Vigogo bandarini wadaiwa kuiba kontena la madini

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe

Vitendo vya wizi katika Bandari ya Dar es Salaam vimeendelea kushika kasi na kuisababishia serikali kukosa mapato yake baada ya vigogo katika bandari hiyo kudaiwa kuiba kontena lenye madini aina ya Tantalite yenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 10.

Madini hayo  yanapatikana  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burudi pekee na yamekuwa yakisafirishwa kutoka katika nchi hizo kupeleka nje kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kutokana na wizi huo ambao Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameandika katika nyaraka zao kuwa una thamani ya Dola za kimarekani 22,000, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameagiza maofisa waliohusika wakamatwe. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kwa miezi minne serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka serikali ya Rwanda kuhusu kuwapo kwa mtando wa wezi wa madini hayo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dk. Mwakyembe alisema  kutokana na vitendo hivyo, juzi Balozi wa Rwanda nchini alimpigia simu kumweleza kuwapo kwa tatizo hilo ambalo limekuwa likilalamikiwa na kampuni na wafanyabiashara wanaosafirisha madini hayo kupitia bandari ya Dar es Salaam.

“Balozi wa Rwanda aliponipigia simu kunieleza kuwa mawaziri wawili kutoka Rwanda ambao ni Waziri wa Uchukuzi na Waziri wa Biashara watakuja hapa nchini kujadili suala hili ambalo tayari makampuni makubwa yameacha kupitisha madini hayo katika bandari ya Dar es Salaam,” alisema.

Alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema, alifanya ziara katika bandari hiyo akiwa na askari polisi na kukuta hujuma kubwa zimefanywa na maofisa wa taasisi za serikali.

Alisema madini hayo ambayo thamani yake ni zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 10, lakini maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wameandika katika nyaraka kuwa yana thamani ya dola 22,000.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment