Wanigeria wapata somo kutoka TBS

 


UJUMBE wa wabunge, maseneta na maofisa wa Shirika la Viwango la Nigeria (SON), wameonyesha kufurahishwa na sheria ya mwaka 2009 inayoendesha Shirika la Viwango la Tanzania (TBS).


Akizungumzia Dar es Salaam jana kuhusu lengo la ujio wao, Kiongozi wa msafara huo na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Nanedu Usman alisema wamekuja kujifunza uendeshaji wa TBS kwa sababu ni moja kati ya mashirika yenye mafanikio barani Afrika.


“Tumekuja kujifunza TBS jinsi ya kusimamia viwango na tunaamini kuna mambo muhimu tutakayochota kutoka hapa, kwenda kuimarisha shirika letu,” alisema Usman na kuongeza:
“Tumechagua Tanzania baada ya kuona viwango vyake viko juu, baada ya kuangalia mashirika mengi ya viwango Afrika.”


Aliongeza kuwa Afrika inatakiwa kuungana na kupambana na uingizaji bidhaa zisizo na ubora, ili kulinda viwanda na masoko yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Son, Dk Joseph Odumodu alisema ziara yao imelenga kuimarisha ushirikiano kati ya mashirika ya viwango ya Afrika, ili kulinda viwanda na masoko ya nchi hizo.


“Afrika tunapaswa kuungana kupambana na uzalishaji na uingizaji bidhaa zisizo na ubora, ambazo kwa kiasi kikubwa zinaharibu uzalishaji wa viwanda na masoko yetu,” alisema Dk Odumodu.


Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Leandri Kinabo alisema licha ya ujumbe wa Nigeria kuja kujifunza Tanzania, shirika hilo litafaidika pia kutoka kwao.
“Wamekuja kujifunza kuhusu sheria yetu inayoendesha shirika hili. Baada ya kupirtia sheria za nchi nyingi wameona yetu imekwenda mbali kiasi cha kutotoa mwanya wa bidhaa zisizo na ubora,” alisema Kinabo na kuongeza:


“Lakini hata sisi tuna mengi ya kujifunza kutoka kwao. Nia yao ni kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika kupambana na uzalishaji na uuzaji wa bidhaa zisizo na ubora.”
Alisema Nigeria imepga hatua kubwa kwa viwango, kwa hiyo siyo wao peke yao watakaojifunza, bali hata Watanzania wana nafasi kubwa ya kupata ujuzi kutokwa kwa Wanigeria hao.Alisema nchi hizo zina ushirikiano wa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment