MAKADA watatu wa CCM mkoani Arusha wameendelea
kumng’ang’ania Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema baada ya
kuwasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya marejeo ya hukumu iliyomrudisha
bungeni mbunge huyo.
Lema alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha, Aprili 5, 2012 kutokana na kesi iliyofunguliwa na
wanachama watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel,
wakipinga ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilimrejesha
bungeni Lema baada ya kushinda rufaa yake aliyokata mahakamani hapo
akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Makada hao wa CCM
hawakuridhika na hukumu hiyo na sasa wamewasilisha maombi mahakamani
hapo, wakiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya hukumu hiyo huku
wakianisha hoja kadhaa za kupinga hukumu hiyo.
Katika hukumu yake, iliyosomwa na Naibu
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu, Desemba 21, 2012,
Mahakama ya Rufani ilitengua hukumu ya Mahakama Kuu na ikamthibitisha
rasmi Lema kuwa ni mbunge halali wa Arusha Mjini.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji
Bernard Luanda kwa niaba ya jopo la majaji wenzake wawili waliokuwa
wakisikiliza rufaa hiyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa warufani
hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo
ya uchaguzi yaliyompa ushindi.
“Rufaa imefanikiwa na tunatengua hukumu, tuzo
na amri ya Mahakama Kuu.Tunamtangaza mrufani kuwa Mbunge wa Arusha
Mjini,” ilisema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo na kuwaamuru
wajibu rufaa kulipa gharama za rufaa hiyo.
Hata hivyo, makada hao katika maombi yao hayo
wanaliomba jopo la majaji hao lifanye marejeo ya hukumu yake hiyo ama
mahakama kupitia kwa jopo jipya la majaji isikilize upya rufaa hiyo na
kutoa uamuzi wa rufaa hiyo ya Lema.
Sambamba na rufaa hiyo, pia makada hao wa CCM
wanaomba rufaa yao waliyokata pia wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu
Arusha (Cross Appeal), ishughulikiwe haraka.
Katika maombi hayo,
makada hao kupitia kwa wakili wao Alute Mughwai wanadai kuwa sababu
zilitolewa na jopo hilo la majaji kuhusiana na haki yao ya kisheria
kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi inapingana na uamuzi mwingine
wa mahakama hiyo.
Wanabainisha mkinzano huo kuwa ni katika aina
ya sheria ambayo inapaswa kutumika, ambayo ni ya Sheria za nchi za
Jumuiya ya Madola na Sheria ya Uchaguzi ya Taifa, huku wakibainisha kuwa
mkinzano huo katika suala moja unaharibu hadhi ya mahakama.
Pia
wanadai mahakama ilikosea iliposema kuwa hapakuwa na ushahidi katika
kumbukumbu za mahakama kuonyesha kuwa wao walikuwa ni wapigakura
waliojiandikisha.
Wanaongeza kuwa pia mahakama hiyo ilikosea
kusema kuwa haki ya mpigakura katika kupinga matokeo ya uchaguzi yana
mpaka na kwamba ni kwa jambo ambalo linahusiana na uvunjwaji wa haki zao
za kupiga kura tu.
Katika rufaa yake, Lema kupitia kwa mawakili
wake, aliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, lakini
katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufaa iliibua na kutolea uamuzi hoja
mpya ambayo haikuwa imetolewa na upande wowote.
No comments:
Post a Comment