JESHI la Polisi mkoani Mwanza kwa kusaidiana na
maofisa wa Benki ya NMB imewatia mbaroni watu watatu ambao wanadaiwa
kuiba kiasi cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti.
Watuhumiwa hao wamenaswa baada ya kuwekewa
mtego na maofisa wa benki na polisi kwenye saa 6.00 usiku wa Februari
10, mwaka huu na mtuhumiwa mmoja alibambwa akichukua fedha katika ATM ya
NMB kwenye Tawi la PPF Plaza Mwanza.
Baada ya kunaswa kwa mtuhumiwa huyo, alisaidia
kuwaelekeza polisi walipo wenzake, ambao walikutwa katika hoteli moja
jijini Mwanza wakiwa wamejipumzisha.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mwanza, Christopher Fuime
alisema pia walikamata vifaa mbalimbali ambavyo walikuwa wakitumia kwa
ajili ya kufanyia uhalifu huo.
“Kwa muda mrefu sasa Jeshi letu lilikuwa
likihangaika na wahalifu wa aina hiyo kwani tangu Oktoba 2012 tumekuwa
tukipokea kesi mbalimbali za wizi wa fedha katika akaunti zao, lakini
tumefurahi tumewatia mbaroni,” alieleza Fuime.
Kamanda Fuime alidai kuwa tangu kutiwa mbaroni kwa watuhumiwa hao, hawajasikia malalamiko ya wizi tena.
Alisema polisi walikuwa wakipata wastani wa malalamiko 15 katika kipindi cha siku 14.
“Hawa
jamaa inaelekea ndiyo vinara wa wizi huu, ingawa haina maana kwamba
kukamatwa kwao uhalifu huu utapungua. Wizi huu una mtandao mpana sana
kwa vile hata wahalifu hao wamedokeza kuwa wamekuwa wakishirikiana na
wataalamu wa kompyuta kutoka nchini Bulgaria,” alisema.
Vifaa walivyokamatwa navyo
Vifaa
vilivyokamatwa navyo ni kadi za bandia 194 za kuchukulia fedha katika
ATM za Benki ya NMB, ambapo kati yake kadi 95 zilikuwa na namba
0225152975 zinazotumia namba ya akaunti ya 2258103695 zenye jina na
picha ya mtu anayedaiwa kuwa ni mtumiaji mwenye jina la Molely L. P.
Kadi nyingine 99 zilikuwa na namba 0506056317 za akaunti namba
5068000322 zikitumia jina moja la Mnuo Z. E na picha moja.
Mbali na kadi hizo pia waliweza kunasa kadi 36
za Benki za DTB, ambazo kati yake kadi 18 zilikuwa na jina moja la
Kelvin G. Gratias na namba 20497883, kadi 12 zikitumia jina la John J.
Paul zenye akaunti namba 2049783 huku kadi sita zikitumia jina moja la
Joseph Donald akaunti namba 2049783.
Kadi nyingine tatu zenye maandishi ya Download
List na nyingine ikiwa ni kadi ya Visa ya Benki ya KCB yenye namba
4183546040003827 zikitumia jina la Elikana Zacharia. Kadi nyingine
zilikuwa ni tupu zisizo na maandishi wala nembo ya benki yoyote na
nyingine zikiwa ni Soviet Royalty, kadi ya raia ya Urusi ikiwa na namba
000724.
Pia walikutwa na kadi ya Benki ya Amerikani yenye namba 549012345678 zilizokuwa zikitumia jina la Richard Croswell.
Walikamatwa pia wakiwa na vifaa mbalimbali vya
kielektroniki ikiwamo kamera za siri tatu za kienyeji ambazo
zimetengenezwa kwa kufungwa betri za simu ya mkononi na pia walikamatwa
na kifaa cha kutengenezea kadi bandia (Magnetic Card reader), mikebe
mitatu ya rangi za kupulizia kamera za usalama katika ATM ili
wasionekane wakati wa wizi wao, ‘printer’ pamoja na kifaa cha kuchomea
vifaa vya umeme.
Wizi ulivyofanyika
Wahalifu hufika katika
mashine za kutolea fedha ambapo hatua ya kwanza ni kuzima kamera za
usalama za eneo husika kwa kuzipulizia rangi maalumu ili kuzitia ukungu
hivyo kuharibu mwonekano wake na kuruhusu wao kuingia eneo hilo bila ya
kuonekana na kufanya wizi wao.
Mara baada ya kuziharibu kamera za
usalama, walikuwa wakianza kwa kuweka kamera zao za siri ili kunasa
namba za siri za kufungulia akaunti ambazo huzisoma katika ‘kompyuta’ na
kuzinakili katika daftari lao maalumu na kisha kuchukua kadi zao bandia
na kuchukua fedha.
Wizi huo wa kuchukua fedha waliufanya nyakati
za usiku saa sita hadi saa tisa usiku wakati ule wa kutegea kamera zao
ulifanyika muda ambao huwa na wateja wengi hasa siku za mapumziko.Hatua za benki kuzuia wizi huo:
Meneja wa Benki ya NMB, Kanda
ya Ziwa, Straton Chilongola alipoulizwa kuhusiana na wizi huo alisema
kwamba jambo hilo linashughulikiwa na Polisi, hivyo yeye hana maelezo ya
ziada.
“Naomba kama mnataka suala hili fuatilieni
polisi kwa vile wahalifu wote na kesi kwa jumla inashughulikiwa huko,
kwa upande wangu mimi siyo msemaji wa benki kulingana na uzito wa suala
hili,” alisema.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya benki hiyo
zilieleza kwamba kutokana na kuongezeka kwa malalamiko ndani ya wateja
wao walilazimika kuweka watu katika mitambo yao ya kamera ikiwa ni
pamoja na kufuatilia kwa ukaribu nyendo za wizi huo ambapo waliweza
kubaini muda na wakati ambao wamekuwa wakiingia na hivyo kuwasiliana na
maofisa wa Polisi kwa lengo la kuweka mtego.
Idadi ya malalamiko ya wateja
Kaimu Kamanda
Fuime alieleza kwamba, tangu kipindi cha Oktoba 5, 2012 hadi Februari
10, mwaka huu kitengo cha jeshi hilo kwa njia ya uhalifu wa njia ya
mtandao (Cyber Crime) kiliweza kupokea jumla ya malalamiko 135 na
kuyafungulia majalada ya uchunguzi wa wizi huku wastani wa kupokea
malalamiko kwa siku moja ukiwa ni kesi 15.
No comments:
Post a Comment