Waandishi Wetu,
Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda ametekwa na watu wasiofahamika
na kisha kumjeruhi vibaya kwa nondo, mapanga na kisha kumng’oa meno,
kucha na kumharibu jicho la kushoto.
Tukio hilo la kinyama linafanana kwa kiasi
fulani na lile la alilofanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari
Tanzania, Stephen Ulimboka.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi
usiku wakati Kibanda akirejea nyumbani kwake Goba Punguni, Kata ya Mbezi
Juu, kutoka kazini.
Tayari mwandishi huyo mkongwe wa habari,
amesafirishwa jana kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Aliondoka
jana akisindikizwa na daktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimu (Moi).
Mkasa wenyewe
Akizungumza kwa tabu
alipokuwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu
(ICU), hospitalini Moi, Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New
Habari (2006), alisema:
“Nilifika nyumbani kwangu kama saa sita usiku
nikitokea kazini na nilipofika kwenye lango la kuingia ndani nilipiga
honi ili mlinzi anifungulie. Lakini ghafla nilivamiwa na kundi la watu
ambao walivunja kioo cha gari langu upande niliokuwa nimekaa. Nilitokea
kupitia mlango wa abiria lakini sikuweza kuwakimbia watu wale kwani
walinikamata na kuanza kunishambulia kwa vitu vizito.”
“Baada ya kutoka kwenye gari, nahisi
nilikanyaga sehemu mbaya, nikateleza na kuanguka wakanifuata...niliona
kama watu watatu hivi wakaanza kunishambulia. Sikuwa nafahamu
kilichojiri, lakini nilisikia mwingine akimwambia mwenzake afande
‘mshuti... mshuti’ huyo alipoelekeza mtutu na kujaribu ‘kushuti’ (kupiga
risasi) ilikuwa kama vile imegoma.
“Nikiwa bado niko chini, wakanipiga kwa kitu
cha ncha kali kwenye jicho la kushoto, wakaning’oa meno na kucha katika
vidole vya mkono wa kulia, walinipiga sana na nilipata maumivu makali.
Baada ya kunipiga na kunijeruhi waliniburuza hadi bembeni ya nyumba
yangu na kunitupa na wakaondoka, baadaye majirani na wasamaria wema
walikuja kuniokoa.
Mashuhuda baada ya tukio
Akizungumza jana,
mzazi mwenzake, Angella Semaya alisema wakati Kibanda alipovamiwa
hakusikia lolote: “Niliamshwa na kelele za majirani ndipo nami nikaenda
eneo la tukio. Sikuamini kama alikuwa Kibanda kwani alikuwa ametapakaa
damu huku akigugumia maumivu makali... kwanza sikumjua kama ni yeye kwa
jinsi alivyokuwa.”
“Nina wasiwasi na hawa watu kuwa wametumwa kwa
kuwa hawakuchukua chochote zaidi ya kumdhuru mwili,” alisema. Angella
aliondoka jana na Kibanda pamoja na Mwandishi wa Habari, Eric Kabendera
ili kumsindikiza Afrika Kusini atakapokuwa anapata matibabu.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari
(2006), Hussein Bashe alisema: “Tulikuwa na Kibanda hadi usiku kama 5:30
hivi, tukifuatilia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya na tulipoona
hakuna kinachoendelea zaidi, tukaagana kurudi makwetu.”
“Kwa kweli taarifa za kuvamiwa na kushambuliwa
kwake zimetushtua, kwani ameumizwa sana hasa jicho. Daktari alishauri
jicho liondolewe lakini nilikataa, jopo la madaktari bingwa wa macho
wamemtazama na kuthibitisha kweli limeumia sana, tumewasiliana na
mwajiri wetu ameamua kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
“Nawashukuru madaktari kwa jinsi walivyompokea
na kumshughulikia katika kiwango kinachotia moyo. Pia waandishi kwa
umoja waliouonyesha kwa kujitokeza haraka na kumjulia hali.”
Tasnia ya habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeelezea kushtushwa na tukio la kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa mwenyekiti wake.
Taarifa ya TEF iliyotolewa jana na Katibu
wake, Neville Meena, imesema shambulio hilo ni uthibitisho kwamba
mazingira ya kikazi ya waandishi wa habari Tanzania siyo salama tena...
“Tunapaswa kuchukua hatua za kutathmini upya mazingira ya kazi zetu, ili
kuhakikisha kwamba walau tunakuwa salama.”
Alisema mwendelezo wa vitendo vya
kuwashambulia waandishi wa habari ambavyo katika siku za karibuni
vimeibuka, vinalifanya jukwaa liamini kwamba wanahabari sasa wanatishwa
ili wasiweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Utesaji huu aliofanyiwa Kibanda unafanana na
ule aliofanyiwa Dk Ulimboka. (Rejea vitendo vya kupigwa kichwani,
kung’olewa kucha na meno).
Aidha, Meena alisema: “Tunaamini kwamba
yaliyomkuta Kibanda hayawezi kutenganishwa na msimamo wake kikazi au
kama mtu binafsi. Tunasema hivyo tukizingatia kwamba wahusika
hawakuchukua chochote liwe, gari au vitu vilivyokuwamo ndani ya gari
hilo vikiwamo laptop, ipad, simu za mkononi na vinginevyo.”
"Tunaamini vyombo vya dola, vitachunguza na
kuwatia mbaroni kisha kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa tukio
hili na mengine kadhaa ambayo sasa yamegeuka kuwa sehemu ya utamaduni
katika nchi yetu.”
Awali, Mjumbe wa Bodi ya TEF, Theophil Makunga
alisema wakati huu wanahabari na wanafamilia wakisubiri uchunguzi juu
ya tukio hilo, kitendo hicho hakina budi kulaaniwa.
“Hatuwezi kusema
nini chanzo cha tukio hilo kwa sasa, lakini tunaamini limetokana na kazi
yake. Tunalaani vikali kwani tunaweza kusema kazi yetu sasa si salama
tena,” alisema Makunga.
Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Jesse Kwayu
alisema tukio hilo halina uhusiano na ujambazi kutokana na mazingira ya
jinsi lilivyotokea na kutaka hatua za haraka za kisheria zichukuliwe
dhidi ya wahusika.
Mhariri wa Habari wa Tanzania Daima, Edson
Kamukara alisema: “Matukio ya kutekwa na kushambuliwa kwa waandishi wa
habari yamekuwa yakishika kasi... ni jambo la kusikitisha na hatuwezi
kukaa kimya kwa hili.”
Baada ya tukio
Katika taarifa yake jana, Dk
Nchimbi alisema Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema ameteua
timu ya maofisa wa polisi wanne kutoka Makao Makuu ya Upelelezi kuungana
na wapelelezi kutoka Kanda Maalumu ya Polisi Mkoa wa Kinondoni ili
kuhakikisha waliohusika wanakamatwa.
Baadaye jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema ofisi yake imeunda jopo la
maofisa wa polisi tisa ambao wameshaanza kazi ya upelelezi wa tukio
hilo.
Kova alisema kitendo alichofanyiwa Kibanda si
cha kihalifu, bali kukomoana na visasi kwa kuwa upelelezi wa awali
umeonyesha kuwa waliomvamia hawakuchukua chochote.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(Maelezo), Assah Mwambene alisema Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo kupitia idara yake imepokea kwa mshtuko tukio la kupigwa na
kutendewa ukatili.
Alisema kitendo kilichofanywa kwa mhariri huyo ni ukatili uliopitiliza na kwamba wanaliachia Jeshi la Polisi lifanye kazi yake.
Wamjulia hali
Kabla ya Kibanda kupelekwa
Afrika Kusini, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk
Gharib Bilal walifika kumjulia hali. Wengine ni Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene na Yussuf Omar
Chunda na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT),
Dk Reginald Mengi.
Mengi na Mbowe
Akizungumza tukio hilo, Dk
Mengi mbali ya kulaani, aliwataka waandishi wa habari kuandika ukweli na
kuhakikisha haki inapatikana kwa kuwa jambo hilo ni zito.
Alisema
kuna haja ya polisi kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli halisi
upatikane na wahusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Mbowe alisema: “Tuungane katika kutetea uhuru
wa vyombo vya habari. Uvamizi wa Kibanda ni doa kubwa katika tasnia ya
habari bila kujali yuko chombo gani na yeye ndiye mkuu wa Jukwaa la
Wahariri, ni wazi atakuwa amezungukwa na maadui wengi.”
Imeandikwa na Joyce Mmasi, Aidan Mhando, Bakari Kiango, Salhim Shao, Beatrice Moses na Aziza Masoud.
No comments:
Post a Comment