Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta
amewashukuru wananchi pamoja na Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kushinda
nafasi hiyo huku akiahidi kuijenga upya Kenya.
Uhuru amesema ataweka kipaumbele kwenye
kutunza rasilimali za nchi na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi wote,
pia kuwawezesha wanawake na vijana.
Katika hotuba yake aliyotoa muda
mfupi baada ya kutangazwa mshindi jana, Kenyatta alisema anawashukuru
wagombea alioshirikiana nao katika mchakato wote wa uchaguzi na
kuwakaribisha kuungana.
“Nawashukuru wagombea wenzangu wote kwa
kujitolea kwa moyo kushiriki katika kinyang’anyiro hiki kwa kuwa jambo
hilo limezidi kuonyesha demokrasia iliyopo nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa anaahidi kushirikiana vyema na
wagombea hao akiwamo Raila Odinga kwa ajili ya kuijenga upya nchi yao,
akiwakaribisha na kuwataka waondoe kinyongo kutokana na ushindi
alioupata.
“Tulianza zoezi zima kama timu na
nitashirikiana nanyi kama timu, ikiwamo kuhakikisha tunafuata yale yote
yaliyopo kwenye katiba hususan kuhakikisha kila mwananchi anapata haki
yake anayostahili.”
Kiongozi huyo pia aliwashukuru watu mbalimbali
waliofanikisha uchaguzi huo kwenda vyema ikiwamo vyombo vya habari
katika nchi hiyo ambavyo vilikwenda sambamba katika kuripoti matukio
yote ya uchaguzi, pamoja na vyombo vya usalama vilivyosimamia chaguzi
hizo.
“Usalama bado ni tatizo katika nchi yetu,
lakini ningependa kuvishukuru vyombo husika kwa kufanikisha tunavyozidi
kuendelea suala hilo litakuwa vizuri,” alisema.
Uhuru alieleza
hayo baada ya Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) kumtangaza kuwa
mshindi katika uchaguzi uliofanyika Machi 4 akiwa amegombea kwa tiketi
ya muungano wa Jubilee.
Uhuru aliibuka mshindi katika uchaguzi
huo kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizohitajika ili kupata
ushindi kulingana na mahitaji ya Katiba Mpya ya nchi.
Matokeo
yaliyotolewa na IEBC yanaonyesha kuwa Uhuru alipata kura 6,173,433
ambazo ni asilimia 50.07 huku mpinzani wake Raila Odinga akipata
5,340,546 ambazo ni asilimia 43.28.
Kwa ushindi huo, Uhuru
amepata idadi kubwa ya kura inayohitajika na Katiba Mpya ambayo ni zaidi
ya asilimia 50+1 na kuzuia uwezekano wa kurudiwa kwa uchaguzi.
Uhuru
pamoja na mgombea mwenza wake, William Ruto wamepata ushindi huo huku
wakiwa wanakabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu
(ICC) kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Ushindi
huo umepingwa na mpinzani mkuu wa Uhuru, mgombea urais kupitia muungano
wa Cord, Raila Odinga ambaye amesema ‘kamwe hawatayatambua’ na kuahidi
kuyapinga mahakamani.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa
kwa matokeo hayo, Odinga alisema anajiandaa kwenda mahakamani kupinga
matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru.
Odinga, aliwaambia
waandishi wa habari kuwa matokeo yaliyotolewa na tume hiyo yalikuwa
yamehujumiwa hasa baada ya kutokea hitilafu katika mitambo ya
elektroniki iliyokuwa inatumiwa katika shughuli hiyo.
“IEBC
imerudia makosa yaleyale ya uchaguzi mkuu wa 2007, kwa kuwa tuna
mahakama tunayoiamini tunaomba watu wetu watulie hadi mahakama
itakapotoa uamuzi. Wenzetu pia wajiepushe na aina yoyote ya ghasia,”
alisema.
Alisema kwamba hana tatizo la kushindwa iwapo ameshindwa
kihalali, lakini kwa matokeo haya ana jukumu kubwa la kupinga
mahakamani ili kulinda mahitaji na heshima ya wapiga kura.
Aidha, alisema kugoma kwa mitambo hiyo kulichanganya mambo katika shughuli ya kuhesabu kura.
Alisema
kuwa baada ya kutokea hitilafu, kura alizokuwa amepata katika maeneo
bunge ambayo ni ngome zake, ziliongezwa kwenye hesabu ya kura za
muungano pinzani wa Jubilee.
Siku moja kabla ya kutangaza matokeo
hayo, IEBC ilikiri kuwa matatizo yaliyosababishwa na mtambo wake wa
kupeperusha matangazo ni pamoja na kuongeza mara nane kura
zilizoharibika.
Baadhi ya wananchi walieleza kuwa na wasiwasi
kuhusu idadi kubwa ya kura zilizoonekana kuharibika, kwani zilikuwa kura
zaidi ya 300,000 ambapo kwa sasa zimepungua mpaka kufika idadi ya kura
80,000, baada ya kuhakiki kura hizo kwa mara ya pili.
Pingamizi lao lilikataliwa
Mapema
wiki hii, wakati shughuli ya kuhesabu kura za urais ilikuwa inafanyika,
wanaharakati walifungua kesi mahakamani kutaka uchaguzi usimamishwe
kutokana na hitilafu mbalimbali zilizotokea , lakini mahakama kuu
ilitupilia mbali kesi yao ikisema kuwa haina uwezo wa kufanya uamuzi
katika kesi hiyo, na kuwa ni mahakama ya juu zaidi pekee inayoweza
kusikiliza kesi hiyo.
Matokeo hayo na mivutano yote iliyopo kwa
sasa vinatokea baada ya siku tano tangu Wakenya kupiga kura kuchagua
rais, magavana, maseneta, wabunge, wawakilishi wanawake na wawakilishi
wodi.
Tume ya uchaguzi ilichukua zaidi ya saa tano kukagua hesabu ya kura hizo kabla ya kutangaza matokeo hayo jana mchana.
Kwa
mujibu wa maagizo yaliyopo katika Katiba Mpya ya nchi hiyo, mshindi wa
uchaguzi anatakiwa kutangazwa iwapo tu ametimiza masharti ya kikatiba ya
kutangazwa kuwa rais wa nne wa Kenya.
Pamoja na ushindi wa kura kwa zaidi ya asilimia 50 lazima awe ameshinda asilimia 25 katika nusu ya kaunti zote 47 nchini Kenya.
No comments:
Post a Comment