Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa ameanza kuisakama
Idara ya Usalama wa Taifa kuwa wanatumia mbinu mbalimbali kuwahujumu na
kwamba mbinu zinazofanywa na idara hiyo ni kueneza propaganda walizodai
za uongo dhidi yao.
Akizungumza jana makao makuu cha chama hicho
jijini Dar es Salaam, Dk Slaa alisema: “Tumezibaini mbinu zinazofanywa
na Usalama wa Taifa kwa kutumiwa na CCM kueneza propaganda za uongo
dhidi yao kwa lengo la kukichafua chama, lakini haziwezi kufanikiwa
kwani tayari tumegundua mbinu zao.”
“Chadema ni chama makini na hakiwezi
kuyumbishwa na mtu yoyote wala idara yoyote inayotumiwa na baadhi ya
watu ili kutaka kukizohofisha,” alisema Dk Slaa ambaye mara kwa mara
amekuwa akilalamika kuchezewa rafu.
Hata hivyo, viongozi wanaohusika na idara hiyo
akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika
walipotafutwa na gazeti hili kwa nyakati tofauti ili kuzungumzia tuhuma
hizo za Dk Slaa, hawakuwa tayari kuzizungumzia.
Waziri Mkuchika alisema asingeweza kuzungumzia
tuhuma hizi kwa kuwa hakuwa amezisikia wala hafahamu ni ujumbe upi
uliomo katika kauli ya Dk Slaa.
“Mimi nimeshinda kwenye Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala tangu asubuhi na sasa ndiyo natoka, kwa hiyo
sijasikia hiyo kauli wala huo mkutano wa (Dk Slaa). Kwa hiyo siwezi
kujibu chochote kwa sasa,” alisema Mkuchika na kuongeza:
“Nadhani tumeelewana na pengine tusubiri pindi
nitakapofahamu ni kipi amekizungumza na nikafanyia uchunguzi tutaona
kama kuna cha kujibu basi tutajibu wakati huo, lakini kwa sasa siwezi
kusema chochote.”
Mapema gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa
Usalama wa Taifa, Rashid Othman ili kuzungumzia madai hayo ya Chadema
lakini mara zote simu yake ilikuwa haipatikani.
Baadaye Mwananchi iliwasiliana na Naibu
Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jacky Nzoka ambaye alijibu kwa kifupi na
kukata simu: “Mimi siyo msemaji tafadhali.”
Hata hivyo, katika tuhuma hizo Dk Slaa alisema
mifano hai ipo kwake kwani kila wakati amekuwa akizungukwa na watu wa
idara hiyo kwa malengo yao binafsi, lakini malengo yao hayawezi
kufanikiwa kwani wao wapo makini katika hilo.
“Mimi kila wakati Usalama wa Taifa wamekuwa
wakinizunguka zunguka kwa mambo yao binafsi wanayoyafuatilia kwangu,
lakini nataka niwaambie kwamba nimewagundua na mbinu zao haziwezi
kufanikiwa ila nawataka wasichoke kunifutalia na waendelee tu,” alisema.
Chadema na Sh400 milioni
Dk
Slaa alikiwakilisha Chadema kusaini mkataba wa ushirikiano na Chama cha
Konservative cha Denmark ili kuinua uwezo wa vijana na wanawake
kisiasa.
Chama hicho kimeahidiwa kupewa Sh400 milioni
kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kujiimarisha kisiasa kwa Baraza la Vijana
la chama hicho (Bavicha) na lile la Wanawake (Bawacha).
“Sisi leo tunasaini mkataba huu, lakini hatuufanyi siri kama
vyama vingine vinavyofanya kwani mkataba huu upo wazi na kwamba kila mtu
atakayetaka kuona atapewa,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yatatolewa kwa watu 900
wa Bavicha na 900 wengine kutoka Bawacha na yanatarajia kuanza siku
chache zijazo hadi Desemba mwaka huu yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo
wa kisiasa vijana wa Chadema na wanawake ili kuhakikisha wanaimarika
kisiasa Tanzania,” alisema Dk Slaa.
Akizunguza wakati wa kusaini mkataba huo,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Conservative, Rolf
Aagaard-Svendsen alisema lengo la ushirikino wao ni kuwajengea uwezo wa
kisiasa vijana ili washiriki vizuri katika medani za kisiasa.
No comments:
Post a Comment