Wapinzani watikisa Bunge

  Wasusia kikao kuunga mkono hoja ya Mbatia
  Sasa kuandaa hoja kuwaondoa Spika na Naibu

Baadhi ya wabunge wa upinzani, wakisusia kikao cha bunge kwa kutoka ndani ya ukumbi mjini Dodoma jana. Hatua hiyo ilikuwa ni kupinga uamuzi wa naibu spika Job Ndugai, kulikataa ombi la mbunge wa kuteuliwa James Mbatia, aliyeomba hoja yake binafsi kuhusu kuzorota kwa elimu nchini, iahirishwe hadi baadaye kutokana na baadhi ya hoja yake ya msingi kukataliwa.

Wabunge wa upinzani jana walitikisa Bunge kwa kususia kikao na kutoka nje kwa nia ya kuunga mkono msimamo wa James Mbatia (NCCR-Mageuzi ) wa kukataa kuhitimisha hoja binafsi iliyowasilisha bungeni bila kupatiwa nakala ya mitaala rasmi ya elimu nchini.
Kabla ya hatua hiyo, Mbatia, mbunge wa kuteuliwa alishinikizwa  na Naibu Spika Job Ndugai , kuhitimisha hoja yake bila kupatiwa nakala za mitaala rasmi ya shule za msingi na sekondari.

Mbatia alisema anazihitaji nakala hizo ili zithibitishe au kukanusha hoja binafsi aliyoiwasilisha bungeni juzi  kuwa hakuna mitaala rasmi ya elimu.

Baada ya wapinzani hao kutoka nje,  walitoa tamko ambapo Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tindu Lissu alisema wanaandaa hoja ya kupeleka bungeni kuwaondoa  Spika Anna Makinda  na Naibu wake  Ndugai.

Viongozi hao wanaondelewa  kwa maelezo kuwa hawana imani nao kwa vile wanaendesha vikao vya Bunge bila kufuata kanuni na pia kuwepo na upendeleo bungeni.

Tofauti za kiitikadi ziliibuka tangu juzi pale Mbatia alipowasilisha bungeni hoja ya udhaifu wa sekta ya elimu nchini na kuomba Bunge liunde Kamati Teule kuuchunguza.  Hata hivyo, pendekezo la Mbatia lilikwama baada ya Spika Makinda, kuitisha kura za ndiyo na hapana ambapo  wabunge wa CCM walio wengi walipinga kuundwa  kamati teule.  Lissu alisema hoja iliyowasilishwa na Mbatia ni muhimu lakini inazimwa ili isijadiliwe.
Alisema ukiachilia mbali suala hilo ni kwamba  kuna maamuzi mengi yametolewa  lakini  Spika anayakalia bila kutoa maelezo.

 “Kuna rufaa zaidi ya 10 amezikalia …..Bunge wanaliendesha ki-CCM sisi hatupo kwa ajili ya chama tawala ila kwa ajili ya wananchi sasa zinapotokea hoja kubwa ambazo zina maslahi ya taifa na kutaka kuzizima ili tusizijadili hatupo tayari kwa hilo ndiyo maana tunasema hatuna imani na Spika na Ndugai,” alisema.

Alisema Bunge lilipoanza waliomba wajadili suala la wananchi wa Mtwara lakini walitakatiliwa na kuelezwa kuwa  kamati ya wabunge itaundwa kufuatilia jambo hilo.
 Alisema pamoja na hilo  kikao chao kimeazimia kupeleka hoja ya Spika na Naibu wake kama dharura bungeni  juu ya suala hilo ili lijadiliwe.

Pia wamemtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Shukuru Kawabwa, kujiuzulu na kama hatafanya hivyo mamlaka ya uteuzi kumfukuza,  bila hivyo watapiga kura za kukosa imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa hatua ya kulidanganya Bunge na wananchi juu ya mitaala.

Alieleza kushangazwa na  Waziri Kawambwa aliyetakiwa kuonyesha mtaala wa elimu badala yake aliwasilisha kipande cha karatasi ambacho hakumpatia Mbatia  ili kuthibitisha ama kufuta kauli yake.

Lissu alisema kitendo hicho ni uchakachuaji wa mitaala na kulidanganya Bunge wakati  hakuna mitaala ya elimu.

Alisema watatafuta fursa ili kuhakikisha kuwa kunaandaliwa kanuni ya kuendesha Bunge la vyama vingi badala ya mfumo uliopo sasa. Mbunge wa Vunjo (TLP)  Augustino Mrema,   alisema mabilioni yaliyotolewa na Marekani kwa ajili ya kutengeneza mitaala, yametumika kiujanja  huku  uchapishaji wa vitabu ukifanyika nje.

Alisema hayo ni  matumizi mabaya ya fedha kwani uchapishaji ungefanyika nchini na kutoa ajira kwa vijana.

Alikumbusha kuwa tangu  mwaka jana Mbatia aliomba mtaala kwa  Kawambwa lakini  ameshindwa kuuwasilisha bungeni licha ya kuahidi kuuleta  bungeni.
“Mapambano yameanza rasmi  lengo ni kuikomboa nchi ili kupata maendeleo bila ubabaishaji.”

Mtoa hoja  Mbatia alisema  anataka kuona taifa linakuwa na elimu endelevu kama nchi nyingine zinavyofanya katika sekta hiyo. Alisema tangu uhuru mwaka  1961 hakuna mtaala rasmi wa elimu na lengo lake  kudai mtaala huo ni kutaka kufuta kauli  aliyoitoa kama alilidanganya Bunge na kumshangaa Kawambwa kufanya ujanja katika suala nyeti.

Alitaka  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua  fedha zilizotolewa ili kufahamu madudu yaliyopo katika wizara hiyo na kujionea jinsi zilivyotumika katika kuandaa vitabu ambavyo havina viwango.

 Kwa upande wake Naibu Spika, Ndugai alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alisema kanuni zinaruhusu kutoa hoja ya kutokuwa na imani kwani ni haki yao kueleza hilo.

Alipinga kuwa anakiuka kanuni za Bunge na kuipendelea  CCM na kwamba amekuwa mara nyingi akiupendelea upinzani, hivyo waliotakiwa kulalamika ni wabunge wa CCM.

 Hali ilikuwa hivyo jana baada ya Naibu Spika kumtaka Mbatia ahitimishe hoja yake. Mbatia aliomba mwongozo akiomba kupata kwanza  nakala hizo ili ajiridhishe kwa kuwa utafiti wake ni wa kweli ama anahitaji kuomba radhi.

Mbatia akizungumza kwa unyenyekevu alimuomba Spika kutumia busara na hekima na kulitendea haki taifa kwa kufanya maamuzi yenye manufaa kwa wananchi kama inavyoeleza dua ya kuliombea Bunge na taifa.

Alisema inashangaza kuona Waziri akitangaza bungeni kwamba kuna mitaala rasmi lakini mbunge anapoomba kuiona hapewi.

"Nimeomba kwa watendaji wake hiyo mitaala sijapata, kwanini tunailinda hiyo taasisi ya uendelezaji wa mitaala?  …. tunaendelea kulisha sumu watoto wa Tanzania na uozo huu?" alihoji.
Alisema "Mheshimiwa Naibu Spika tumwogope Mwenyezi Mungu, kwa moyo wa uchungu kabisa na hili nalifanya ‘above political ideology,’ suala la elimu halina itikadi ya chama, taifa hili linapoangamia haliangalii CCM, CUF, Chadema wala NCCR-Mageuzi, Mheshimiwa Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira), alipokuwa Naibu Waziri wa Elimu ya Juu tuliyazungumza haya Oktoba 14, 2006 kwenye ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni."

Alisema katika mazungumza hayo walijadili namna ya kuondoa tofauti za kielimu hapa nchini.  Alisema Novemba 30, 2008 alitoa kitabu akihoji 'tunataka kukumbatia giza au nuru' ambacho kilikuwa kwa maslahi ya Watanzania wote.

Alisema elimu pekee ndiyo mkombozi wa Tanzania lakini watoto wanaofundishwa sasa hawapewi elimu ya kuwasaidia kulikomboa Taifa. Alisema hali hiyo inachochea wananchi kuasi na kwamba wabunge wanayo nafasi ya pekee kubadilisha mwenendo huo kwa kuisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya nchi.

"Hivi tunajisikiaje Rais wetu anaposimama na kueleza kwamba mitaala yetu inatuongoza hivi na vile? Tunampa heshima gani wakati mitaala hii hatuioni? Waziri Mkuu anahitimisha mara kwa mara akieleza mitaala yetu iko hivi na hivi mbona hatuioni?" alihoji.

Baada ya maelezo hayo Ndugai alimtaka Mbatia kueleza anatumia kanuni ya ngapi ya Bunge kuomba kufanya hivyo.

Mbatia alisimama na kueleza kwamba anatumia kanuni ya 69(1) inayomruhusu mbunge kuomba kuhairishwa kwa Bunge au hoja ya kuahirisha mjadala kwa kutoa sababu za ombi lake.
Alisema ameomba hoja yake iahirishwe hadi atakapopata nakala ya mitaala rasmi.

Hata hivyo, Ndugai alisema kifungu kinachofuata cha kanuni hiyo kinamruhusu kutumia busara kuamua kuahirisha mjadala ama vinginevyo hivyo busara yake inamtuma kumwagiza Mbatia ahitimishe hoja yake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliahidi kwamba serikali italeta nakala za mitaala hiyo kabla ya kuahirishwa kwa Bunge Februari 8, mwaka huu.

Mbatia alipomaliza kuzungumza, Ndugai alisema kwamba kutotekelezwa kwa ahadi ya serikali hakuzuii hoja za Bunge kuendelea hivyo kumtaka tena ahitimishe hoja yake jambo lililoibua hasira za wabunge wa upinzani na kutoka nje.

Awali, Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, alisisitiza umuhimu wa kutekelezwa kwa ombi la Mbatia akieleza kwamba kutowasilishwa bungeni mitaala hiyo kunadhihirisha kuwa Waziri anawababaisha wabunge na kuwadharau.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alisema hakuna mitaala rasmi na badala yake kilichopo ni rasimu iliyochapwa mwaka jana.

No comments:

Post a Comment