Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo
alikuwapo wakati askari wake walipoingilia msafara huo na kusababisha
vurumai kubwa.
Waombolezaji hao walikuwa wakiuhamisha mwili wa
marehemu Fungungu kutoka Hospitali ya Runzewa kuupeleka katika Hospitali
ya Geita.
Sakata hilo la ndugu na polisi lililotokea saa
nane mchana juzi Jumamosi katika Pori la Samina, Geita na polisi wakiwa
kwenye magari matatu wakiwa wamesheheni silaha mbalimbali walifika na
kuzuia mwili wa marehemu kusafirishwa.
Baadhi ya ndugu wa marehemu akiwamo mkewe,
wanadai kwamba Fungungu alifariki dunia baada ya kupigwa risasi na
polisi wanaosemekana kwamba walimvamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia
Alhamisi iliyopita kisha kupora mamilioni ya fedha. Wanadai kwamba
alipigwa risasi tumboni na kichwani katika Kijiji cha Runzewe, Wilaya ya
Bukombe mkoani hapa.
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa kiasi cha
Sh360 milioni kiliporwa. Kati ya fedha hizo, Sh60 milioni zinadaiwa
kwamba zilikuwa kwenye gari wakati Sh300 milioni zilikuwa kwenye
masanduku mawili yaliyokuwa ndani ya nyumba.
Pia ndugu hao walidai kwamba Sh1.2 milioni
zilichukuliwa na askari wawili wa kiume baada ya kumpekua mke wa
marehemu kwenye nguo za ndani.
Pia askari hao wanadaiwa kupora mali
mbalimbali za marehemu zikiwamo redio mbili, video kamera moja, nguo za
marehemu ikiwamo kanzu, mashine ya printer, mashine ya inventor,
karatasi za picha, deki mbili za kucheza CD, pamoja na nguo za mke wa
marehemu.
Mapema Kamanda Paulo alikuwa ameeleza kuwa
marehemu alijiua mwenyewe baada ya kumjeruhi Polisi, Fortunatus Beatus
kwa risasi lakini taarifa hizo zimepingwa vikali na ndugu na jamaa wa
marehemu ambao wanadai marehemu aliuawa na polisi akiwa nyumbani kwake.
Polisi kuzuia waombolezaji
Baada
ya polisi kuyasimamisha magari manane yaliyokuwa katika msafara huo wa
kupeleka mwili wa marehemu kwenda kuhifadhiwa katika chumba cha maiti
Hospitali ya Geita, kulizuka mabishano makali kati ya Kamanda Paulo na
ndugu wa marehemu.
Inadaiwa kwamba polisi walikuwa wakishinikiza
mwili huo urejeshwe Runzewe, Bukombe kwa kuwa tayari ulikuwa umefanyiwa
uchunguzi jambo ambalo liliwakera waombolezaji hao.
Kabla ya kamanda huyo kufika eneo hilo,
msafara huo ulisimamishwa na Polisi wa Usalama Barabarani ambao walikuwa
wamefuatana na wale wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakiongozwa na Mkuu wa
Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita, Leonard Makona.
Baada ya
kuusimamisha msafara huo, Makona aliwataka ndugu wa marehemu kumsubiri
Kamanda Paulo ambaye alifika baada ya takriban dakika 10.
Mwandishi wa habari hii ambaye alikuwa katika eneo la tukio, alishuhudia ndugu wa marehemu na Kamanda Paulo wakirushiana maneno.
“Mnapeleka wapi mwili wa marehemu, ina maana
hamkuridhika na uchunguzi wa daktari wa Bukombe?” alihoji kwa ukali na
kujibiwa pia kwa ukali na kaka wa marehemu, Mariatabu Fungungu: “Kwa
nini mnatusimamisha? Tunaomba tuite waandishi wa habari hapa ili waje
washuhudie tukio hili. Kwa nini msikae ofisini?”
Baadaye, kamanda huyo aliwaamuru askari wake kuwaingiza katika
gari la polisi ndugu watano wa marehemu wakiwamo mke wa marehemu, Lucia
Kilaza (23) na Mariatabu. Walifanya hivyo kwa kutumia nguvu na kisha
kuondoka nao hadi katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita.
Ndugu wa marehemu walilalamikia kitendo hicho wakisema kilikuwa na lengo la kuficha ukweli wa tukio hilo.
Mke wa marehemu
Kilaza
alidai kuwa kifo cha mumewe kilitokea baada ya zaidi askari 20 kuvamia
nyumbani kwake yapata saa tisa usiku na kumwamuru Fungungu kutoka nje na
alipogoma, ndipo walipoanza kupiga risasi na kuvunja vioo vya madirisha
na milango na risasi kumpata marehemu. Pia alidai kuwa walipiga mabomu
ya machozi.
Alisema baada ya tukio hilo, walivunja mlango
na kuingia ndani kisha kumchukua mumewe ambaye tayari alikuwa amefariki
na kumtupa nje... “Mimi pia walinichukua wakanitupa nje ya uzio baadaye
wakaanza kunipekua nguo za ndani na kuchukua Sh1.2 milioni ambazo
nilikuwa nimezificha baada ya kuona wameanza kufyatua risasi.”
Wakizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Bukombe,
Profesa Kalikoyela Kahigi na Diwani wa Runzewe, Yusufu Fungameza
walisema Serikali inatakiwa kuingilia kati suala hilo ikiwa ni pamoja na
kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika katika tukio.
Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda
Paulo aliwaahidi waandishi wa habari kwamba angelitolea ufafanuzi jana
Jumatatu. Hata hivyo, alishindwa kufanya hivyo kwa madai kwamba anapisha
kwanza uchunguzi wa mwili wa marehemu kwenye Hospitali ya Geita.
Ndugu wa marehemu wamegoma kuuzika mwili wa
marehemu wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike kwa kutumia jopo maalumu la
madaktari huku wakiitaka Serikali kuunda tume kuchunguza tukio hilo.
Mtandao wa ujambazi Mbeya
Katika
hatua nyingine; Watu wanaodaiwa kujihusisha na matukio ya uhalifu
katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Morogoro na Dar es Salaam wamenaswa na
polisi huko Mbeya.
Mtandao huo unadaiwa kuwahusisha askari mmoja wa
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU) pamoja na wafanyabiashara maarufu wa Mbeya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani
Athumani alisema jana kuwa watu 29 wanaodaiwa kujihusisha na mtandao huo
wanashikiliwa na jeshi hilo.
“Askari hao mbali na kujihusisha na matukio ya
ujambazi moja kwa moja, pia walikuwa na tabia ya kuwaazima majambazi
sare za jeshi ambazo zilikuwa zikitumika kwenye matukio mbalimbali ya
uhalifu,” alisema.
Alisema watuhumiwa wote hao wanakabiliwa na
tuhuma za mauaji, ujambazi na kupokea mali za wizi na walikamatwa katika
maeneo ya Mkwajuni, Chunya na Makambako na Mafinga, Iringa.
Kamanda Athumani alisema kuwa watuhumiwa 13
watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ujambazi, mauaji na kupokea
mali za wizi, wengine saba watasafirishwa kwenda Iringa ambako ndiko
watakakofikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kamanda Athumani alisema uchunguzi wa
watuhumiwa wengine 16 bado unaendelea na wataachiwa kwa dhamana na
watatakiwa kuripoti vituo vya polisi watakavyopangiwa.
No comments:
Post a Comment