Moshi mweupe wafuka, Papa mpya apatikana
Kardinali Jorge Bergoglio wa
Argentina amechaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki Duniani, akiwa ni wa
kwanza kutoka barani Amerika na wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi
ya miaka 1,000.
Baada ya kuchaguliwa na makardinali wenzake 115, Kardinali Jorge Bergoglio (76) alichagua kufahamika kwa jina la Francis I.
Maelfu ya mahujaji, watalii na waumini wa Kanisa
Katoliki waliokuwa wamejazana katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu
Petro, Vatican kushuhudia moshi mweupe uliofuka saa 4:00 usiku kwa saa
za Afrika Mashariki kuashiria kuchaguliwa kwake, waliripuka kwa shangwe,
nderemo na vifijo.
Muda mfupi baada ya moshi huo kutoka, kardinali
mmoja alisimama katika ‘varanda’ ya Kanisa la Mtakatifu Petro na
kutangaza “Habemus Papum” (tumepata papa mpya).
Papa Francis I
alikuwa miongoni mwa waliokuwa wanawania nafasi hiyo na papa
anayeondoka, Benedict XVI mwaka 2005, ambapo aliripotiwa kuibuka wa
pili.
Kabla ya kuchaguliwa kwake, Papa Francis I ambaye
kwa wadhifa wake pia anakwenda kuwa Askofu wa Roma, alikuwa Askofu Mkuu
wa Jimbo la Buenos Aires, Argentine na kwa muda wote wa utumishi wa
utumishi alikuwa huko huko nyumbani.
Anakuwa Papa wa 266 kuwahi kuongoza kanisa hilo lenye waumini zaidi ya bilioni 1.2 duniani.
Baada ya kutangazwa kwake, Papa Francis I alijitokeza kuzungumza kwa mara ya kwanza kama Askofu wa Roma.
Akiwa amechaguliwa katika awamu ya tano ya upigaji
kura, inaelezwa kuwa alikuwa miongoni mwa mapapa waliochaguliwa kwa
haraka baada ya muda mrefu, akiwa sawa na Benedict XVI (2005) na Pius
XII aliyechaguliwa mwaka 1939.
Mshindi alitakiwa kupata kuta 77 au robo tatu ya makardinali 115 walioshiriki uchaguzi huo.
Papa
Francis I anachukua nafasi iliyoachwa na Papa Benedict XVI aliyejiuzulu
Februari 28, mwaka huu, ikiwa ni miaka 600 tangu Papa wa mwisho
kujiuzulu.
Yeye ni nani
Papa Francis I, ni Papa wa kwanza kutoka Shirika la Jesuit ambaye ametumia muda wake mwingi wa utumishi nyumbani Argentina.
Anafahamika kwa utumishi uliotukuka kwa uangalizi
wa kanisa na mapadri, mambo ambayo yanatajwa kuwa sifa kubwa ya
kuchaguliwa kuwa Papa.
Papa huyo amedumu katika maisha ya kufundisha na
kuongoza mapadri. Amefanya kazi Amerika ya Kusini ambako kuna Wakatoliki
wengi. Kardinali Bergoglio anatambulika kwa kutamadunisha Kanisa la
Argentina, lililokuwa miongoni mwa makanisa ya kihafidhina huko Amerika
Kusini.
Amechagua jina la Papa Francis I, chini ya uangalizi wa Mtakatifu Francis wa Assisi.
Alizaliwa Buenos Aires katika familia ya mfanyakazi wa reli. Alipata upadrisho mwaka 1969.
Aprili
15, 2005, mwanasheria wa haki za binadamu alimfungulia mashtaka ya
jinai kwa kushirikiana na maofisa wa jeshi kuwateka mapadri wawili wa
Jesuit mwaka 1976, akiwa kiongozi wao aliwafukuza katika utumishi
kutokana na migogoro katika jumuiya hiyo.
Msemaji wake alikanusha vikali tuhuma hizo na hakuna uthibitisho uliotolewa kumhusisha na madai hayo.
Kauli yake ya kwanza
Baada ya kutangazwa kuwa Papa wa 266, Kardinali Jorge Bergoglio (76) aliwataka waumini wa Kanisa Katoliki duniani kumwombea.
Papa huyo aliyechagua jina la Francis I, alisema:
“Kama mnavyofahamu, kazi ya mkutano wa uchaguzi ilikuwa ni kuchagua
Askofu wa Roma,” Francis I aliueleza umati uliokuwa unashangilia katika
Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro, huku akiwapungia mikono.
“Ni mimi hapa. Ninadhani makardinali wenzangu wamenichagua mimi kutoka mbali...Niko hapa. Ninapenda kuwashukuru kwa kunipokea.”
Akiwa kardinali alipambana na Serikali ya
Argentina chini ya Rais Cristina Fernandez de Kirchner kuhusu msimamo
wake dhidi ya ndoa za mashoga na utoaji bure wa huduma za uzazi wa
mpango, ambazo zimekuwa zikipingwa na Kanisa Katoliki duniani kote.
No comments:
Post a Comment