Abiria wakigombania kuingia katika daladala.
Dar es Salaam. Mamlaka ya
Udhibiti wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imepandisha nauli za
daladala, mabasi ya kwenda mikoani, usafiri wa reli na tozo za majini
kuanzia Aprili 12, mwaka huu.Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Ahmad
Kilima alisema jana kuwa nauli za daladala zimeongezeka kwa asilimia
24.46 kwa kuzingatia maoni ya wadau na gharama za uendeshaji.
Kwa upande wa usafiri wa daladala nauli
zimepanda kwa umbali tofauti kutoka Sh300 hadi 400, Sh350 hadi 450,
Sh500 hadi 600, Sh650 – 750 na kwa wanafunzi kutoka Sh150 hadi 200
katika sehemu yoyote watakayokwenda.
Nauli za usafiri wa mabasi makubwa ya masafa
marefu nauli hizo zimeongezeka kwa viwango tofauti. Mathalan kwa basi la
kawaida kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ni Sh30,700, njia ya vumbi
kutoka Kigoma hadi Sumbawanga Sh25,400 na basi la hadhi ya kati (Semi
Luxury) kati ya Dar na Mwanza ni Sh61,400, wakati basi la hadhi ya juu
(Luxury) kati ya Dar na Arusha ni Sh 36,000.
Kilima alisema: “Kuanzia Aprili 12 mwaka huu,
kati ya kilometa 0 hadi 10, nauli ya daladala itakuwa Sh400 badala ya
Sh300 zinazolipwa hivi sasa.
“Pia nauli za mabasi ya kwenda mikoani
zimeongezeka kwa asilimia 20.3 kwa mabasi ya kawaida, mabasi ya kati kwa
asilimia 16.9 na mabasi ya daraja la juu kwa asilimia 13.2,” alisema.
Kilima alisema nauli za mabasi ya mikoani
zimepanda kutoka Sh30.67 hadi Sh36.89 kwa kilometa kwa mabasi ya daraja
la kawaida katika njia za lami.
Kwa upande wa mabasi ya kawaida kwa
njia ya vumbi imepanda kutoka Sh37.72 hadi Sh 46.11 kwa kilometa na
kwamba mabasi ya hadhi ya kati, nauli zimepanda kutoka Sh45.53 hadi Sh
53.22 kwa kilometa.
Alisema mabasi ya hadhi ya juu nauli zimepanda kutoka Sh51.64 hadi Sh58.47 kwa kilometa.
“Kupanda
kwa nauli kunatakiwa kwenda sambamba na huduma bora na kwamba Sumatra
imepiga marufuku kutumia wapigadebe kuuza tiketi za safari”alisema.
Usafiri wa Reli
Katika
uamuzi huo, usafiri wa reli pia umepanda ambapo daraja la kwanza Dar es
Salaam hadi Morogoro, nauli mpya na ya zamani katika mabano ni
Sh21,100, (Sh16,852), Dar hadi Dodoma Sh34,700, (Sh27,788), Dar es
Salaam-Tabora Sh54,800, (Sh43,859).
Dar es Salaam-Isaka Sh62,100,
(Sh49,662), Dar- Shinyanga Sh65,300 (Sh52,229) Dar –Mwanza Sh74,800 (Sh
59,818), Dar- Kigoma Sh75,700, (Sh60,599)
Daraja la pili, Dar es Salaam-Morogoro
Sh16,600, (Sh13,280), Dar es Salaam-Dodoma Sh26,400 (Sh 21,092), Dar es
Salaam-Tabora Sh40,500 (Sh 32,364), Dar es Salaam-Isaka Sh45,800,
(Sh36,605), Dar es Salaam-Shinyanga Sh48,000 (Sh38,390), Dar es Salaam-
Mwanza Sh54,700 (Sh43,747), Dar es Salaam-Kigoma Sh55,400 (Sh44,305).
Daraja la tatu, dar es Salaam-Morogoro Sh8,800
(Sh6,138), Dar es Salaam-Dodoma Sh13,500 (Sh9,374), Dar es
Salaam-Tabora 20,400 (Sh14,173), Dar es Salaam-Isaka Sh22,800
(Sh15,847), Dar es Salaam –Shinyanga Sh24,000 (Sh16,628), Dar es
Salaam-Mwanza Sh27,200 (Sh18,860), Dar es Salaam- Kigoma Sh27,500
(Sh19,084).
Akizungumzia tozo za majini, Kaimu Mkurugenzi
huyo alisema mamlaka hiyo imeridhia ongezeko la tozo la asilimia 34.3
kwa vyombo vinavyotumia bandari za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA).
Alisema awali TPA walipendekeza tozo hizo
kuongezeka kati ya asilimia saba hadi 400 kulingana na aina ya huduma
zinazotolewa kwa meli zinazotumia bandari za mamlaka hiyo.
No comments:
Post a Comment