Mahakama ya Afrika inayoshughulikia haki za
binadamu yenye makao yake jijini Arusha imeamuru Serikali ya Libya
kuendesha kesi inayomkabili mtoto wa kiongozi wa zamani wa Libya,
Muammar Gadaffi kwa uhuru na haki.
Saif al-Islam Gaddafi, ambaye ni mtoto wa pili wa
Gadaffi amekuwa akishikiliwa na vyombo vya usalama vya Libya tangu
Novemba 19, 2011 baada ya kukamatwa wakati akijaribu kukimbia nchi hiyo
baada ya kuuawa kwa baba yake na kaka yake, Mtassim Gaddafi, Oktoba 20,
2011.
Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika yenye makao
makuu mjini Addis Ababa, Ethiopia ndiyo iliyowasilisha shauri hilo
kwenye Mahakama ya Afrika kwa kuwa Serikali ya Libya haijaridhia
mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Kutokana na hali hiyo, hata familia ya Gadaffi
ilishindwa kufungua kesi hiyo kwani taasisi au watu binafsi wa Libya
hawana uwezo wa kisheria wa kufungua kesi kwenye mahakama hiyo kutokana
na kikwazo cha Serikali yao.
Shauri hilo lenye namba 002/2012 lilisikilizwa na
majaji kumi na moja walioongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Sophia
Akuffo kutoka Ghana, Ijumaa iliyopita.
Wengine waliokuwemo kwenye jopo hilo ni pamoja na
Makamu wake, Jaji Fatsah Ouguergouz, Jaji Mkuu wa zamani, Augustine
Ramadhan pamoja na Majaji Sylvain Ore, Duncan Tambala, Gerald Niyugeko,
Bernard Ngoepe, Elsie Thompson, Hadji Guisse, Kimelabalou Aba na Ben
Kioko.
Jopo hilo la majaji pia limeiamuru Serikali ya
Libya kuruhusu ndugu, jamaa na marafiki wa mtuhumiwa huyo kumtembelea
kipindi chote shauri dhidi yake linaposikilizwa.
Serikali ya Libya imetakiwa kutoa taarifa
mahakamani kuhusu utekelezaji wa amri hiyo siku 15 tangu kupokelewa kwa
nakala ya hukumu.
Familia ya Gadaffi imekuwa haifurahishwi na mwenendo wa kesi ya Saif huko Libya.
No comments:
Post a Comment