Maombi ya Lwakatare yapangiwa jaji

 
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare akifunguliwa pingu alipofikishwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini  Dar es Salaam hivi karibuni.

Dar es Salaam. Maombi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare kupinga utaratibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumfutia mashtaka kisha kumkamata na kumfungulia tena mengine, tayari yamepangiwa jaji wa kuyasikiliza.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Lwakatare, zinadai maombi hayo yamepangwa kusikilizwa na Jaji Lawrence Kaduri. Hata hivyo, tarehe ya kusikilizwa kwa maombi hayo haijapangwa.


Lwakatare anayekabiliwa na kesi ya ugaidi na mwenzake Ludovick Joseph, kupitia kwa jopo la mawakili wanaomtetea, wiki iliyopita aliwasilisha maombi Mahakama Kuu Dar es Salaam akipinga uamuzi wa DPP kuwafutia mashtaka kisha kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka hayo.


Siku hiyohihyo alipowasilisha maombi hayo, Mahakama Kuu ilitoa hati ya kuita majalada yanayohusiana na kesi yao, ikiiamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iwasilishe majalada hayo mahakamani hapo.


Majalada hayo namba 37 na namba 6 yote ya mwaka 2013, yalishawasilishwa Mahakama Kuu, kwa awamu mbili. Jalada la kwanza, namba 37 liliwasilishwa Mahakama Kuu Jumatatu na jalada la pili namba 6 liliwasilishwa Jumanne, wiki hii.


Katika maombi yake Mahakama Kuu yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura, yakiambatanishwa na hati ya kiapo cha Wakili Peter Kibatala, Lwakatare anaomba mahakama hiyo iitishe majalada hayo na ifanye marejeo ya mwenendo wa kesi katika Mahakama ya Kisutu.


Kwa mujibu wa maombi hayo ya marejeo namba 14 ya mwaka 2013, lengo la kuiomba mahakama hiyo iitishe majalada hayo ni kufanya uchunguzi ili kujiridhisha yenyewe kuhusu usahihi na uhalali wa mwenendo wake.
Pia, wanaomba Mahakama Kuu ifanye marejeo na/au kutengua hati ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuwafutia mashtaka watoa maombi (Nolle Prosequi), kabla ya kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka hayohayo.


Sambamba na hayo, wanaomba Mahakama Kuu iamuru Mahakama ya Kisutu itoe uamuzi wa maombi ya dhamana, uliokuwa umepanga kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emillius Mchauru, Machi 20, mwaka huu katika kesi namba 37.


Maombi mengine ni kurejea, au kutengua mwenendo wa kesi katika kesi namba 6 iliyofunguliwa baada ya hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi hao, badala yake mwenendo wa kesi katika kesi namba 37 uendelee.


Pia, wanaomba Mahakama Kuu iamue kwamba utaratibu uliotumiwa na wajibu maombi (Jamhuri) kutoa hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi katika kesi namba 37, ilikuwa kinyume cha sheria na/au haukuwa sahihi.


Lwakatare na mwenzake, Joseph, wanakabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manne ya kula njama na kufanya mipango ya kumteka, kisha kumdhuru kwa sumu Dennis Msacky.


Walikamatwa Machi 13, mwaka huu na kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Jumatatu, Oktoba 18, ambako walisomewa mashtaka hayo, ambayo waliyakana, baada ya kuulizwa kama wanayakubali au la.

No comments:

Post a Comment