Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba
Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba (74), amedai
mahakamani kuwa alimwelekeza aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Marehemu Daudi Balali, asisaini mkataba wa kuipa kazi kampuni
tanzu ya Alex Stewart ( ASSAYERS) Government Business Corporation hadi
atapofanya mazungumzo na Rais (wakati huo Benjamin Mkapa).
Mramba alitoa madai hayo jana wakati akihojiwa na wakili wa
Serikali, Shadrack Kimaro, mbele ya jopo la mahakimu watatu wakiongozwa
na Mwenyekiti John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela wanaosikiliza
kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mshitakiwa huyo na wenzake wawili wanakabiliwa na mashtaka ya
matumizi mabaya ya madaraka, kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex
Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart
(ASSAYERS) Government Business Corporation.
“Nilimweleza Balali aanishe kwa sababu bado nilikuwa sijamaliza
kazi kwa kumshauri Rais hatua za kukubali mkataba na kujua jinsi ya
kupata fedha za mkataba huo kwa kuwa bajeti ya mwaka wa fedha ilikuwa
imeshapitishwa (wakati huo),” alidai Mramba na kuongeza:
“Mkataba ule ulikuwa wa Serikali na ulilipwa kwa fedha za serikali,
kwa sababu nilikuwa nimefunga bajeti ya mwaka huo, nilitaka kukutana na
Rais kumshauri na kumuelekeza jinsi ya kupata fedha.” Alidai kuwa
maagizo yake kwa Gavana ya kufanya ainisho yalikuwa kujenga imani kwa
mkandarasi kwa serikali kwamba ina nia ya kujenga na hatimaye itasaini
mkataba huo. Hata hivyo, kuhusu maelezo aliyohojiwa na kuyatoa kwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuinisha mkataba,
alidai kuwa alikuwa na maana ya kuinisho ni kuingia mkataba.
Alidai kuwa, hajawahi kusomea mambo ya kodi bali alikuwa na mamlaka
ya kusamehe kodi, kwamba alikuwa anapata ushauri kutoka kwa wataalamu
wa masuala ya kodi kutoka Wizara ya Fedha na washauri wa jopo la
wataalamu wa uchumi ambalo liliundwa kwa ajili ya kumshauri Waziri wa
Fedha.
Alidai, alikuwa anatumia vigezo vya kusamehe kodi kutokana na
faida ya umma inayoweza kupata kama vile makampuni ya kutengeneza
barabara na kwamba kukiwa na kodi kubwa makampuni yanaweza kukataa
kutengeneza. Mbali na Mramba washtakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa
Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja
Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanadaiwa kuwa, kati ya Agosti
mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi
wa umma kama mawaziri na katibu mkuu walitumia vibaya madaraka.
No comments:
Post a Comment