Mtoto mlemavu wa ngozi afariki baada ya kukatwa mkono
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Antony Rutta
Mtoto Lugolola Bunzari (7) mlemavu wa ngozi
(albino) amepoteza maisha baada ya kukatwa mkono na kuvuja damu nyingi,
kwenye tukio lililotokea wiki hii mkoani Tabora.
Kadhalika babu wa mtoto huyo aliuawa wakati akijaribu kumuokoa mjukuu
wake baada ya kushambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na
kuvuja damu nyingi.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Antony Rutta, alisema mtoto huyo
alikatwa mkono wa kushoto na mauaji hayo yalitokea juzi saa 10 alfajiri
katika kitongoji cha Kinondoni kilichoko kijiji cha Kanoge wilayani
Kaliua mkoani humo.
Akizungumza na waadishi wa habari alisema watu nane ambao
hawajafahamika wakiwa na gobore, mapanga na marungu walivamia nyumbani
kwa Bunzari Shinga (33) baba wa mtoto huyo, kuishambulia familia yake
kabla ya kumkamata mtoto huyo na kumkata mkono walioondoka nao.
Alisema pamoja na kumkata mkono mtoto huyo walimpiga mapanga
Zengabuyaga Meli (95) babu wa mtoto huyo aliyejaribu kumsaadia mjukuu
wake asiuliwe.
Meli aliyekatwa mkono wa kulia , kichwani na begani alivuja damu nyingi na kufariki dunia muda mfupi baadaye.
Aidha Kamanda Rutta alisema licha ya watu hao kusababisha vifo vya watu
hao pia waliwajeruhi baba wa mtoto huyo Shinga kwa kumpiga risasi mguu
wa kulia ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa ya Kitete mjini
hapa .
Pia Kamanda alisema walimjeruhi Dama Buyaga bibi wa albino huyo na
sasa amelazwa Kitete na hali yake inaelezwa kuwa hairidhishi.
Alihusisha mauji hayo na imani za kishirikina na kwamba uchuguzi
unaendelea na kuongeza kuwa mauaji hayo ya albino ni ya kwanza mkoa
humo.
Alisema familia ya Shinga inaishi porini hivyo ilikuwa vigumu kupata
msaada kutoka kwa majirani. Kamada Rutta alitoa wito kwa wananchi na
raia wema kushirikiana na polisi kuwabaini na kuwakamata waliohusika
na mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment