hawa waliambulia simu mbili aina ya Samsung…
hatukupata namba ya pikipiki, ila polisi wangu walifika eneo la tukio"
alisema na kuongeza:
"Eneo la tukio tumeokota risasi na ganda la risasi iliyotumika
ninachosema ni kwamba wananchi watambue kuwa wizi wa kutumia pikipiki
upo hivyo wachukue tahadhari kwa kutoa taarifa mapema …," alisema na
kuongeza kuwa hakuna aliyejeruhiwa
No comments:
Post a Comment