Mauaji ya kinyama

  Watatu wauawa kwa mapanga, nane hoi

Mkazi wa Kijiji cha Bitale, Dotto Issa (24), akiwa amelazwa wodi namba 5 ya Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni kwa matibabu ya majeraha baada ya yeye na wenzake saba kucharangwa mapanga na mtu anayesadikiwa kuwa na ugonjwa wa akili.

Mkazi wa Kijiji cha Bitale katika Wilaya ya Kigoma, Stanford Richard (30) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine wanane kwa kuwacharanga mapanga.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi baada ya mtuhumiwa huyo kuvamia nyumba za majirani zake na kumshambulia kila mtu aliyemuona kwa panga.

Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Dismas Kisusi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliouawa kuwa ni Rudia Richard (70), Ezema Razalo (65) na Sebastiani Julius (22), wakazi wa kijiji hicho.

Kisusi aliwataja waliyojeruhiwa kuwa ni Pendo Jumbe (35), Jumbe Budio (50), Richard Manase (60), Lith James (55), Shukrani Manase  (30), Doto Issa (24) , Remmy Kagiye (8) na Seraphina  Mayage (65),  wakazi wa kijiji kicho.

Alisema watu hao ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni, wamepata majeraha makubwa na hali zao siyo za kuridhisha.

Kisusi hakueleza sababu za mauaji hayo, lakini alisema kuna taarifa zinadai mtuhumiwa huyo ni mgonjwa wa akili. Mmoja wa majeruhi hao, Dotto, aliiambia NIPASHE wodini hapo kuwa mtuhumiwa huyo wanaishi naye jirani,  alishutuka akimcharanga kwa panga wakati anapika chakula nyumbani kwake.

Dotto alisema baada ya kucharangwa mapanga, mama yake mzazi, Rudia Richard,  alikwenda kumsaidia, lakini naye alicharangwa kwa panga na kufa.

Habari zinadai mtuhumiwa huyo alianza kumshambulia mama yake mzazi, Seraphina  Mayage na kumjeruhi.

Kwa mujibu wa Kisusi, mtuhumiwa huyo anatajia kufikishwa mahakamani leo kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk. Leonard Subi, alithibitisha kupokelewa maiti watatu hospitalini hapo ambao ni mwanaume mmoja  na wanawake  wawili na majeruhi hao ambao wamelazwa wodi namba tano na saba.

Dk. Subi alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment