Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa
Polisi Zanzibar imesambaza picha ya mchoro ya
mtu anayedaiwa kumuua kwa kumpiga risasi, Padri Evaristus Mushi wa
Kanisa Katoliki mwezi uliopita.
Mchoro huo uliosambazwa kwa vyombo
vya habari jana na Ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, unamwonyesha
mtu aliyevaa kofia ya baraghashia.
Katika taarifa hiyo, Polisi ilisema kwamba mtu
atakayesaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo atazawadiwa Sh10 milioni...
“Mwananchi yeyote ambaye anamjua mtu aliyefanana na mchoro huo atoe
taarifa katika kituo chochote cha polisi na iwapo atakuwa ndiye mhusika
atapewa zawadi hiyo.”
Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa
hakupatikana jana kutoa maelezo zaidi juu ya hatua hiyo, lakini Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Haji Abdallah Hanna
alithibitisha kuwa taarifa hiyo imetoka Polisi.
Hata hivyo, Kamanda Hanna hakuwa tayari kutoa
ufafanuzi zaidi kwa maelezo kwamba upelelezi wa suala hilo unafanywa na
Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
Kuuawa kwa Padri Mushi lilikuwa tukio la tatu
kubwa la kushambuliwa kwa viongozi wa dini baada ya kumwagiwa tindikali
kwa Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhil Soraga na kupigwa risasi Padri
Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki.
Kitendo cha kutoa picha hiyo ni hatua kubwa katika upelelezi wa kifo cha Padri Mushi, ambacho kilitikisa visiwani Zanzibar.
Pia
hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kutua kwa maofisa wa Shirika la
Upelelezi la Marekani (FBI), ambao wanasaidiana na Polisi wa Tanzania
kuchunguza tukio hilo.
FBI wana kawaida ya kutumia picha na michoro pale wanapochunguza matukio makubwa ya uhalifu au ugaidi.
Mathalan, pale wanapotaka kupeleleza kwa
kutumia michoro ya sura za wahalifu wasiowafahamu, hufanya mahojiano na
watu waliokuwapo kwenye tukio na wakati wakipata maelezo hayo, huwa na
wataalamu wao wa uchoraji karibu ili kujaribu kutengeneza sura za watu
wanaotafutwa.
FBI walikuja nchini baada ya kualikwa na
Serikali ya Tanzania ambayo inataka kujua chanzo cha vitendo
vinavyotishia maisha ya viongozi wa dini huko Zanzibar.
Hii ni mara ya pili kwa FBI kufanya kazi
Tanzania baada ya mwaka 1998 walipokuja kuchunguza kulipuliwa kwa bomu
kwa ubalozi wa Marekani.
No comments:
Post a Comment