WANAUME waliooa wanawake wenye mishahara mikubwa
au vyeo kuwazidi wao, huathirika kisaikolojia wakati wa tendo la ndoa
na wengi wao hutoka nje ya ndoa. Utafiti umebaini.
Utafiti huo uliofanywa katika nchi za Denmark na
Marekani umebaini kuwa wanaume wanaopata mshahara mdogo, hawashiriki
tendo la ndoa kwa ufanisi na wake zao walio na mishahara mikubwa,
ukilinganisha na wanaume walio na kipato kikubwa kuwazidi wake zao.
Msaidizi katika utafiti huo Dk Lamar Pierce ambaye
pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Mipango katika Chuo Kikuu cha
Washington alisema kuwa wanaume huwa dhaifu kiutendaji katika tendo la
ndoa, inapotokea mwanamke ana cheo au kipato kikubwa kuliko yeye. Hata
hivyo, utafiti huo haukuwahusisha wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa.
Mtafiti huyo alisema kuwa hali hiyo ni mbaya zaidi
katika nchi za Afrika, ambapo mfumodume umetawala huku mapinduzi ya
kijinsia yakianza kushika kasi.
Dk Pierce alifanya utafiti huo kwa kuchunguza
taarifa za sampuli zaidi ya 600,000 za wakazi wa Denmark, ambapo
wanandoa wenye umri wa kuanzia miaka 25 hadi 49 walichunguzwa, kuanzia
mwaka 1997 hadi 2006.
Ilibainika kuwa kwa mabadiliko ya kijamii katika
siku za hivi karibuni, wanawake wamekuwa watafutaji wakuu kuliko
wanaume, yamevunja tamaduni na wajibu wa mwanamume, hali inayowaathiri
kisaiokolojia wanaume.
“Hamu ya tendo la ndoa na ufanisi vinahusiana kwa
karibu na kipato, mitandao ya marafiki, cheo na ile hadhi ya mwanamume
kuwa kiongozi katika familia,” alisema.
Akizungumzia utafiti huo Dk Kitila Mkumbo,
Mhadhiri Mwandamizi katika Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
alisema kuwa madhara wanayoyapata wanandoa wa aina hiyo yanasababishwa
na tamaduni na mfumodume.
Alisema mila na desturi zinawafanya wanaume wasijiamini pale wanapochangia kidogo katika familia.
“Iwapo mwanamume atamchukulia mke wake kama rafiki
na siyo msaidizi wa nyumbani, hawezi kuathirika, tatizo kubwa ni kuwa
wanahisi kukosa hadhi ya ‘ubaba’,” alisema Mkumbo.
Alisema kwamba wanaume wengi wa aina hiyo hutoka
nje ya ndoa zao kuwatafuta wanawake wanyonge zaidi yao, ambapo hupata
faraja ya tendo la ndoa.
Aliongeza: “Wanaume wengi, ambao wake zao wana
hadhi na kipato kikubwa, mara kwa mara huwa na hasira, ukali bila
sababu, mambo ambayo husababisha waikose raha ya tendo la ndoa kwa wake
zao.”
Hata hivyo, Dk Mkumbo alisema kuwa baadhi ya
wanawake huonyesha dharau kwa waume zao pindi wanapopandishwa vyeo au
kuongeza kipato, jambo linalowaathiri wanaume.“Vyeo, fedha nyingi hasa
kwa upande wa wanawake, ndicho chanzo cha kuanguka kwa ndoa nyingi,
iwapo tu wanandoa hao hawatakuwa makini,” alisema na kuongeza:
“Wanandoa wanapaswa kuongozwa na upendo, badala ya ndoa yao kuongozwa na mali.”
Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano aliyesajiliwa na
Global Source Watch, Dismas Lyassa alisema kwamba utafiti huo una ukweli
kwa kiasi kikubwa katika dunia ya sasa.
Alisema kutokana na mila nyingi, hata katika
vitabu vya dini mwanamke ameumbwa kama msaidizi na siyo mtafutaji, hivyo
mabadiliko hayo yanawaathiri wanaume.
“Zipo familia ambapo mwanamke mwenye kipato
anataka kufanya mapenzi pale anapotaka yeye tu, mume wake anapohitaji,
yeye husingizia kachoka. Hili linasababisha hata familia hizo ziwe na
watoto wachache,” alisema.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Kitengo cha Saikolojia, Chris Mauki alisema kuwa kipato kinaweza
kuathiri ndoa kutokana na tabia za wanandoa.
“Kasumba inaweza kuwa chanzo cha madhara katika
ndoa, ambayo mwanamke ana kipato kikubwa. Mwanamume mwenye kipato kidogo
anaweza kuhisi tu kuwa, anadunishwa wakati siyo kweli,” alisema Mauki.
Alisema kwamba kasumba hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu
ufanisi katika tendo la ndoa kwa sababu kwa kawaida ugomvi na malumbano,
uhusika moja kwa moja na tendo la ndoa.
Watafiti hao walisema kuwa hawana uhakika hasa
chanzo cha tatizo hilo, lakini kukosa fahari ya uanaume na mfumodume,
huweza kuchochea hasira na kutokujiamini.
Ilibainika kuwa wanaume wengi walitumia viagra au
dawa nyingine kuongeza nguvu za kiume, ili waongeze ufanisi kwenye ndoa
katika mazingira ambapo, mwanamke ana kipato kikubwa.
Cha ajabu katika utafiti huo ni kuwa, hali hiyo
haikuonekana kwa wanandoa ambao mwanamke alikuwa na kipato kikubwa tangu
kuanza kwa uhusiano.
Badala yake hali hiyo ilionekana kwa wanandoa
ambao awali mwanamke alikuwa na kipato kidogo kisha kikaongezeka wakati
wa uhusiano.
Watafiti hao walisema kuwa inawezekana wanaume
huathirika kisaikolojia na hutaka kuongeza nguvu ili waonyeshe ufahari
wao, ambao wameshindwa kuuonyesha katika kipato.
Alisema mabadiliko hayo huwafanya wanaume kuhisi vyeo vyao vimechukuliwa na hivyo kuathirika kisaikolojia.
Utafiti huo ulifanyika Denmark nchi ambayo inachochea zaidi haki za wanawake.
Hata hivyo, Dk Pierce alisema siyo vyema
kuhitimisha kuwa mishahara ya wanawake inawaathiri wanaume wote katika
tendo la ndoa, bali wapo wanaopenda kuoa wanawake wenye kipato kikubwa
kuwazidi. Mtafiti wa nchini Marekani, Dk Karen Robinson alisema wanawake
wenye vipato vikubwa au vyeo katika jamii, wanatakiwa waheshimu hisia
za wenza wao, badala ya kuchanganya nafasi zao, kipato katika maisha ya
ndoa. “Wanatakiwa waepuke maneno yanayoweza kuudhi au kuchochea
mfadhaiko wa kisaikolojia, ili kulinda ndoa,” alisema Dk Robinson.
No comments:
Post a Comment