MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa
Ibrahim Lipumba amesema ni aibu kwa Tanzania kutumia takwimu za miaka ya
nyuma ambazo zinatumia gharama kubwa kifedha na muda mwingi badala ya
kuwa njia mbadala na rahisi ya kupata takwimu kwa wakati.
Lipumba alisema hayo jana wakati akizungumza
machache kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa Mpango wa Sauti za Wananchi
ambapo alitoa pongezi kwa Taasisi ya Twaweza kwa juhudi zao za kutumia
simu za mkononi ili kupata maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Profesa huyo alisema jitihada hizo
zitawawezesha kukusanya taarifa kwa njia ya simu ambayo itatumia gharama
ndogo lakini kwa ufanisi pia ina uwezo wa kuwafikia Watanzania waishio
kila upande wa nchi. “Tunahitaji kujua taarifa halisi zinazogusa maeneo
ya wananchi ambayo Serikali inatakiwa kuyafanyia kazi kupitia sera
zake,mfano Sera ya Serikali ya wazee ambayo inawataka wapate matibabu
bila malipo, je inafanya hivyo…,hivyo kupitia mpango huu tunaweza kupata
taarifa halisi,”alisema.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela
Kariuki alitoa pongezi kwa niaba ya Serikali kwa Twaweza ambao ndio
waandaaji wa mpango huo akisema una umuhimu kwa wananchi na kwa Serikali
pia katika kupata maoni yao na kuandaa sera ambazo zinakidhi haja na
matakwa ya wananchi.
Kariuki alisema mpango huu ni wakupata maoni
mbalimbali kutoka kwa wananchi hususani yanayohusu afya,elimu na maji,
ili kujua ni jinsi gani sekta hizi zinatoa huduma kwao namna ambavyo
Serikali inawajibika.
No comments:
Post a Comment