Dar es Salaam. Bunge limeingia katika mzozo
mwingine na Chadema baada ya kudaiwa kutoa ripoti polisi likitaka
wabunge 28 wa upinzani waitwe ili wahojiwe katika Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na fujo zilizotokea bungeni
Februari, mwaka huu.
Hata hivyo, chama hicho kikuu cha upinzani
kupitia kwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, kimepinga
hatua hiyo kikisema kamati hiyo haipo kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya
113(7) kwa kuwa imemaliza muda wake tangu Februari 8, mwaka huu na Spika
hajaunda nyingine.
Hata hivyo, madai hayo ya Lissu yamepingwa
vikali na Naibu Spika, Job Ndugai ambaye amesema kamati hiyo pamoja na
nyingine mbili za Uongozi na ile ya Kanuni zinatambulika mpaka
zitakapoundwa nyingine... “Hizo tatu ni ‘ongoing’ (zinaendelea)
zisipokuwapo, basi Bunge hakuna.”
Mvutano huo ni wa pili katika siku za karibuni
baada ya ule uliotokea katika Kikao cha Bunge la Februari baada ya
Wabunge wa Chadema kuzua tafrani zilizosababisha kukatishwa kwa kikao
kimoja cha Bunge hilo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Lissu alisema
yeye na wabunge wenzake wapatao 28 watafika mbele ya kamati hiyo lakini
wamekubaliana kuwa hawako tayari kuhojiwa nayo.
Mbali ya Lissu, jana
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara mjini
Musoma alisema wabunge wa chama chake hawatakwenda kuhojiwa na kamati
hiyo.
Lissu alisema njia iliyotumika kuwaita mbele ya kamati hiyo kwa kupitia polisi ni kinyume na utaratibu.
“Utaratibu
uliotumika ni haramu kwa kuwa polisi ndiyo wametumika kutujulisha
kwamba tunatakiwa tufike mbele ya kamati hiyo, kutumiwa ujumbe wa polisi
si sawa kwani utaratibu wa Bunge unajulikana,” Lissu alisema na
kuongeza:
“Kamati iliposema bungeni kuwa mimi na
wenzangu watatu ni vinara wa fujo ilituhukumu tayari, hivyo kisheria
wale wengine waliobaki walikuwa hawana makosa kwa mujibu wa sheria
zetu.”
Ilidaiwa kwamba Ofisi ya Bunge iliiandikia
Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi kutaka kuwaelekeza makamanda wake
kufikisha taarifa hizo.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema hakuwa na taarifa hizo na kuahidi kufuatilia.
Alipoulizwa kuhusu wabunge hao kuitwa kwa
kutumia polisi, Ndugai alisema hakuwa na taarifa hiyo na kuelezea
wasiwasi kwamba suala hilo limefikia hatua hiyo.
“Sidhani kama
imefikia huko (kutumia polisi kuwaita wabunge), kwani kamati ina
utaratibu wake wa kumwita mtu yeyote hata asipokuwa mbunge, kwa kweli
sijui na sifikirii kama watakuwa wamefikia huko,”alisema Ndugai.
Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kumpigia simu Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari kumpa wito wa kufika mbele ya kamati hiyo ya
Bunge na pia alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karatu (OCD), kuwapa
taarifa Mbunge wa Karatu, Israel Natse na Mbunge wa Viti Maalumu Cecilia
Paresso.
No comments:
Post a Comment