Spika wa Bunge,Anne Makinda
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda ameongezewa ulinzi
pamoja na kubadilishiwa namba za gari analotumia kutokana na vitisho
anavyovipata kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakimtumia ujumbe wa
simu.
Taarifa ambazo Mwananchi imezipata
zinaeleza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa Chadema kutoa
namba za Spika na kuzigawa kwa wafuasi wake waliofika kwenye mkutano
uliofanyika kwenye Viwanja vya Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam hivi
karibuni ili wamtumie ujumbe mfupi wa simu.
Hivi karibuni gazeti hili liliripoti kuwa
Spika Makinda amepokea ujumbe mfupi wa simu zaidi ya 400 na kupigiwa
simu zinazofikia 200 za kumkashifu na vitisho.
Taarifa zilizopatikana
jana zinaeleza kuwa Spika Makinda amekuwa akitumiwa ujumbe mfupi wa
vitisho ambavyo inaonyesha kuwa wananchi wana hasira naye na ndiyo maana
ameongezewa ulinzi.
Vyanzo vyetu vya habari vimeeleza kuwa gari la
Spika Makinda limebadilishwa namba kwa kuondolewa herufi S ambayo
humaanisha Spika na kuwekwa namba nyingine ambazo bado hazijajulikana.
“Watu wanaomtumia ‘meseji’ wana hasira,
wanaweza kumdhuru na ndiyo maana ameongezewa ulinzi. Hata magari yake
aliyokuwa akitumia yamebadilishwa na kupewa mengine tofauti,” kilieleza
chanzo chetu cha habari.
Spika Makinda mwenyewe alipopigiwa simu ili
kueleza kuhusu suala hilo la kuongezewa walinzi simu yake ilikuwa ikiita
tu bila kupokelewa.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah naye
simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.Tangu Chadema wagawe namba
hiyo baada ya kumtuhumu Spika pamoja na msaidizi wake, Job Ndugai kuwa
amekuwa akipindisha kanuni wakati wa kuliongoza Bunge.
Taarifa zilieleza kuwa wamekuwa wakisumbuliwa
na kutumiwa ujumbe za vitisho.Wakati hayo yakitokea, tayari Ofisi ya
Bunge imesema itawachukulia hatua kali wale wote waliotumia lugha chafu
kwa ujumbe mfupi ama kupiga moja kwa moja kwa Spika na Naibu wake.
Katibu Mkuu wa Bunge, Dk Kashililah juzi
alisema kuwa kutoa namba si tatizo, bali kuzitumia namba hizo kinyume na
taratibu ndiyo haitakiwi, jambo ambalo linaweza kusababisha baadhi yao
kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Wote waliotoa lugha za matusi kwa Spika
Makinda na Naibu Ndugai watachukuliwa hatua za kisheria. Tutawatafuta
kwa njia zote, hii itasaidia kuwa fundisho kwa watu wenye tabia kama
hizo ambao wanapewa namba kwa manufaa ya wananchi, lakini wanazitumia
kinyume chake,” alionya Kashililah.
“Tutawasaka kwa kila hali, tutawabaini tu kwa
kushirikiliana na idara mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na Polisi ili wachukuliwe hatua kali.”
Mkurugenzi wa
Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alipoulizwa jana kuhusu msimamo
wa chama chake baada ya kutoa namba hizo kwa wananchi alisema; “Bunge
halijatuuliza ila wakituuliza tutajibu.”
No comments:
Post a Comment