Polisi wa kikosi cha kuzuia fujo FFU wakiwajibika katika kudhibiti maandamano ya waislamu jijini Bdar es Salaam
SHUGHULI katika Jiji la Dar es Salaam jana
zilisimama kwa muda baada ya wafuasi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda, kuandamana huku
wakipambana na askari polisi waliotanda katika maeneo mengi ya mji.
Wafuasi hao waliotawanywa mara kwa mara na kwa
mabomu ya machozi na askari polisi, walitumia stali mpya kuandamana hadi
kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kufikisha ujumbe
wao.
Vurugu hizo za polisi kupambana na waandamanaji
hao zilianza mchana baada ya swala ya Ijumaa hadi saa 9:00 alasiri huku
mitaa mingi katika jiji la Dar es Salaam ikiwa wazi kutokana na watu
wengi kuondoka maeneo hayo.
Watu hao waliandamana kushinikiza Ponda ambaye yupo ndanmi akikabiliwa kesi ya wizi na uvunjifu wa amani ashiwe kwa dhamana.
Watu hao walitokea katika misikiti mbalimbali ya
Jiji la Dar es Salaam baada ya swala ya Ijumaa ikiwemo, Kwamtoro,
Magomeni na Buguruni kuelekea ofisi za DPP zilizopo barabara ya Ohio na
Sokoine eneo la posta wakiwa katika vikundi vidogovidogo, tofuati na
mandamano ambayo yamezoeleka kufanyika.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam inawashikilia zaidi ya watu 90 ambao walishiriki kuhamasisha
na kufanya maandamano.
Kaimu wa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Mohamed Msangi alisema kati ya watu hao watawahoji ili kuwabaini
wahusika wakuu na kufikishwa mahakamani.
“Kama inavyofahamika wazi kwenye msafara wa mamba
kenge hawakosekani sasa tutawahoji ili tuweze kuwapata wahusika wakuu
na tuweze kuwachukulia hatua za kisheria kwani hao ni wavunjifu wa
amani,”alisema.
Msangi alisema jeshi hilo lilipiga marufuku
maandamano hayo lakini watu hao wamekaidi amri hiyo na kwamba sasa
watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kulikuwa na vikundi vya watu katika maeneo
ya Buguruni, Mnazi Mmoja na Kariakoo ambao walikuwa katika makundi huku
wengine wakiandamana katika makundi
“Tumeweza kuchukua hatua kwa watu waliyokuwa
wanataka kujaribu kuvunja amani kwa kufanya maandamano kwani
tumedhibiti hali hiyo na kuweza kuwakamata watu 80 ambao wapo katika
kituo cha Polisi Kati na Msimbazi,”alisema Msangi.
Alisema hali sasa ni shwali na kwamba vurugu ambazo zilitaka kujitokeza zimedhibitiowa.
Maandamano
Majira ya saa7:45 mchana askari
waliyokuwa wameva nguo za kiraia na wengine walikiwa katika sare za
Jeshi la Polisi walitanda njia zote zinazopita eneo la Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mshitaka nchini DPP huku wakitoa tahadhari kwa watu
waliokusanyika pamoja kutawanyika.
Kadri muda ulivyokuwa ukienda ndipo idadi ya askari ilivyozidi kuongezeka huku wakiwa wameshikilia silaha za moto.
Mbinu wazotumia askari
Askari
walikuwa wakitumia pikipiki za mikuu miwili maarufu kama boda boda
kuzungukia mitaa ya katikati ya jiji kwa lengo la kuwasambaratisha
waandamanaji hao.
Askari wengine walikuwa wakitumia magari ya kiraia
kuzunguka katika mitaa ya katikati ya jiji ambapo walipokuta
mikusanyiko ya watu walikuwa wakiwakamata na kuwachukua katika magari
hayo.
Msikiti wa Mtoro
Katika hali
ya kushangaza Imamu wa Msikiti wa Mtoro alisikika akiwatangazia waumini
wake kuwa waislam hawatakiwa kuogopa bali wanatakiwa kuandamana kwenda
kwa DPP.
“Ukiwa Muislamu hutakiwi kuogopa kutetea haki yako,siku ya
leo maandamano ni lazima,”alisema Kiongozi huyo ambaye jina lake
alikupatikana mara moja.
Baada ya tangazo hilo Waislamu hao,
walitawanyika na kujigawa mmoja mmoja kitu ambacho kilionekana
kuwachanganya Askari Polisi Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU).
Baada
ya kufika mbele ya jengo la polisi la Msimbazi watu hao walianza
kuungana kwa makundi na kufanya Polosi waliokua kwenye doria kuwazuia
kuendelea na safari na walipo kaidi agizo hilo walianza kuwafukuza kwa
kutumia mabomu ya machozi.
Msikiti wa Temeke Tungi
WATOTO
kuanzia miaka kati ya nane hadi tisa walionekana kwenye lango kuu la
kuingilia kwenye msikiti huo wakigawa vipeperushi ambavyo vilikuwa
vinawahamasisha waumini hao kuandamana hadi kwa DDP kwa kile
kilichodaiwa viongozi wa waislam hawapatiwi dhamana.
Kipeperushi
hicho kinasema “Kimsingi mfumokristo ndani ya Serikali unawahujumu
waislamu hivyo wanapaswa kuendelea kupambana kukataa kufanywa raia
daraja la pili.
IIiendelea kusomeka hivi, “tukumbuke madhalimu
hawarudi nyuma kama Shekh Ponda ataendelea kunyimwa haki yake ya dhamana
Alhamisi hii,mara baada ya swala ya ijumaa waislamu wote wanatakiwa
kuandamana kuelekea kwa DDP,akatueleze kwa nini viongozi wa waislamu
hawapati dhamana”
Ilipofika saa 6:20 mawaidha yalianza kwa
kuionya serikali kwa kutowadhamini waumini wa dini hiyo kwa kile
walichodai kutomtendea haki Sheikh Ponda kwa kutompa dhamana.
Mmoja
wa maimamu wa msikiti huo alisema walimwandikia barua DDP ili aweze
kukutana nao kujadili suala la kupewa dhamana hiyo lakini akawataka
wakutane Februali 28 mwaka huu.
Hali tete Buguruni
Kilionekana
kikundi cha dini ya kislamu wakiandamana huku wakiimba Takbir
wakielekea Kariakoo lakini walitawanywa kwa kurushiwa mabomu ya machozi
na askali wa jeshi la polisi waliokuwa zaidi ya saba waliojazana kwenye
Defender moja.
Baadaye lile kundi liliungana na waislamu kutoka
msikiti wa Ilala ambao walitupiwa mabomu ya machozi zaidi ya manne ili
kuwatawanyisha waandamanaji hao na kusababisha magari kusimama zaidi ya
dakika 30.
Lile kundi lilikutana na kupitia njia za mkato ambapo
walitokea maeneo ya mtaa wa Jangwani kuelekea barabara ya Msimbazi ndipo
polisi walipowabaini na kuwatupia mabomu ya machozi na kusababisha
mwanafunzi mmoja kuzimia.
Kariakoo
Maduka mengi katika eneo la Kariakoo yalifungwa kwa hofu ya kuvamiwa na kuibiwa bidhaa na waandamanaji hao.
Mwananchi lilifika katika maeneo hayo muda wa saa 7.00 mchana na kukuta eneo hilo likiwa na watu wengi kama ilivyo kawaida.
Watu
mbalimbali ambao hujipatia kipato kutokana na shughuli mbalimbali
sokoni hapo walilaani kufungwa kwa biashara siku ya jana wakisema kuwa
inawafanya wakose kipato cha siku.
“Hawa waislamu wanatukosesha uhuru
wa kufanya kazi, mpaka sasa walau mtu ungekuwa umapata chochote kwa
kazi zetu lakini maduka yamefungwa na sisi tunakosa kazi” alisema mtu
mmoja aliyefahamika kwa jina la Muddy ambaye ni mbeba mizigo wa soko la
Kariakoo.
Shule zafungwa
BAADHI ya shule zilizopo katikati
ya jiji zililazimika kusitisha masomo jana kwa kuhofia maandamano hayo.
Miongoni mwa Shule zilizofungwa ni pamoja na Shule ya Msingi Bunge
Hata
hivyo, eneo hilo lilikuwa na ulinzi wa kutosha kwani baadhi ya barabara
za kuelekea katika ofisi hiyo zilikuwa zimefungwa na hakuna mtu
yeyote aliyekuwa akikatiza katika eneo hilo.Magari pia hayakuwa
yakipita katika eneo hilo.
Katika kuimarisha ulinzi, Polisi
walilazimika kutumia pikipiki, magari na mbwa kufanya doria katika
maeneo yaliyo karibu na ofisi ya DPP.
Kadhalika, Polisi walikuwa
wanatumia magari binafsi ambayo ndani yake kulikuwa na askari
waliovalia kiraia jambo ambalo lilisaidia kuwakamata baadhi ya
waandamanaji kiurahisi. Kutokana na hilo kila kiku
ndi kilichojaribu kupita kuelekea kwa DPP kilikamatwa.
Hadi saa 11 jioni waandishi wa habari walipoondoka katika eneo hilo bado kulikuwa na ulinzi mkali.
Mnazi mmoja
Maandamano
hayo yaliyokuwa na sura mpya ya kimya kimya tofauti na
ilivyozoeleka,yalifanikiwa kupenyeza mpaka eneo la Mnazi Mmoja huku
askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiendelea kuwadadisi
wahusika wote waliokuwamo katika maandamano hayo.
Magari ya kikosi hicho yalikuwa yakizunguka katika maeneo hayo kwa lengo la kusitisha maandamano.
Maandamano
hayo yaliyokuwa na idadi kubwa ya vijana huku wakiwa wamevaa mavazi ya
kawaida hatua iliyowachanganya askari hao kufanya maamuzi ya
kuwatawanya.
Zaidi ya saa tatu, hofu ilikuwa vimetanda miongoni mwa
wakazi waliokuwa katika shughuli zao mbalimbali za kijasiriamali kuanzia
maeneo yote ya Mnazi mmja,Kariakoo na Posta.
Katika Mitaa hiyo
juhudi za askari wanaotumia usafiri wa pikipiki walifika eneo hilo na
kuwakamata zaidi ya waandamanaji 15 walikuwa mstari wa mbele huku
wengine wakitawanyika kwa njia za vichochoroni ili kutimiza lengo la
kufika kwa DPP.
Katika maeneo mengine ni pamoja na mitaa ya kituo cha Akiba baada ya askari kuvamia na kuwakamata waandamanaji hao.
Askari hao waliokuwa wametanda kila kona katika maeneo hayo ili kuhakikisha wanafanikiwa kuzuia maandamano ya wafuasi.
Mmoja kati ya waliokamatwa katika purukushani
hilo,ni mwandishi wa habari kutoka chombo kinachadaiwa kurusha
matangazo ya kiislamu (jina halikufahamika mapema) baada ya
kujichanganya katika kundi la waandamanaji hao bila kuwa na kitambulisho
chochote
Habari hii imeandikwa na Aidan Mhando, Aisha Ngoma, Pamela Chilongola, Julius Mathias ,Bakari Kiango, Kelvin Matandiko
No comments:
Post a Comment