Somalia yaondolewa marufuku ya silaha

Baadhi ya silaha haramu zilizonaswa na wanajeshi wanaoshika doria Somalia

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, limepiga kura kuiondolea Somalia kwa muda marufuku ya uuzaji wa silaha nchini Somalia kwa mwaka mmoja.

Marufuku hiyo, ni moja ya marufuku iliyowekwa zamani sana mwaka 1992, na itaweza kuondolewa kwa muda kama hatua ya kuisaidia serikali mpya ya Somalia.

Nchi kadhaa zilikuwa na tashwishi kuhusu hatua kulegeza marufuku hiyo kwa hofu ya kuendeleza vita nchini Somalia.

Duru zinasema kuwa pande hizo mbili ziliweza kuafikia mwafaka kuhusu swala hilo, na kuondoa marufuku dhidi ya silaha ndogo ndogo na bado wamewekewa vikwazo dhidi ya silaha nzito.

Baraza hilo pia lilipiga kura kuongeza muda wa wanajeshi wa muungano wa Afrika wanaoshika doria nchini humo na kuwapa mwaka mmoja zaidi.

Serikali ya Hassan Sheikh Mohamud, imekuwa ikishinikiza marufuku hiyo kuondolewa. Aliingia mamlakani mwaka
2012 baada ya kuchaguliwa kwake kwenye uchaguzi wa kwanza tangu enzi ya rais, Mohamed Siad Barre.

Hata hivyo bado kutakuwa na vikwazo dhidi ya kuingiza silaha kadhaa nchini Somalia ikiwemo, makombora ya masafa marefu, bunduki za viwango vikubwa na kadhalika.

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International,limesema kuwa hatua hiyo imekuja mapema na kuwa bado kuna haja ya kuweka vikwazo ili kuzuia silaha kuwa mikononi mwa watu wasiostahili.

Marufuku ya kununua silaha kwa Somalia iliwekwa mwaka 1991 baada ya kuporomoka kwa serikali ya aliyekuwa rais Siad Barre mwaka 1991 na kisha kuzuka vita vibaya kati ya mababe wa kivita kwa misingi ya koo.

No comments:

Post a Comment