Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akiongoza maandamano
WAKATI Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda tume
kuchunguza matokeo mabaya ya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012,
Chadema kimesisitiza msimamo wake kwamba kitafanya maandamano
kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na
Naibu wake, Philipo Mulugo wajiuzulu.
Mapema wiki iliyopita Pinda alitangaza kuunda tume
kuchunguza matokeo hayo, hatua ambayo Rais Jakaya Kikwete alitangaza
kuiunga mkono katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi aliyoitoa juzi.
Lakini jana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema watafanya maandamano makubwa aliyoyaita ya kihistoria, katika
mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam ili kushinikiza
kutekelezwa kwa hatua hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika
Viwanja vya Shule ya Sekondari Mtatatila, Sumbawanga mkoani Rukwa, Mbowe
alisema: “Lengo la maandamano ni kuwataka waziri wa elimu na naibu wake
wajiuzulu kwani wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na
kusababisha watoto wa maskini kufanya vibaya kwenye mitihani yao.”
Alisema maandamano hayo yatahusisha wafanyakazi wa
Serikali, mama lishe na wafanyabiashara wa usafirishaji wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari... “Siku hiyo hakutakuwa na masomo wala
kazi, kila kitu kitasitishwa.”
Mbowe alisema maandamano hayo yatakuwa ya
kihistoria na kwamba Chadema kinataka kuwafungua macho wananchi walio na
kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kusomesha watoto wao nje ya nchi
ili washinikize Dk Kawambwa na Mulugo waachie ngazi.
“Tunataka shule za sekondari na msingi zisigeuzwe
kuwa vituo vya kulelea watoto, bali vifanye kazi za kutoa elimu, kama
ilivyokusudiwa,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe aliwataka wananchi kuwa makini
na uchochezi unaofanywa na baadhi ya vyama vya siasa, badala yake
waangalie chama chenye sera, mtazamo na harakati za kuleta mabadiliko
yatakayokuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
“Njia sahihi ni kuhakikisha mnajiondoa, kwani ili
muweze kujua mustakabali wa maisha yenu ni lazima mhakikishe mnakuwa
makini kufanya uamuzi ulio sahihi kwa viongozi mnaowataka, ”alisema
Mbowe.
Hii ni mara ya pili katika mwaka huu kwa Chadema
kutaka viongozi wajiuzulu. Mwezi uliopita, chama hicho kilimtaka Spika
wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai wajiuzulu kwa maelezo
kuwa wamekuwa wakiminya demokrasia, kuubana upinzani na kupendelea chama
tawala (CCM) bungeni.
No comments:
Post a Comment