FAMILIA nne katika Kijiji cha Ihahi, Wilaya ya
Mbarali hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuteketezwa kwa moto
na wananchi wenye hasira baada ya kuwatuhumu kufanya mauaji ya
kishirikina.
Tukio la kuteketezwa kwa nyumba hizo lilitokea
jana saa 9:00 mchana na kusababisha mali zote zilizokuwa ndani ya nyumba
hizo, ikiwamo mifugo kuteketea kwa moto.
Watu waliochomewa nyumba zao walitambulika kwa
majina ya Mohamed Mangea (48) ambapo pamoja na mkewe, Pili Hamisi
wanahisiwa na ushirikina huo, Ramadhani Mhongole na wengine
waliotambuliwa kwa jina moja moja la Mzee Mwampishi na Sekilulumo.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili
wamedai kuwa wamefikia hatua ya kuteketeza makazi ya watu hao baada ya
Serikali ya wilaya hiyo kupuuza madai yao dhidi ya watu hao walipotoa
taarifa za mauaji.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ramadhan Hassan
alisema tuhuma za kuwapo kwa mauaji ya kishirikina yaliyofanywa na watu
waliochomewa nyumba zao yamekuwapo kwa muda mrefu sasa, lakini Serikali
ngazi ya wilaya haikuzifanyia kazi ipasavyo. Alisema taarifa za awali
zilipofika Serikali, mapema mwezi uliopita, Serikali ilimtuma afisa wa
upelelezi kutoka kituo cha Polisi Chimala kwa ajili yan kushughulikia
suala hilo.
Alisema mpelelezi huyo aliendesha kura za siri kwa
ajili ya kuwabaini watu wanaojihusisha na ushirikina kijijini
hapo,ambapo wananchi walipiga kura bila matatizo.
Alisema matokeo ya kura hiyo yalionyesha
watuhumiwa waliochomewa nyumba kuwa ndio vinara wa ushirikina na Polisi
iliwakamata na kuwapeleka kituoni.
Alisema hata hivyo watuhumiwa hao walirejea
uraiani baada ya muda mfupi,hali iliyosababisha wananchi waliokuwa na
hofu ya maisha yao, kupandwa na ghadhabu na kuamua kuteketeza nyumba zao
kama njia ya kuwaondoa katika kijiji chao.
Kwa upande wake,Ramle Ibrahim ambaye ni mtoto wa
mmoja wa waathirika wa tukio la kuchomewa nyumba alisema kabla ya
kuchoma nyumba ya wazazi wake, kundi la vijana walikwenda nyumbani kwao
wakiwa wamebeba mapanga na kuanza kuwapiga wazazi wake na kuwataka
waondoke kijijini hapo na wakati wa tukio hilo wazazi wake pamoja na
wenzake walilazimika kukimbilia kituo cha polisi kwa ajili ya kunusuru
maisha yao.
Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili jana
jioni, Polisi walikwenda kijijini hapo na kukamata watu wawili, tukio
ambalo lilisababisha wananchi kuandamana kwenda kituo cha Polisi cha
Chimala ili kushinikiza wenzao kuachiwa huru. Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya,Diwani Athuman alipoulizwa kuhusiana na tukio hili alidai kuwa
yupo Dodoma kwa shughuli za kikazi na kumtaka mwandishi wa habari hii
kuwasiliana na Kaimu wake Barakael Msaki.
No comments:
Post a Comment