Nicolaus Mgaya
Dar es Salaam: Siku chache baada ya Mwenyekiti
wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Ayoub Omar kuvuliwa
wadhifa wake, imebainika kuwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Nicolaus
Mgaya naye amenusurika kung’olewa kwenye wadhifa wake.
Mgaya aliliambia Mwananchi jana kuwa njama za
kumng’oa kwenye wadhifa huo zilipangwa na wapinzani wake ambao walitoa
hoja dhaifu bila ushahidi kuwa ana uhusiano wa wanawake (hawakutajwa).
“Hoja zao hazikuwa na maana, walikuwa wakihisi
tu kuwa natembea na mwanamke fulani bila kuwa na ushahidi, pia suala
hilo halihusiani na utendaji wangu wa kazi,” alisema Mgaya na kuongeza:
“Unajua katika umoja wowote lazima kuwe na
majungu watu wanaweza kuwa na sababu zao nyingi tu, hivyo sikuona ajabu
niliposikia nafanyiwa zengwe.”
Alisema hoja za kutakiwa kung’oka
zilijadiliwa na kumalizwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji
kilichomalizika juzi, ndiyo maana hazikuibuka tena katika kikao cha
Baraza Kuu la Tucta kilichomalizika jana jioni.
“Ripoti ya kikao cha utendaji ndiyo huletwa
katika kikao cha baraza kuu na kwa kuwa suala hilo halikuwa na ushahidi
lilikwisha hukohuko,” alisema Mgaya.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani
ya kikao cha Baraza Kuu la Tucta kilichomalizika jana jioni zilisema
kuwa baadhi ya wajumbe waliibua hoja kwamba Mgaya ameshatimiza miaka 61,
hivyo anatakiwa kustaafu kwa mujibu wa sheria.
“Baadhi ya wajumbe waliibua hoja hiyo lakini
haikuwa na nguvu, ila pamoja na hayo jambo hili lazima litakuja kumbana
Mgaya baadaye,” zilieleza taarifa hizo.
Ayoub alivuliwa wadhifa wake
juzi kwa mujibu wa Katiba ya Tucta kifungu cha 16.6.8 kinachoeleza kuwa
kiongozi wa shirikisho hilo atakoma
kuendelea kushikilia ofisi ikiwa atastaafu kwa mujibu wa sheria.
Mgaya alisema pamoja na Ayoub kuwa na kazi
mpya baada ya kustaafu lakini alipoteza sifa ya kuendelea kuwa
Mwenyekiti kwa kuwa katiba inaeleza kwamba kiongozi lazima awe mwajiriwa
katika sekta ya umma au ile binafsi.
Mgaya alisema kwa sasa nafasi ya Omari
inakaimiwa na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Notibuga Masikini na
kwamba ataendelea na wadhifa huo kwa miezi 12.
“Mwakani tutakuwa na
mkutano mkuu wa kazi ambapo pamoja na mambo mengine tutapata nafasi ya
kuchagua mwenyekiti mpya, Katiba ipo wazi kama siyo mwajiriwa huwezi
kuendelea na wadhifa wowote,” alisema Mgaya.
Katika maelezo yake, Ayoub alisema kuwa
viongozi wenzake walikuja na hoja kwamba hakuwa na kazi kwani alikuwa
amestaafu katika kiwanda cha Mbolea Mbeya, lakini alisisitiza kuwa baada
ya kustaafu alipata kazi sehemu nyingine.
Wakati hayo yakitokea, habari nyingine
zinasema wajumbe wa Baraza Kuu la Tucta kutoka mikoa ya Mbeya, Arusha na
Dodoma walihoji mapato na matumizi ya Tucta, huku wakitaka kujua kiasi
cha fedha kilichopatikana kutokana na kodi ya majengo ya shirikisho
hilo.
No comments:
Post a Comment