China
Dar es Salaam. Mwanafunzi wa
Kitanzania aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Huazhong
nchini China, Leonard Peter Tambalu amefariki dunia ghafla katika
mazingira ya kutatanisha wakati akiwa anajiandaa kurejea nchini.
Tambalu aliyekuwa mwaka wa pili katika chuo hicho
kilichopo kwenye mji wa Wuhan, alifikwa na mauti hayo Machi 17 mwaka huu
wakati akiwa katika Uwanja wa Ndege mjini Beijing. Marehemu alikuwa
Ofisa Kilimo Mwandamizi kutoka wilayani Iramba mkoani Singida.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Christina Midelo
hakukubali wala kukanusha kuwapo kwa tukio hilo. “Sina taarifa za kifo
cha kijana huyo, wanaoweza kuzungumza ni Ubalozi wa China kwa kuwa ndio
waliokuwa wakimsomesha.”
Balozi wa Tanzania nchini China, Philip Marmo,
ambaye yupo nchini kutokana na ushiriki wake katika mapokezi ya Rais wa
China, Xi Jinping, alikiri kufahamu suala hilo. Katibu wa Umoja wa
Wanafunzi wanaosoma vyuo mbalimbali katika mji wa Wuhan (Wtasa),
Humphrey Sikauki, alithibitisha kifo cha Tambalu na kwamba mwili wake
ulikuwa unafanyiwa uchunguzi na maofisa wa serikali ya China
wakishirikiana na wale wa Tanzania.
“Tangu alipofariki madaktari walisema ripoti
ingetolewa baada ya siku saba ambazo ziliisha Jumatatu, mpaka sasa hiyo
ripoti hatujaipata lakini Mwambata wa Elimu katika Ubalozi wa Tanzania
nadhani atakuwa ameipata kwa sababu ndiye alikuwa akiiwakilisha Tanzania
katika uchunguzi huo,” alisema Sikauki.
Gazeti hili lilijaribu mara kadhaa kuwasiliana na
Mwambata wa Elimu katika Ubalozi wa Tanzania nchini China, George
Manongi lakini mawasiliano yalikuwa magumu, kutokana kushindwa
kusikilizana.
Kifo cha Tambalu
Tambulu
ambaye alifika China Septemba 2011 kwa ajili ya masomo yake ya fani ya
Kilimo, alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Chinese -Japanese
Friendship.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, baada ya kufika
Uwanja wa Ndege wa Beijing alianguka, kabla ya kupelekwa hospitalini,
ambako ilibainika kwamba alikuwa amekwishafariki.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa, uongozi wa hospitali
ulitoa siku saba za uchunguzi kabla ya kutoa mwili wa marehemu, lakini
tatizo kubwa limekuwa ni uwezo wa kuusafirisha mwili huo.
Habari zinasema Wizara ya Kilimo haiwezi kuwajibika moja kwa moja kuusafirisha mwili wa marehemu isipokuwa halmashauri yake.
Marmo kwa upande wake alisema ni vigumu kwa
Serikali kusafirisha mwili huo kwani haina bajeti ya masuala hayo na
kwamba yeye atachangia kama Watanzania wengine.
Habari zaidi zinasema
Serikali ya China imekataa kumsafirisha marehemu kutokana na kifo hicho
kutokuwa cha kawaida (natural death).
“Manongi aliwaambia ndugu wa marehemu Tanzania
kuwa kampuni aliyowasiliana nayo inaweza kusafirisha mwili huo kwa Dola
za Marekani 40,000 au 45,000,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kinapasha pia kuwa, Mwambata huyo
aliwasiliana na mwajiri wa marehemu (Wizara ya Kilimo) kuhusu
kumsafirisha na mwajiri akakataa kwa sababu marehemu alikuwa mikononi
mwa Serikali ya China.
“Alitaka ndugu wawajibike kuusafirisha mwili hadi nyumbani kwao Shinyanga kwa mazishi,”kilisema.
Chanzo hicho kinaeleza kuwa, Mwambata pia
aliwaeleza ndugu kuwa chuo alichokuwa akisoma kilisema hakiwezi
kuusafirisha mwili kutokana na ukubwa wa gharama lakini kinaweza
kuuchoma na kusafirisha majivu.
Gazeti hili liliwasiliana na Mwambata huyo, lakini
alipokuwa akipokea simu yake na mwandishi anamsikia lakini kwa upande
wake alikuwa hasikii hivyo kuitika tu “haloo, haloo…”
Alipotumia ujumbe mfupi wa maneno, alijibu kuwa simu yake imeshindwa kuutambua ujumbe huo kwani maandishi yalikuwa hayasomeki.
No comments:
Post a Comment